ASKOFU GWAJIMA AMPA ZA USO KIKWETE,AMBEBA LOWASSA,DK SLAA,SOMA HAPA KUJUA
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana
alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa Mbunge wa
Monduli (CCM), Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa
kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Pia askofu huyo,
amewataka waumini wote wa kanisa hilo kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi,
Alhamisi ijayo siku ambayo atakwenda kukamilisha mahojiano dhidi ya tuhuma za
kumtukana Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Akihubiri mamia ya
waumini waliofika kanisani hapo kwa ajili ya ibada ya Pasaka jana, Gwajima
alisema kumekuwa uvumi kwamba kuhojiwa kwake na polisi kulitokana na
kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na kuzungumza na
waumini wake.
Alisema
alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996 wakati huo mbunge huyo akiwa Waziri wa Ardhi na tangu
kipindi hicho amekuwa mtu wake wa karibu.
Alisema
alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994 kabla hajagombea nafasi ya urais
kupitia Chadema na kwamba tangu wakati huo amekuwa rafiki wa familia.
“Hawawezi
kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa karibu hata kabla hawajawa na
ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao karibu,” alisema.
Asimulia
mahojiano
Akizungumzia
mahojiano yake na polisi, Gwajima aliwaeleza waumini wake kwamba mambo mengi
aliyohojiwa hayakuhusiana na suala la kumkashifu Kardinali Pengo.
“Polisi walinihoji
mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali
ya Pengo yalikuwa machache sana,” alisema.
Hata hivyo,
Gwajima alisema hana ugomvi na polisi wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa
ushirikiano kwa vyombo hivyo. Akitoa mfano, alisema Februari mwaka huu
alipeleka barua polisi kueleza anataka kudhamini kampeni kwa ajili ya kupinga
mauaji ya albino kwa kushirikiana na jeshi hilo.
“Niliwaeleza
kwamba tungezunguka na polisi mikoa yote Tanzania na wamenijibu kwamba nipeleke
ratiba ya shughuli hiyo ili tuanze,” alisema.
Alisema pia
alidhamini mafunzo ya ulinzi shirikishi kwa vijana 400 kwa kushirikiana na
polisi... “Shughuli hizi zinaonyesha kwamba sina ugomvi na polisi, bali
nimekuwa rafiki kwa kushiriki katika shughuli zenye masilahi kwa Taifa.”
Viongozi
wamiminika
Alisema pia hana
ugomvi na Serikali na kwamba viongozi wake wamekuwa wakimiminika katika kanisa
lake.
Aliwataja viongozi
hao kuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Uchukuzi, Samuel
Sitta, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe.
Viongozi wengine,
alisema ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye, Mbunge wa Kawe
(Chadema), Halima Mdee na wabunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Vicky
Kamata wote wa CCM “Kama ningekuwa na ugomvi na Serikali viongozi hawa
wasingekuja katika kanisa langu kwa nyakati tofauti. Hii inaonyesha nilivyo na
uhusiano mzuri na Serikali,” alisema.
Alhamisi ijayo
Askofu Gwajima
amewataka waumini wake kumsindikiza katika Kituo cha Polisi siku ambayo
atahojiwa kwa mara nyingine. “Nitakwenda Central Police Alhamisi saa moja
asubuhi, nawaomba waumini wote mfike katika eneo hilo lakini msilete fujo wala
kumtukana mtu, kuweni watulivu wakati wote nitakapokuwa nahojiwa,” alisema.
Askofu huyo
alitakiwa kuhojiwa Alhamisi iliyopita lakini polisi waliahirisha kutokana na
hali yake kutokuwa ya kuridhisha.
Hata hivyo,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Jeshi
la Polisi halitaruhusu mkusanyiko wa watu katika eneo hilo wakati Askofu
Gwajima atakapohojiwa.
“Atatakiwa
kufika na wakili wake na mtu mmoja ambaye ataona anafaa kuingia naye kwenye
mahojiano. Kama kuna waumini wanajiandaa kukusanyika katika ofisi zetu hapa
Central Polisi, wafahamu kwamba haturuhusu na wakikaidi tutachukua hatua.”
Ilivyokuwa
kanisani
Gwajima alifika
katika kanisa hilo lililopo kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe saa 5.00
asubuhi na kupokewa kwa shangwe na waumini walioanza kufika tangu saa 2.00
asubuhi.
Msafara wa magari
matatu; Toyota Land Cruiser mbili na Hammer, yaliwasili kwenye viwanja vya
kanisa hilo na kulakiwa na waumini walioyazingira kwa shangwe na vigelegele
wakitaka kumwona Askofu Gwajima.
Chanzo Gazeti
la Mwananchi
No comments
Post a Comment