RAIS KIKWETE KUBURUZWA MAHAKAMA YA THE HAGUE,UKAWA WAMUONYA,WASEMA ATAJUTA SOMA HAPO KUJUA
Viongozi wa Ukawa pichani |
Na Fredy Azzah, Zanzibar
UMOJA wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamemuonya Rais Jakaya Kikwete, wakisema ndiye
mwenye dhamana ya kulinda usalama wa wananchi na akiendelea kutumia vibaya
vyombo vya dola, Novemba mwaka huu watamburuza Mahakama ya Kimataifa ya Makosa
ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi.
Kauli hiyo
ilitolewa jana mjini Zanzibar na viongozi wa Ukawa, katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Uwanja wa Kibanda Maiti wenye lengo la kutafuta wadhamini kwa
mgombea urais wa umoja huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa.
Akizungumza
katika mkutano huo jana mjini hapa Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalimu Seif Sharif Hamad, alisema CCM wanahubiri
amani wakiwa majukwaani lakini wakishuka wao ndio wa kwanza kuivunja.
“Kama kuna
watu wana nidhamu ni watu wa Ukawa, Mbeya, Arusha, watu wawalikuwa wanasubiri
kwa amani, polisi wanapiga mabomu, wao ndiyo wanaleta tensheni katika nchi,
siyo wafuasi wa Ukawa.
“Namwambia
Kikwete (Rais), atimize wajibu wake, akifanya vinginevyo watakwenda ICC,
Kikwete ondoka kwenye nchi ikiwa salama kama ulivyokabidhiwa ikiwa salama,
wananchi wakukumbuke kuwa umeiacha salama,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni
mgombea urais wa Zanzibar kupitia umoja huo.
Mbatia
Akihutubia
katika mkutano huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amewataka
wanasheria wa Ukawa, kuanza kuandika matukio yote yanayotokea nchini kwa sasa
ili wayawasilishe katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC).
“Tumeshawaagiza
mawakili wetu waandike matendo yote maovu yanayofanywa, waandikie ICC, wapeleke
nakala kwa mabalozi wote ili Fatou Bensouda (Mwendesha mashitaka Mkuu wa ICC)
aje aanze kuangalia yanayofanyika hapa.
“Tumechoka
kudanganywa, tumechoka kuibiwa ushindi wetu, mwaka huu tunasema, hapana,
hapana. Walikuja kuandikisha watu wao hapa na baada ya Ukawa kutangaza
mgombea watu wao wote sasa wamehamia Ukawa,” alisema Mbatia.
Alisema
Watanzania kwa sasa wanataka mabadiliko kwa asilimia 99, na jeshi la polisi
likiendelea kuvunja amani, Novemba mwaka huu watakwenda ICC.
Juma Duni
Naye
Mgombea Mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, alisema ni bahati mbaya sana
watawala wanadhani kutumia mabavu kutawasaidia kubaki madarakani jambo
ambalo kwa sasa haliwezi kutokea.
Lowassa na Kingunge
Kwa upande
wake Lowassa alisema kitendo cha CCM kumvua wadhifa wake Kamanda wa UVCCM,
Kingunge Ngombale Mwiru kwa sababu tu mwanasiasa huyo mkongwe alitumia
demokrasia kueleza hisia zake ni kuchuma laana.
Alisema
Kingunge ambaye ni mmoja wa waasisi wa TANU na CCM, alikuwa amebaki kama mfano
ndani ya chama hicho kutokana na historia yake.
“Nianze
kwa kueleza masikitiko yangu kwa hatua aliyochukuliwa mzee Kingune jana (juzi),
mzee huyu alibaki kama kielelezo cha TANU, yote yaliyomfika ni kutokana na
kutoa maoni yake, hatua waliyochukua ni laana… laana ya Kingunge itawapata,”
alisema Lowassa.
Lowassa
alisema amefika Zanzibar kuomba wadhamini kwa sababu anataka kupambana na
umaskini na anauchukia.
“Nilivyoona
sipewi nafasi ya kupambana nao huko CCM nikaondoka, niliondoka kwa maneno ya
Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa) kwamba Watanzania wanataka mabadiliko,
wasipoyatapa ndani ya CCM watayapata nje ya CCM, naifahamu Tanzania,” alisema
Lowassa.
Akizungumzia
kuhusu Katiba mpya, alisema tangu wakati wa G55 alikuwa ni muumini wa Serikali
tatu na kwamba hata kwenye Tume ya Jaji Wairioba alisema hilo.
“Nilisema
nataka Serikali tatu lakini Muungano ubaki, muungano huu siyo wa uongozi ni wa
watu. Nataka Muungano imara ndani ya watu imara, Serikali tatu
inayozingatia mahitaji ya watu sawa ya watu wa Zanzibar na wale wa Bara,”
alisema.
Mgeja
Aliyekuwa
mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja,
alisema Ukawa ni meli iliyosalama na itawavusha Watanzania kwenda kwenye maisha
yenye matumaini.
Alisema
Watanzanai wanataka mabadiliko na ndiyo maana aliamua kuachana na chama chake
cha awali ili awe sehemu ya ukombozi.
“Ndiyo
maana nikaondoka CCM… tatizo la Chama Cha Mapinduzi ni mfumo ambao unatesa
Watanzania. Tumejitahidi sana kuuguza mgonjwa, lakini ikifika mahali unauguza
mgonjwa haponi ujue kuna tatizo kubwa,” alisema Mgeja.
Alisema
moja ya matatizo makubwa ya chama chake cha awali ni watu kutotaka kuambiwa
ukweli.
“Kingunge
(mmoja wa waasisi wa CCM na TANU), juzi kwa sababu ya kusema ukweli,
wamemfukuza kwenye ukamanda wa UVCCM, Mzee Moyo (Hassan Nassor ), naye kwa
kusema ukweli yakampata yaliyompata na mimi kwa kusimamia ukweli mwaka juzi kwa
kutaka nafasi ya uenyekiti itenganishwe na urais wakataka kunichinja,” alisema.
Alisema
licha ya kuwa Katiba ni moja ya mahitaji makubwa ya wananchi, jambo hilo
halijawahi kuwa ajenda ya CCM.
“Namuomba
Kinana (Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman) atoe walau muhutasari wa lini CCM
iliwahi kujadili suala la Katiba, lakini ilipoanza presha ya msukumo wa Katiba
kutoka Chadema, CUF ilibidi Rais (Jakaya Kikwete) aufuate,” alisema.
Alisema
baada ya Ukawa kuona mambo hayaendi, wakaamua kujitoa kwenye Bunge Maalumu la
Katiba na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan,
amepewa zawadi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa CCM.
Mbowe
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema ni
vema viongozi wakavitumia vyombo vya ulinzi na usalama kwa masilahi ya watu
wote na siyo kwa chama kimoja.
“Tunavihakikishia
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kulinda wananchi kwa sababu hata
tukiunda serikali yetu, hatutavipeleka likizo, vitaendelea na jukumu lake.
“Hawana
sababu ya kuwa na hofu, wataingiwa hofu wanaounda vikundi vya kutesa
Watanzania, tunawataka viongozi wetu watumie vizuri majeshi yetu, siyo mali
yao, wasitumike kubagua wananchi siyo kulinda chama kimoja cha kisasa” alisema.
Alisema
Zanzibar ni lulu ambayo dunia nzima inaitolea macho lakini Wazanzibari hawaioni
kwa kuwa hawajafaidika.
“Zanzibar
inajulikana kuliko hata Tanzania bara, ni lulu inayotakiwa na dunia nzima,
lakini wananchi wengi wa Zanzibar hawajui thamani ya Zanzibar kwa sababu maisha
yao hayafanani na thamani ya Zanzibar.
Umeme
Tokea saa
3.45 asubuhi umeme ulikatika katika mji mzima wa Unguja na kukwamisha shughuili
kadhaa za uzalishaji mali huku watu kadhaa wakishindwa kufuatilia mkutano wa
Ukawa hadi uliporejea majira ya saa 11.45 jioni hali iliyoibua hisia na
kueleza kukatika huko ni kutokana na sababu za kisiasa.
Katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Zanzibar,
Lowassa alipokewa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, Mjumbe wa
Braza Kuu la CUF Jussa Ladhu, Waziri wa zamani wa SMZ Mansoor Yussuf Himid na
msafara wake kupita katika barabara kuu ya Nyerere hadi eneo la mkutano.
Majimbo Ukawa hadharani
Vyama
vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) vimetoa orodha ya mgawanyo wa
majimbo 203 ya Ubunge Tanzania bara.
Katika
mgawanyo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kitasimamisha
wagombea katika majimbo 137 kikifuatiwa na Chama cha Wananchi(CUF) majimbo 49,
NCCR Mageuzi 14 na NLD ikiambulia majimbo matatu huku majadiliano yakiendelea
katika majimbo 12.
Katika
mgawanyo huo, Chadema imechukua majimbo yote ya mikoa ya Arusha, Mara,
Shinyanga, Geita, Njombe, Rukwa, Manyara, Katavi na Singida huku CUF ikichukua
majimbo yote ya Mkoa wa Lindi.
Wakati
NCCR Mageuzi ikijipatia majimbo sita ya Mkoa wa Kigoma, Chadema wataweka mgombea
katika majimbo ya Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini.
Chama cha
NLD kinachoongozwa na Dk. Emanuel Makaidi kimepata majimbo matatu ya Lulindi,
Masasi na Ndanda katika mkoa wa Mtwara kikigawana na CUF majimbo yaliyobaki.
Katika
Mkoa wa Simiyu, CUF imeambulia Jimbo la Busega huku majimbo mengine
yakichukuliwa na Chadema.
Katika
Mkoa wa Dodoma, majimbo ya Mtera na Kibakwe yameenda NCCR Mageuzi huku
Kongwa, Bahi, Chilonwa na Dodoma Mjini yakienda Chadema na yaliyobaki yatakuwa
ya CUF.
Katika
Mkoa Kagera, Jimbo la Bukoba Mjini limechukuliwa na Chadema, Vijijini CUF,
Nkenge na Ngara yakienda NCCR Mageuzi na yaliyobaki yamechuliwa na Chadema.
Mkoa wa
Mbeya, majimbo 11 yamechukuliwa na Chadema huku NCCR Mageuzi ikipata jimbo moja
la Ileje.
Katika
Mkoa wa Dar es Salaam, majimbo matano ya Ubungo, Kawe, Ukonga, Ilala, na
Kibamba yamechukuliwa na Chadema, huku CUF ikisimamisha wagombea katika majimbo
matatu ya Kinondoni, Temeke na Mbagala. Majimbo mawili ya Segerea na Kigamboni
yakiendelea na mashauriano.
Mkoani Iringa,
Chadema imechukua majimbo yote kasoro Jimbo la Mufindi Kusini lililochukuliwa
na NCCR Mageuzi.
Katika
Mkoa wa Tabora, majimbo sita ya Nzega Mjini, Igunga, Urambo, Ulyankulu, Sikonge
na Manonga yamekwenda Chadema huku mengine sita yaliyobaki yakichukuliwa na
CUF.
Majimbo
nane ya Mkoa wa Tanga yamechukuliwa na CUF huku manne ya Kilindi, Muheza
Korogwe na Korogwe Mjini yakienda Chadema.
Mkoani
Morogoro, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na Kilosa yamechukuliwa na CUF na
yaliyobaki yote yamekwenda Chadema.
Katika
Mkoa wa Pwani, majimbo matatu ya Chalinze, Kibaha Mjini na Vijijini yameenda
Chadema na yaliyobaki yamekwenda kwa CUF.
Mkoa wa
Ruvuma, Chadema imepata viti vinne vya Peramiho, Mbinga Magharibi, Mashariki,
Madaba na Songea Mjini huku CUF ikichukua majimbi ya Tunduru Kusini, Namtumbo
na Tunduru Kaskazini na NCCR Mageuzi wakipata kiti kimoja cha Mbinga Mjini.
Mkoa wa
Mwanza Chadema imepata majimbo saba na CUF imepata mawili ya Kwimba na Sumve.
Katika
Mkoa wa Kilimanjaro, Jimbo la Vunjo limechukuliwa na NCCR Mageuzi huku
yaliyobaki yakichukuliwa na Chadema.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu NCCR Mageuzi, Nderakindo Kessy,
alisema mgawanyo huo umezigatia vigezo walivyojiwekea katika umoja huo na hivyo
unapaswa kufuatwa na wagombea wote wa Ukawa.
Alisema
mambo ya msingi waliyozingatia katika mgawanyo huo ni matokeo ya ubunge ya
mwaka 2010 na kama jimbo lina mbunge ambaye anatokea katika umoja huo jimbo
hilo liliachwa katika chama husika hata kama mbunge huyo hataendelea.
“Kigezo
kingine ni matokeo ya udiwani ya mwaka 2010, kama chama kina idadi kubwa ya
madiwani katika jimbo hilo kinaachiwa na kikiwa na idadi kubwa ya wenyeviti wa
serikali za mitaa pia kinaachiwa,”alisema Kessy.
Kessy
alisema pia waliangalia mila na desturi ya eneo husika na sifa binafsi pamoja
na ubora wa mgombea aliyejitokeza.
“Ieleweke
kwamba, mgawanyo huo wa majimbo hautahusiana na mgawanyo wa kata za kugombea
udiwani mwongozo wa kuachiana kata ndio utumike katika maamuzi ya kuamua namna
ya kugombea katani,” alisema.
Naye Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo alisema watahakikisha Ukawa inashinda si kwa
kiti cha urais tu hata majimbo.
Akizungumza
katika hafla hiyo ya kubadilishana fomu, Naibu Katibu Mkuu wa NLD, Masudi
Makujunga alisema chama chake hakijaenea sehemu kubwa hivyo wanaweza kumudu
majimbo matatu.
Naye Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema waliochukua fomu nje na makubaliano
hayo viongozi wa vyama katika umoja huo wahakikishe hazirudishwi.
Akizungumzia
suala la kurudisha fomu siku mbili kabla ya tarehe husika, Mnyika alisema tume
ya uchaguzi itoe ufafanuzi kauli hiyo na iwe hiari.
habari kwa hisani ya Mwanahalisi oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni