Zinazobamba

Mkurugenzi wa Tgnp akisoma tamko la wanamtandao wa FEMACT kuhusu wanawake kupewa nafasi ya kuongoza vyombo vya dola kwa kupewa nafasi za uwairi mkuu, speaker wa bunge na kadhalika. mchakato ulivyo sasa unaminya uhuru wa wanawake kujiingiza katika harakati za uchaguzi.




Sehemu ya wanahabari wakifuatailia taarifa hiyo ya wana FEMACT.
 TAMKO LAO HILI HAPA.

Wakati joto la uchaguzi kuelekea Oktoba 25 likizidi kupanda, kuna kila dalili kuwa msingi mkuu wa Demokrasia ya uchaguzi ambao ni ushiriki wa kila raia katika mchakato huo unalegalega. Pamoja na maandalizi yanayoendelea kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, yapo mambo kadhaa ambayo yanahitaji kuwekwa sawa. FemAct imeamua kuchangia katika kuleta suluhu ya baadhi ya mambo hayo kwa kuchambua changamoto zilizopo na kupendekeza suluhu.
 Taarifa hii ni sehemu ya mchango huo wa Mtandao wa FemAct. Uchaguzi ni suala la kikatiba. Kwa mujibu wa ibara ya 21(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kila raia anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi. Aidha, ibara ya 8 inabainisha kuwa Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote ya nchi na kwamba serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.
Kiutendaji, njia kuu kwa wananchi kukasimisha mamlaka na madaraka yao ni kwa kuchagua viongozi wao kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa miaka yote ya uhai wa taifa letu tangu uhuru na kwa uwazi zaidi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Uchaguzi ndiyo njia kuu kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa serikali kutekeleza mipango ya maendeleo katika kipindi cha uongozi kinachowekwa kikatiba na kisheria. Tanzania inaingia katika uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi kwa mara ya nne mwaka huu uchaguzi wa kwanza ukiwa ule wa mwaka 1995. Pamoja na miaka 20 ya demokrasia ya Vyama vingi, ukuaji wa usawa wa Kijinsia bado unasuasua.
 Zipo dalili kuwa wanawake, vijana na Watu wenye Ulemavu wanakwamishwa kushiriki na kushindana kutokana na vikwazo mbalimbali. Kwa mfano, vyama vya siasa, ambavyo ndiyo njia pekee ya kuwania uongozi wa kuchaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 39 (1) (c) na ibara ya 69 (1) (b) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, vimetawaliwa na mifumo kandamizi ikiwemo mfumo dume ndani ya taasisi hizo ukiwa kikwazo kikuu kwa ushiriki wa makundi hayo kama wagombea wa uchaguzi.

 Kati ya vyama takribani 24 vyenye usajili halali, ni chama kimoja tu cha ACT kina mwanamke kama Mwenyekiti wa Chama, huku vingine viwili vikiwa na makatibu wakuu wanawake vikiwemo ADC na DP.
Kwa vyama vingine, safu nzima ya uongozi ndani ya chama kuanzia mwenyekiti hadi wajumbe wa vikao muhimu vya chama zimeshikiliwa na wanaume.
 Hii inapelekea ukakasi na kuminya sauti za wanawake katika maamuzi mengi ikiwemo uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi. Pamoja na juhudi hizi kwa baadhi ya vyama FemAct inatoa angalizo kuwa uteuzi wa wanawake usiwe kwa kuzingatia idadi tu bali pia kuwe na fursa ya kushiriki kikamilifu katika kutoa mamuzi kwenye ngazi zote.
Mtandao kupitia mashirika wanachama imekua ikifanya mafunzo kwa watangaza nia na viongozi wa kisiasa kuhusu masuala ya uongozi na demokrasia. Mafunzo hayo yaliwalenga wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika tamthmini ya awali, hasa baada ya mchakato wa ndani ya vyama kuanza, makundi hayo yamekua yakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na lugha za matusi na za kudhalilisha, dharau na kejeli, ukatili wa kijinsia na wakati mwingine rushwa ya ngono, matumizi makubwa ya fedha n.k.
Hali hiyo inaashiria kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwa makundi hayo jambo linaloweza kusababisha kukata tamaa kwa makundi hayo.

Kwa hali inavyoonekana mwaka huu, ni dhahiri kuwa idadi ya wanawake watakaoteuliwa kupeperusha bendera za vyama vyao katika nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani itakuwa ndogo sana kwa sababu ya visingizio kadhaa. Ndiyo maana, uamuzi wa Chama cha Mapinduzi kumsimamisha mwanamke katika nafasi ya mgombea mwenza wa urais kitendo ambacho kinatoa hali inayofanya kuwepo uwezekano wa kuwa na Makamu wa Rais Mwanamke Tanzania ni jambo la kupongezwa, tulitarajia na vyama vingine vya siasa kuzingatia usawa wa kijinsia katika uteuzi wao. Bila kujali kama mwenza huyo na mgombea wa chama chao watashinda au la, historia iliyowekwa itabaki vizazi na vizazi ikionesha jinsi Tanzania ilivyofikia utayari wa kuwa na Makamu wa Rais mwanamke. FemAct inaendelea kudai kama ilivyokua tangu mchakato umeanza, kuwa chama chochote kitakachoingia madarakani kihakikishe kuwa moja kati ya nafasi kuu tatu yaani nafasi ya uraisi, makamu wa raisi na waziri mkuu ishikiliwe na mwanamke. Kwa upande wa Wanawake ambao ni asilimia 50 na Vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 kama wapiga wakuu katika uchaguzi, hamasa ya wanawake kujitokeza imeonekana kuzidi kupanda. Katika zoezi la uandikishaji wapiga kura linalokamilishwa hivi sasa, wanawake wengi walionekana katika misururu mirefu kuanzia alfajiri huku wengi wakiwa wamebeba watoto. Hata katika uchaguzi uliopita mwaka 2010 ambapo ni asilimia 42% tu ilijitokeza kupiga kura kumchagua Rais wa Tanzania, takwimu zinaonesha kuwa wengi katika hao walikuwa ni wanawake, vijana na wasichana. Hamasa kubwa iliyoonekana wakati wa uandikishaji inaashiria kuwa mwitikio wa jumla katika uchaguzi wa mwaka 2015 unaweza ukawa mara mbili ya mwaka 2010. Hili ni jambo la afya kwa uchaguzi na ukuaji wa Demokrasia nchini. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa maandalizi yaliyobaki kuelekea siku ya upigaji kura yanahakikisha kuwa kunakuwa na hali ya amani, utulivu na wezeshi kwa mazingira rafiki kuwezesha wananchi kupiga kura. Kwa hatua zilizokamilika mfano uteuzi ndani ya vyama umeonesha dalili za uvunjifu wa amani hivyo tunatoa angalizo kwa serikali, vyama vya siasa na wapiga kura kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika kwa amani na utulivu kwani makundi yanayoathirika zaidi katika uvunjifu wa Amani ni wanawake,watoto na watu wenye ulemavu. Kuhusu uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi, Mtandao unaona changamoto kubwa mbili. Kwanza, matumizi mabaya ya fursa ya viti maalum vya wanawake katika nafasi ya ubunge na udiwani, ubunge na uwakilishi; pamoja na matumizi makubwa mno ya fedha katika uchaguzi kiasi cha kuwanyima fursa wanawake, vijana na wasichana kumudu kugharamia michakato ya kugombea katika uchaguzi. Taarifa kwamba baadhi ya vyama vimekuwa vikiwazuia wanawake kugombea nafasi za viti vya majimbo na udiwani kwa kisingizio kuwa wao wasubiri viti maalum ni za kusikitisha sana. Dhana ya viti maalum ni kuwezesha kunyanyua idadi ya wanawake wanaoshiriki katika siasa. Aidha, viti maalum vinapaswa kuwa ni nafasi za kujengea uwezo wanawake na wasichana na sio kuvifanya kuwa vya kudumu. Viti maalum bila juhudi nyingine za kupanua fursa za wanawake kushitriki Siasa ni sawa na kazi bure. Pia, mifumo ya kuwezesha wagombea kufadhili shughuli za uchaguzi inapaswa kuwa jukumu la vyama na siyo mgombea mmoja mmoja. Hii itapunguza uwezekano wa wagombea kuumiza vichwa kufikiria wapi wapate fedha za kufanyia maandalizi ya uchaguzi ikiwemo kuendesha kampeni. Mfumo wa sasa ambapo rasilimali za uchaguzi ni jukumu binafsi la mgombea unashawishi na kulea wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi. 3 Jambo jingine la kuliangaliza taifa wakati huu ni kuhusu siasa nyepesi za kuhamahama vyama, sambamba na kukosekana kwa mfumo mbadala wa wagombea huru. Hili nalo limekuwa kikwazo kwa wanasiasa makini ambao wangependa kugombea bila kudhaminiwa na vyama vya siasa. Kuwepo kwa wanasiasa wanaohama vyama baada ya majina yao kuenguliwa katika vyama vyao kupitia kura za maoni, licha ya kuwa ni haki yao kufanya hivyo, ni bora vyama vya siasa vikahakikisha kuwa vinakuwa na utaratibu wa kuchuja watu wanaokimbilia katika vyama vyao katika misingi ya kiuwajibikaji na uongozi bora nas si kwa maslahi binafsi. Kutokana na hili, kunahitajika elimu ya uraia inayoweka bayana misingi mikuu ya demokrasia ya uchaguzi ambapo anayegomea anapaswa kujua kuwa kunakushinda au kushindwa na kuwa tayari kukubali matokeo. Vinginevyo, dhana nzima ya demokrasia inakuwa haina maana kwa kuwa wanaoshindwa wanakuwa chanzo cha migogoro na fujo kiasi cha uwezekano wa kutoweka kwa amani.


 Imetolewa, Lilian Liundi Abdullah Othman Mkurugenzi Mtendaji, TGNP Mtandao Mwenyekiti – FEMACT Mratibu, FEMACT Kwa Niaba ya; 1. Life Skills Association (LISA) 2. Tanzania Education Network (TENMET) 3. Tanzania Citizens’ Information Bureau (TCIB) 4. Journalists Environmental Association of Tanzania (JET) 5. Binti Leo 6. African Youth 7. African Life Foundation 8. Pwani - DPA

Hakuna maoni