LOWASSA AMPUUZA MAKAMBA,NI KWENYE URAIS WAKE SOMA HAPA KUJUA
Mbunge wa Monduli (CCM),
Edward Lowassa, amesema watu wanaosema anawalipa watu wanaomshawishi awanie
nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, ni upuuzi na uongo na kwamba hawezi
kuwajibu kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili.
Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana mjini hapa, kufuatia
baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, akisema
baadhi ya watu wanatumia vibaya umaskini wa Watanzania kwa kuwakusanya na
kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza mbele ya wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste
kutoka sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya
kuwagharimia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi na kwamba wengi
wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.
“Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis
Mgeja) kusema leo (jana) kuna mtu kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo
kidogo, ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo
wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu,”
alisema.
Alisema makundi yanayomshawishi awanie nafasi hiyo wanafanya
hivyo kwa utashi wao, mapenzi yao kwa taifa na Mungu wao na kwamba ‘lugha
nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo.’
Awali, Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa
Lowassa wanalipwa, ni walioishiwa hoja, wamefilisika na sasa wanatapatapa na
kwamba kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao
wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.
“Nimekaa muda mrefu kwenye siasa, wengine bado wanahitaji wapate
muda wa kujifunza na katika siasa hatuwajui ni wapi walipotokea, wakipata muda
mzuri wajifunze, wawe na adabu, watulie kuliko kuzusha maneno ambayo huna
uhakika nayo, ambayo ni dhambi kubwa sana,” alisema Mgeja. Alisema wakati wa
sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais
Jakaya Kikwete alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa
kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya siyo makosa.
“Tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani
kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni
nguvu, mjengeni suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi. Kama viongozi
tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka
mbele, niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna
mwingine zaidi ila Mheshimiwa Lowasa,” alisema Mgeja.
Aidha, Lowassa alizungumzia ujio wa wachungaji hao nyumbani
kwake jana, akieleza kuwa umeandika historia katika maisha yake kwani
hakutegemea kupokea kundi kubwa kama hilo la watumishi wa Mungu.
Alisema watu ambao wamemfuata kumshawishi amewaambia kuwa nafasi
ya urais ni kubwa na inahitaji maombi.
“Ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige
magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye
anitiaye nguvu,” alisema.
Mapema, Mratibu wa ujio wa Wachungaji hao, Mchungaji Benedickto
Kamzee, kutoka Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi
huo bila kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.
“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala
halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.
Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT,
TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango
yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.
Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi,
Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni,
Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.
Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same,
Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe, Mwibara, Kisarawe, Nachingwea na Kilolo.
WANAFUNZI, WAFANYABIASHARA WANENA
Wakati huo huo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara mjini
hapa waliokwenda kwa Lowassa juzi kumshawishi agombee, wamesema kwa Lowassa hakukuwa
na ubwabwa wala soda na kwamba kauli ya Makamba inaonyesha kuwa Lowassa ni
kiongozi anayefaa ndio maana watu wanampinga.
Rais wa Kitivo cha Imformative katika Chuo Kikuu cha Dodoma,
Goodluck Philip, alisema wanafunzi walikwenda kwa Lowassa kwa utashi binafsi na
bila shinikizo na kwamba kauli ya kuhongwa imewadhalilisha.
Alisema kauli hizo zinalenga kuwatisha watu wakati msingi wa
kufanya hivyo ni wa kidemokrasia.
Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Dodoma, Norbati
Pangaselo, alisema wapinzani wa Lowassa wanatakiwa kujenga hoja badala ya
kuzusha uongo kwa nia ya kumchafua.
WAZAZI WAJA JUU
Mbio za uchaguzi wa urais zimeanza kukichanganya CCM, kufuatia
Jumuiya ya Wazazi kutoa tamko kali la kutaka kuwachukulia hatua wenyeviti
na makatibu wa mikoa wa jumuiya hiyo na wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya
waliokwenda nyumbani kwa Lowassa kumshawishi agombee urais mwaka huu na
kumpatia Sh. 600,000 wakidai ni kwa niaba ya baraza hilo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, alisema CCM ina maadili na taratibu
zake kwa wanachama wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
"Viongozi 20 wa jumuiya waliokwenda kwa mgombea mmoja
(Lowassa), wakae kwenye vyombo vya habari wakanushe hawakwenda kwa niaba ya
Jumuiya ya Wazazi ndani ya mwezi huu na kwamba kukanusha huko hakuzii kuwahoji
kwenye kikao cha maadili” alisema Bulembo.
Alisema vikao vya maadili vya jumuiya hiyo vitakaa kuwajadili na
wakibainika kufanya makosa wanaweza kuchukuliwa hatua ambao ni pamoja na
kufungiwa uanachama miezi sita, 12 na 18 au kufukuzwa kabisa uanachama.
Kwa mujibu wa kanuni ya Jumuiya ya Wazazi toleo la Mwaka 2008
kifungu cha 83 Ibara ndogo ya 11, Baraza la Wazazi Taifa litakuwa na uwezo wa
kumfukuza au kumsimamisha uongozi kiongozi yeyote ambaye uongozi wake huteuliwa
na Umoja wa Wazazi.
Bulembo alisema viongozi watakaojadiliwa na ikibainika wamekiuka
kanuni watakumbwa na adhabu hiyo ni wenyeviti wa wazazi mkoa wa Kilimanjaro,
Simiyu, Mwanza, Mbeya , Morogoro, Shinyanga, Kusini Unguja na Mkoa wa Mara.
Wajumbe wa Baraza Kuu watakaojadiliwa ni kutoka mkoa wa Tanga, Mbeya, Dodoma,
Ruvuma na mkoa wa Njombe wakati Makatibu wa Jumuiya wanatoka mikoa ya Kusini
Unguja, Morogoro na Shinyanga.
Alisema siyo kosa kwa kiongozi au mwanachama yeyote kuonyesha
mapenzi kwa mtu yeyote anayetaka kugombea urais, lakini taasisi ya chama
haiwezi kuwa na mgombea wake itakuwa imekosa sifa.
"CCM ina jumuiya tatu, Jumuiya ya Vijana, Wazazi na
Wanawake, jumuiya mojawapo inaposema ina muunga mkono mgombea fulani haifai
kubaki tena katika CCM kwa sababu kazi ya jumuiya hizi ni kufanya kazi za chama
kutegemeana na maelekezo," alisema.
Alisema unapozungumzia taasisi ambayo ni Jumuiya ya Wazazi yenye
wanachama zaidi ya 2,300,000 Tanzania nzima, hivyo anapotokea kiongozi mmoja
anasema anazungumza kwa niaba ya wanachama hao ni hatari na anavunja maadili ya
chama ambacho hakiruhusu taasisi kujihusisha na mgombea yeyote.
Bulembo alisema CCM itatoa mgombea wake baada ya mkutano
mkuu kwa kazingatia vikao vya chama, hivyo wale wote waliokwenda kwa Lowassa
watachukuliwa hatua kwa kuitumia jumuiya kwa matakwa yao .
"Lakini hawa wagombea urais napenda niwaase, kama wanataka
kugombea ndani ya CCM wafuate taratibu za chama na kusoma vitabu vinavyoelezea
miiko ya chama, lakini unakuta mgombea anakusanya watu Mbeya na maeneo
mbalimbali jamani anataka nini?” alihoji.
CHANZO: NIPASHE
No comments
Post a Comment