MUSWAADA WAKUNYONGA WANAHABARI,WAPINGWA KILA KONA,MCT YAAPA KUFA NA WABUNGE SOMA KUJUA
Jopo la wadau wa habari kutoka asasi, taasisi na vyombo vya
habari nchini, limepanga kuwatumia wabunge kuwashawishi wakatae kupitisha
muswada wa sheria ya habari uliopangwa kuwasilishwa bungeni kwa hati ya
dharura.
Hatua hiyo inatokana na mipango ya Bunge hilo kuweka ratiba ya
uwasilishaji wa miswada miwili ya habari kwa njia ya hati ya dharura, huku
utata ukiibuka kutokana na usiri uliopo ndani ya miswada hiyo.
Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015
na Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015. Jopo hilo chini ya
Baraza la Habari Tanzania (MCT), limekubaliana kutua Dodoma kuanzia kesho ili
kuendesha vikao vya ushawishi ndani na Kamati za Bunge, wabunge na uongozi wa
Bunge ili kuhakikisha miswada hiyo haipitishwi kwa dharura.
Mbali na hatua hiyo, wadau hao wamekubaliana kusambaza nakala
nne za tamko hilo katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Ofisi ya Mpango wa Ubia wa
Uwazi Serikalini (OGP).
Jana, katika mkutano kati ya wadau hao na waandishi wa habari,
walisema lengo la kutoa tamko hilo ni kulitaka Bunge kusitisha uwasilishaji wa
miswada hiyo kwa utaratibu wa hati ya dharura ili kutoa fursa kwa wadau na
wananchi kuiona miswada, kuisoma, kuichambua na kutoa maoni yao.
Walioshiriki kuandaa tamko hilo ni wadau kutoka Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Sahara Media Group, Policy Forum, Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Kampuni ya The Guardian, Mwananchi Communications Ltd, Free
Media Ltd, Hali Halisi Publishers, Taasisi ya Twaweza, Mfuko wa Vyombo vya
Habari (TMF), Tanzania Citizens’ Information Bureau na Shirika la Sikika.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Bara
(Jukata), Deus Kibamba alisema wadau wa habari wanaamini kuwa Serikali na Bunge
hawatakuwa tayari kupokea lawama za wananchi kwa upitishaji wa miswada hiyo
bila kufuata utaratibu wa kawaida.
“Hatutegemei kuona Serikali ikipuuza tamko hili ila inawezekana
tukachukua hatua nyingine, endapo itashindika kwa njia hii ya tamko,” alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Sikika, Irinei Kiria alisema:
“Hatuamini kama Serikali iko tayari kuona ikichonganishwa na wananchi kwa
sababu ya miswada hiyo, wabunge wetu pia hatuamini kama watakubali kuona miswada
hiyo ikipitishwa kwa hati ya dharura bila kushirikisha wadau.
“Miswada hiyo haiwahusu wanahabari pekee, bali hata wadau
wengine, hata CCM hatuamini kama inaweza kukubaliana na upitishwaji wa miswada
hiyo kwa usiri usiojulikana kwa wahusika.”
Akijibu swali kuhusu athari za kutaka kukwamisha miswada hiyo,
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema ni heri
kuzuia kuliko kuruhusu miswada iliyojaa usiri.
Alisema uvumilivu wa harakati za kuhitaji mabadiliko hayo
zimeanza miaka minane iliyopita, hivyo ni vyema kuvumilia ili kuhakikisha
miswada hiyo inazingatia masilahi kwa Watanzania na vyombo vya habari.
“Miswada hii ni mfano wa mtu aliyekuwa na njaa ya miaka mingi,
halafu leo hii unamletea chakula kikiwa kimefichwa bila kujua unamwandalia
chakula gani,” alisema Meena.
Tamko la wadau hao linaelekeza Serikali kupitia mkutano wa 19 wa
Bunge kusoma miswada hii kwa mara ya kwanza kama hatua ya kuifanya iwe tayari
kwa maoni ya wadau kwa miezi inayokuja.
Vyanzo vya ndani ya Bunge hilo vinaeleza miswada hiyo
inatarajiwa kuwasilishwa, kusomwa, kujadiliwa kabla ya kupitishwa Machi 27
mwaka huu katika vikao hivyo vya Bunge.
Hofu ya wadau ilichagizwa zaidi na kauli ya Spika wa Bunge hilo,
Anne Makinda ambayo alilinukuliwa akisema miswada hiyo haijamfikia mezani
kwake.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ambaye alikuwa
mwenyekiti wa tamko hilo, alisema wadau wanatamani kuona miswada hiyo
ikipelekwa bungeni kwa utaratibu wa kawaida.
Chanzo ni Gazeti la mwananchi
No comments
Post a Comment