TUNDU LISSU AMUENYESHA AG,MHAGAMA,NI KUTOKANA NA UGWIJI WAKE WA SHERIA SOMA HAPA KUJUA
Dodoma. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu jana aliwatoa jasho Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge),
Jenister Mhagama kuhusu kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa
akidai kuwa unagusa mambo ya Muungano na kuvunja Katiba ya Nchi.
Mvutano huo ulisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan
Zungu kutamka kuwa Lissu ni mwanasheria mzuri lakini kwa hoja hiyo aiache
Serikali ishinde, akimaanisha kuwa akubali muswada huo upitishwe.
Katika hoja yake, Lissu alisema muswada huo una mgongano
wa kisheria kuhusu mamlaka ya kuweka utaratibu wa kutangaza maafa na kutangaza
hali ya hatari, akisema kuwa sheria hiyo imempora Rais madaraka ya kutangaza
maafa na kuyapeleka kwa waziri.
Masaju na Mhagama walijichanganya na kusababisha wabunge
kuangua kicheko huku Lissu kila alipopewa nafasi akisisitiza kuwa haiwezekani
waziri amshauri Rais kutangaza maafa.
Masaju alilazimika kusoma vifungu mbalimbali vya sheria
huku akisisitiza kuwa kabla ya kuletwa kwa muswada huo, Serikali ilishauriana
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) huku akisoma Ibara ya 32 ya Katiba
inayozungumzia Rais kutangaza hali ya hatari.
Katika hoja yake ya msingi, Lissu alisema, kutokana na
muswada huo kugusa mambo ya Muungano ili upitishwe, inatakiwa upigiwe kura na
theluthi mbili ya wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge
kutoka Zanzibar.
Wakichangia hoja ya Lissu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali waliungana na Lissu kupinga
vifungu vya muswada huo. Hata hivyo, muswada huo haukupitishwa kutokana na
akidi.
No comments
Post a Comment