KUPIGWA KWA LIPUMBA KIKWETE AWAPONGEZA POLISI,SOMA HAPA KUJUA
Pichani ni Profesa Ibrahimu lipumba kiwa kwenye ulinzi wa polisi picha na maktaba. |
Rais Jakaya Kikwete
amewakingia kifua polisi waliotembeza kichapo kwa wafuasi wa Chama Cha Wananchi
(Cuf), na kudai kuwa maandamano na mikutano yote ni lazima iwe na kibali cha
polisi.
Rais Kikwete
aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuwaeleza waandishi wa
habari walichozungumza faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck,
na baadaye kuja mbele ya waandishi wa habari na kujibu maswali mbalimbali.
Akijibu swali
la waandishi wa habari wa Ujerumani, aliyetaka kujua hali ya usalama na haki za
binadamu nchini ikoje hasa ikizingatiwa Januari 27, mwaka huu, kulikuwa
purukushani kati ya polisi na wafuasi wa Cuf, na kutumia nguvu kubwa katika
kuwadhibiti.
Akijibu swali
hilo, Rais Kikwete alisema zipo sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza watu
wanapotaka kuandamana au kufanya mikutano ya hadhara na kwamba ni lazima
zifuatwe kwa kupata kibali cha Polisi.
“Huwezi kuamka
asubuhi na kuanza kuandamana au kufanya mkutano wa hadhara ni lazima sheria na
taratibu zilizopo zifuatwe…vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya mikutano na
maandamano bila kubugudhiwa iwapo wamefuata sheria zilizopo,” alisema na
kuongeza:
“Usipokuwa na
kibali Polisi hawawezi kukuruhusu uandamane au ufanye mkutano.”
Kauli ya Kikwete
imekuja siku mbili tangu Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba (pichani),
kuwaeleza waandishi wa habari kuwa ameanza taratibu za kuonana na kiongozi huyo
ili kujadiliana namna ya kuweka utaratibu wa kutenda haki kwa vyama vya siasa
dhidi ya Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba, mwaka huu.
Chanzo change kiliwasiliana na Prof. Lipumba kujua hatua
aliyofikia katika kutafuta nafasi ya kuonana na Rais, ambaye alisema amepeleka
taarifa kwa njia ya mtandao (Info line), na anasubiri jibu na kwamba amehofia
kupeleka taarifa kwa barua kwa kuwa kuna uwezekano wa barua kufunguliwa kabla
ya kumfikia.
Hata hivyo, baada ya msimamo huo wa Rais Kikwete, Prof. Lipumba
alisema watawasilisha kilio cha vitendo vya uonevu vinavyofanywa na Polisi kwa
Rais Gauck.
Aidha, Rais Kikwete alizungumzia pia uhuru wa vyombo vya habari
akieleza kuwa serikali inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari na ni nchi yenye
vyombo vingi ikiwamo magazeti, runinga na radio zinazomilikiwa na watu binafsi na
kukiwa na vichache vinavyomilikiwa na serikali.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni