Zinazobamba

MIGOGORO YA ARDHI ILIVYOTATURIWA KINONDONI


TYAH: TAARIFA YA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI KWA VYOMBO VYA HABARI
1.0 . Utangulizi:

Wilaya ya Kinondoni ambayo ina jumla ya wakazi wapatao milioni moja na laki tisa, ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 537 ni mojawapo ya wilaya hapa nchini ambazo zimekuwa na migogoro ya ardhi ya muda mrefu, ambapo moja ya sababu pamoja na nyinginezo ni kutokana na ongezeko la hali ya juu sana la wananchi linalosababisha mahitaji na presha ya kugombania ardhi  kuongeeka kwa kasi, kwa mfano; Mkoa wa Arusha una jumla kilomita za mraba 37,576 na idadi ya watu wapatao milioni milioni moja na laki sita huku Mkoa wa Ruvuma ukiwa na ukubwa kilomita za mraba 63,669 na idadi ya watu wapatao milioni moja na laki tatu. Kwa maneno mengine ni kwamba, Mkoa wa Arusha unaizidi kwa ukubwa wilaya ya Kinondoni kwa zaidi ya mara 69, Mkoa wa Ruvuma unaizidi kwa ukubwa wilaya ya Kinondoni kwa zaidi ya mara 118 wakati Mkoa wa Mara unaizidi wilaya ya Kinondoni kwa zaidi ya mara 40, lakini cha kushangaza kuliko vyote ni kwamba, wilaya ya kinondoni pamoja na udogo wake ina idadi kubwa ya watu kuliko mikoa yote niliyoitaji na mingine mingi ambayo sijaitaja.
2.0  Hali Halisi

Heshima aliyonipa Rais Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni kwangu niliitafsiri kama changamoto kubwa ya kuhakikisha nashughulikia kwa kina matatizo ya msingi ya wilaya hii, ambapo katika wakati wa sasa huwezi kutaja changamoto kubwa tatu za wilaya ya Kinondoni ukuaacha kutaja migogoro ya ardhi, kwa ufafanuzi zaidi unaweza kurejea hotuba yangu ya tarehe 28 mwezi wa pili wakati naanza kazi rasmi juu ya mambo niliyoyataja na vipaumbele nilivyoviweka.
Ushahidi wa ukubwa wa tatizo wa migogoro ya ardhi unaweza kudhibitika kupitia idadi ya malalamiko niliyoweza kuyapokea kwa kipindi cha miezi mitatu tu tangu nilipoanza mchakato wa kutenga kila siku ya ijumaa kusikiliza malalamiko ya ardhi na siku ya jumamosi kutembelea maeneo mbalimbal yanayolalamikiwa kwa ajili tu ya kujionea hali halisi, ndani ya miezi mitatu tu nimesikiliza na kufanyia kazi zaidi ya malalamiko 11,300 yatokanayo na migogoro ya ardhi. Huku nikibaini kuwa takribani kesi 1,600 zinazohusu masuala hayo hayo ya ardhi zinafunguliwa kwa kipindi cha kila mwezi mmoja katika Wilaya ya Kinondoni.
Kwa ufupi ni kwamba, kutoka kwenye jumla ya malalamiko zaidi ya 11,300 ya wakazi tofauti tofauti wa wilaya yangu niliyoyasikiliza, pamoja na kupitia taarifa hii ya idadi kubwa ya kesi za ardhi kwenye mahakama zetu ambayo nimekuwa nikiifuatilia kwa ukaribu sana, nimeweza kubaini sababu kadhaa za msingi zinazosimama kama chanzo cha migogoro ya ardhi inayoigubika wilaya ya Kinondoni.
2.1  Uwepo wa watendaji wasio waaminifu ambao kwa makusudi kabisa wanashiriki katika kugawa viwanja kwa mtu zaidi ya mmoja, huku wengine wakidiriki kusaidiana na matajiri wachache kudhulumu wananchi maskini wasiokuwa na uwezo wakutetea haki zao mbele ya vyombo vya sheria vilivyopo.

2.2  Kuongezeka kwa vitendo vya watendaji wa serikali wasio waaminifu ambao wamekuwa wakitumia nyadhifa zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa vinavyopelekea kuuzwa kwa maeneo ya wazi kwa watu binafsi na hivyo, kuwadhulumu wananchi kwa wingi wao, haki zao juu ya matumizi ya ardhi hizo. 

2.3  Kushamiri kwa vitendo vya utapeli wa ardhi ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya watu wachache wakiwemo madalali fake, uvamizi na uporaji wa maeneo kwa nguvu hasa pale kikundi fulani cha watu wanapogundua mmiliki halali wa eneo husika ana uwezo mdogo wakujisimamia na kufikisha mashitaka mahakamani.

2.4  .Uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu sheria za ardhi. Wananchi wengi hawafahamu sheria za umiliki ardhi zinasemaje, hivyo kujikuta mara nyingi wakiwa na matatizo kuhusu umilikaji wao au matumizi ya ardhi.

2.5  . Kuzolota na kuchukua muda mrefu kwa mashauri mbalimbali yahusuyo migogoro ya ardhi mpaka kumalizika kwake, jambo ambalo limekuwa

likiwakatisha sana tamaa baadhi ya wananchi kwenda kwenye vyombo vya sheria hata pale haki zao juu ya ardhi zao zinapochezewa. 

3.0 Hatua tulizochukua na Mikakati tuliyoweka;-

3.1  Wiki moja tu baada ya kuteuliwa nilianzisha utaratibu wa kupokea malalamiko ya migogoro ya ardhi ya wananchi na kuwasikiliza kwa kila siku ya ijuamaa hapa hapa ofisini kwangu, na kwa siku za jumamosi, mimi na kikosi changu maalumu nilichokiunda huwa tunatembelea maeneo husika yenye migogoro ili kujionea hali halisi na kusaidia katika kutoa majawabu ya muda mfupi na  ya kudumu. Kwa ufupi ni kwamba, kupitia utaratibu huu nimeweza kusikiliza malalamiko zaidi ya 11,300 pamoja na kutafuta jawabu stahiki kwa kila mgogoro.

3.2   Kuwashughulikia baadhi ya watendaji wa umma watakaobainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, uporaji na uvamizi wa maeneo ya wazi na rushwa kwenye sekta nzima ya ardhi na hivyo kuzalisha migogoro mipya. Na ninapozungumza hivi sasa, uchunguzi unaendelea kuwabaini watendaji mbalimbali waliohusika kama chanzo cha malalamiko yaliyopo.  

3.3   Kushughulikia changamoto mbalimbali za msingi zinazozikabili mahakama zetu na kuzifanya zichelewe kushughulikia kesi za ardhi zilizopo, kama si kuzikwamisha kabisa, na hivyo kutosaidia katika kumaliza migogoro ya ardhi ndani ya Kinondoni kwa wakati. Na katika eneo hili nimefanya mambo makubwa matatu; Kwanza, niliomba kwenye wizara husika kuondolewa kwa mahakimu ambao wamekuwa wakilalamikiwa sana na wananchi na nimefanikiwa kwenye hilo, kwani mpaka sasa kuna hakimu ameamishwa na tumeletewa hakimu mwingine mwenye historia ya uadilifu na maadili. Pili, Nimetumba maombi kwa wizara husika ili ituongezee mahakimu wawili ili tuwe na jumla ya mahakimu wane wanaosikiliza mashauri yahusuyo ardhi tu, ambapo wizara imekubaliana na maombi yetu na kutuahidi kutupatia mahakimu hao hivi karibuni. Na tatu, nimeshugulikia uongezaji wa wazee wa baraza la mahakama ya ardhi ya wilaya ya Kinondoni kutoka wazee watatu hadi kufikia sita ili kuongeza ufanisi na weledi katika kusikiliza mashauri mbalimbali.

3.4  Kuwajengea uwezo watendaji wa mabaraza ya ardhi ya kata ili waweze kufanya kazi zao za usuluhishi wa migogoro ya ardhi kwa mujibu wa sheria na kwa ufanisi zaidi, ili pamoja na faida nyinginezo, idadi ya migogoro inayokwenda mahakamani iweze kupungua na hivyo ufanisi wa chombo hiki muhimu cha kusimamia na kulinda haki ya kila mmoja wetu uongezeke zaidi.

3.5  Kama nilivyobadilisha mfumo mzima wa PF3, ndivyo ninavyofanya kwenye ardhi, napo nimechukua hatua mahususi ya kuchukua sehemu ya mshahara wangu na kuajiri jumla ya wanasheria watano watakaokuwa wanafanya kazi ya kuwasikiliza na kuwasaidia wananchi hasa wanyonge katika kupata haki zao juu ya madai yao mbalimbali yahusuyo ardhi. Kwani kupitia kusikiliza malalamiko ya wananchi kila ijumaa nimegundua kuwa, zaidi ya asilimia sabini ya walalamikaji hupoteza haki zao kutokana na ufahamu mdogo wa kisheria. Kwasababu hiyo nitumie fursa hii kuwatangazia wanakinondoni kuwa, kuanzia jumatatu hii ya tarehe 15 watakuwepo wanasheria watakaofanya kazi saa zote kwa lengo la kukusaidia wewe mwenanchi ili upate uelewa wa kisheria juu ya haki yako yoyote juu ya umiliki wa ardhi, wanasheria hawa watalipwa kutoka kwenye mshahara wa Mkuu wa Wilaya ambao wamechukua asilimia 75 ya mshahara wangu jambo linalopelekea mwananchi wa Kinondoni kutokulipa hata senti tano anapokuja kupata huduma hii.

3.6  Ili kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza ni vyema pia tukaelewa hatua ambazo ofisi yangu imeamua kuzichukua ili kuhakikisha tunamaliza kabisa migogoro ya ardhi katika wilaya ya kinondoni au kuipunguza kwa kiwango cha hali ya juu sana. Kila mkazi wa wilaya yangu anatakiwa sasa kuchukua copy ya hati au nyaraka yoyote ile inayompa uhalali ya kumiliki ardhi, shamba au kiwanja, copy hizo ninaomba zipelekwe kwa mtendaji wa kata kwani kuanzia tarehe 2 mwezi wa saba, mimi na timu yangu ya watu wa ardhi nitahamishia ofisi zangu kwenye ofisi za kata ili kuhakiki nyaraka hizo na pale itakapobainika kiwanja kimoja kina zaidi ya mmiliki mmoja, tutatafuta mmiliki halali kupitia vyombo tulivyonavyo, na atakayebainika ameghushi nyaraka hatua stahiki zitachukuliwa. Lengo langu ya kuhamishia ofisi kwenye kata, ni kufuta kabisa uzoefu wa kusikitisha wa mwananchi mmoja kugundua kwamba kiwanja chake kinamilikiwa na mtu mwingine baada ya kumwaga roli zake za mchanga ama tofali.


Paul C. Makonda
Mkuu wa Wilaya
KINONDONI



Hakuna maoni