UKAWA WALILIA MAMBO HAYA MANNE,SOMA HAPA KUJUA
Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa umewafungulia viongozi
wa Ukawa kuishinikiza Serikali kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo manne
ili kuondoa mvutano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mambo manne
yanayodaiwa na Ukawa ambayo ni ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya
50, mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya
uchaguzi na urais kupingwa mahakamani ni yale yaliyoafikiwa baina ya Rais
Jakaya Kikwete na vyama vya siasa Septemba 8, mwaka jana.
Mwenyekiti mwenza wa
umoja huo, James Mbatia amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya
kupitishwa kwa Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.
Katika kikao
hicho, Mbatia alisema walitiliana saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu
utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana
kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi
lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika.
Utekelezaji wa
masuala hayo utawezekana iwapo Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni
ili yajadiliwe kwa dharura katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la
Kumi, kwa kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Alipoulizwa
iwapo jambo hilo linawezekana katika Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli
za Bunge, John Joel alisema: “Ndiyo inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha
jambo hili kwa dharura na litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona
linafaa litapelekwa bungeni kujadiliwa.”
Katika hilo
Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa
kufanyika kama ambavyo tulikubaliana na Rais kupitia TCD.”
Alisema ushauri
wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na
matokeo yake yameonekana wazi na kwa msingi huo, suala la kurekebisha maeneo
hayo manne, si la kupuuza hata kidogo.
“Hili lisipofanyika
utaibuka mgogoro mkubwa. Tatizo la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo
yanayoonekana wazi kuwa na mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro
ya wakulima, wafugaji, wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.
Dk Slaa
akata tamaa
Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema endapo Serikali itashindwa kutekeleza
makubaliano hayo, vyama vya upinzani havina budi kuingia katika mapambano kwa
katiba hiyohiyo.
“Kama hatumwelewi
Rais Kikwete katika suala hili, basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi
zozote za Serikali kubadili maeneo haya. Tulikubaliana naye mambo mengi lakini
yote ameshindwa kuyatekeleza, hata hili pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk
Slaa.
Katibu
mkuu huyo wa Chadema alisema umefika wakati wa vyama vya upinzani kupambana
hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya uchaguzi isiyo huru.
“Nimeshinda ubunge
Karatu vipindi vitatu na tume ikiwa ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya
100, nadhani tupambane tu,” alisema.
Alisema umefikia
wakati wa kuing’oa CCM kwa kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa
kufanywa na vyama vya upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili
kuzoa kura zote.
“Tumeshinda Kawe,
Ubungo, Mbeya Mjini na hata Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika
mapambano. Kwanza Bunge lijalo ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko
tunayoyataka hayawezi kufanyika,” alisema.
Kiongozi Mkuu wa
chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe alisema kinachotakiwa kufanywa sasa ni
Baraza la Vyama vya Siasa kuitisha mkutano wa vyama vyote ili kukubaliana mambo
ya kuboresha katika Katiba ya sasa.
“Jambo la pili ni
Rais kuitisha Bunge kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti kujadili mabadiliko
hayo na kuyapitisha ili kuufanya uchaguzi mkuu uwe wa haki na huru,” alisema
Zitto.
Juhudi za kumpata
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk
Asha-Rose Migiro kuzungumzia hatua ambazo Serikali inachukua hazikuzaa matunda
baada ya simu zao kuita mara kadhaa bila kupokewa.
Chanzo ni mwananchi
No comments
Post a Comment