SAKATA LA MAHAKAMA YA KADHI,MAASKOFU WAUMBULIWA NA SERIKALI,AG ASEMA MAHAMA YA KADHI NI SAFI SOMA HAPA KUJUA
pichani ni Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba picha na makta |
Wakati muswada wa
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ukitarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa Bunge
unaoendelea mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amesema
haitakuwa na athari yoyote hasi nchini.
Masaju alitoa
kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Chanzo changu
jijini Dar es Salaam akifafanua juu ya muswaa huo hasa baada ya kuwapo kwa
dalili za mvutano kuhusu uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Alisema tatizo
lililopo ni kwamba serikali haijachukua hatua madhubuti kuwaelimisha wananchi
namna ambavyo mahakama hiyo itakuwa inaendesha kazi zake.
“Suala la
Mahakama ya Kadhi limekuwapo tangu zamani na ilikuwa ahadi za Chama Cha
Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Serikali hatuoni kwa nini
suala hili lisifanikiwe,” alisema.
Masaju alisema Watanzania lazima watambue kuwa Mahakama ya Kadhi
itahusu mambo ya Waislamu wenyewe ambayo ni mirathi, ndoa na talaka.
“Sioni kwa nini
isifanikiwe kwa sababu mahakama hii haiwahusu watu ambao siyo Waislamu na pia
haitakuwa ya kulazimisha,” alisema.
Alisema Mahakama hiyo kwa sababu
itakuwa inashughulikia masuala binafsi kama ndoa na talaka ambayo serikali
haishughuliki nayo.
Alisema
serikali imekuwa ikishughulika na masuala ya jinai kama vile wizi, watu
wanaokula rushwa hivyo mambo binafsi kama ya talaka haishughuliki nayo.
Aliongeza kuwa
kujiunga katika Mahakama ya Kadhi itakuwa ni hiari hata miongoni mwa Waislamu
na gharama za uendeshaji wake serikali haitahusika.
Masaju alisema
suala hilo kama wananchi wakielimishwa haliwezi kuleta mgogoro kwa kuwa ni kitu
cha kawaida na linafanyika katika baadhi ya nchi.
Alisema kimsingi suala hilo linakuzwa na baadhi ya vyombo vya
habari na kusisitiza kuwa Watanzania ni wamoja na watabaki kuwa wamoja.
Aliongeza kuwa
watu ambao hawataki mahakama hiyo wataenda kwenye mahakama nyingine za kawaida.
“Pamoja na
Mahakama ya Kadhi kuamua masuala hayo, mahakama za kawaida zitabaki kuwa na
mamlaka ya kusikiliza masuala ya talaka, mirathi na ndoa,” alisema.
Alisema wakati
wa Bunge Maalum la Katiba Waislamu walitaka suala hili liingizwe katika Katiba
mpya, lakini serikali iliona yasiingizwe kwa sababu ni ya imani za dini na
hivyo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliahidi serikali itapeleka muswada bungeni.
Akijibu swali
la kwamba huenda kuwasilishwa bungeni kwa muswada huo sasa kunalenga kuvuruga
Watanzania kuacha kufikiri masuala muhimu yaliyopo mbele kama uchaguzi mkuu,
Masaju alisema siyo kweli.
Alifafanua kuwa masuala yote kama ya kura ya maoni kuamua Katiba
inayopendekezwa na uchaguzi mkuu yote yana umuhimu na yataenda sambamba.
“Wakristo ni majirani wa Waislamu, Waislamu na Wakristo wanaishi
pamoja, katika baadhi ya familia wengine kuna Waislamu na Wakristo, mwanasheria
mmoja aliniuliza ni amri ipi iliyokuu kuliko yote akasema, mpende Mungu wako
kwa moyo wako wote, mpende jirani yako kama nafsi yako, Waislamu ni jirani
zetu,” alisema.
Masaju alisema kutugwa kwa sheria hii ni kuwezesha Mahakama ya
Kadhi kufanya kazi kwa kufuata utaratibu bila kuingilia mambo mengine ya
serikali.
“Hii siyo mara ya kwanza kutunga sheria. Mtusaidie kama taifa,
sioni sababu Watanzania kupigana na kupinga suala la Mahakama ya Kadhi na
kusababisha kuvunjika kwa amani,” alisema.
Aliongeza kuwa Zanzibar wana Mahakama ya Kadhi, hivyo itakuwa
jambo la kushangaza kwa nini Tanzania Bara kusiwe na mahakama hiyo hali ambayo
italeta manung’uniko kwa Waislamu waliopo bara.
Alisema kwa waliosoma Chuo Kikuu cha Sheria Dar es Salaama suala
la mahakama ya Kadhi hufundishwa kwa mwaka mzima ili kulielewa vizuri.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo
inatumika hata Zanzibar, hivyo siyo jambo zuri bara kusiwe na Mahakama ya Kadhi
kwani itawafanya Waislamu waliopo bara wasononeke.
“Tumeona Waislamu wanaona na Wakristo, hiki ni kitu cha kawaida
kabisa hakuna sababu ya kulipinga, sisi wote tunategemeana, sisi ni ndugu,
binadamu tunaoishi pamoja.
Suala la Mahakama ya Kadhi limekuwa likizungumzwa sana bungeni
tangu Augustino. Mrema alipopeleka hoja binafsi akidai Mahakama hiyo mwaka
1998.
Tangu wakati huo mwaka 1998 - 2000 iliundwa kamati ndogo ya
Bunge kulishughulikia suala hilo chini ya Mwenyekiti wa wakati huo, Arcado
Ntagazwa, aliyekuwa mbunge wa Muhambwe na baadaye liliibuliwa tena mwaka
2002 na Thomas Ngawaiya aliyekuwa mbunge wa Moshi Vijijini na likashughulikiwa
na Kamati ya Katiba, Utawala na sheria chini ya Mwenyekiti wa wakati huo,
Athumani Janguo akiwa mbunge wa Kisarawe.
Baadaye suala hilo lilirudishwa serikalini chini ya Tume ya
Kurekebisha Sheria kati ya 2006 -2008. Tume hiyo ilikuwa chini ya Mwenyekiti
Profesa Ibrahimu Juma.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni