Zinazobamba

MABILIONI YA USWISI YALIPASUA TAIFA,MAMPYA YAIBUKA,SOMA HAPA KUJUA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akitafakari jambo

Tuhuma za kuwapo kwa vigogo wanaoficha fedha katika benki za Uswisi sasa ni dhahiri baada ya ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ) kufichua kuwa wapo Watanzania 99 wenye akaunti za siri nchini humo zenye mabilioni ya fedha.

           Taarifa ya Swiss Leaks iliyotolewa juzi inaonyesha kuwa Watanzania hao, wakiwamo wanasisa na maofisa wa juu wa serikali, wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.

          Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania iko nafasi ya 100 kati ya nchi zenye kiasi kikubwa cha dola kwenye akaunti za siri nchini Uswisi.

          Msingi wa ripoti hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa wa Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi kuthibitisha.

           HSBC ni benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836. Kwa mujibu wa Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yanatokana na aina tatu za taarifa ndani ya benki kwa vipindi tofauti; Mosi ni taarifa za wateja na uhusiano wao na akaunti za benki nchini Uswisi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007. 

          Pili, ni picha kamili ya kiasi cha juu cha fedha kilichokuwapo kwenye akaunti ya mteja katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007 na tatu, ni mawasiliano kati ya mteja husika na wafanyakazi wa benki katika kipindi cha mwaka 2005. Ripoti hiyo ya Swiss Leaks inaeleza kuwa taarifa za kiuchunguzi kutoka kwenye benki nchini Uswis zinaonyesha kuwa akaunti hizo zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kuanzishwa kwa kampuni hewa. 

         Hata hivyo, ICIJ haijataja majina ya Watanzania wenye akaunti hizo, bali wanaeleza kuwa baadhi ya wateja wanaweza kuwa na akaunti nyingine zaidi nje ya Uswisi au kwenye nchi mbalimbali duniani. 

          Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa ufunguaji wa akaunti za siri kwenye benki unafanyika kwa makusudi, ukiendeshwa na mtandao unaohusisha mamlaka mbalimbali katika serikali. 

         “Ni matumaini yetu kuwa (ripoti) hii itasaidia umma kuelewa machungu ya usiri huu. Tunachofanya ni kuionyesha dunia mambo ambayo kamwe watu wasingeweza kuona,” alisema Gerard Ryle, Mkurugenzi wa ICIJ. 

KENYA KINARA AFRIKA MASHARIKI
         Ripoti hiyo pia imeitaja Kenya kama kinara kwa nchi za Afrika Mashariki yenye watu walioficha fedha nyingi Uswis, ikiwa na wateja 742 wenye akaunti za siri zenye dola za Marekani milioni 559.8 (Sh. bilioni 980.14).

           Tanzania ni ya pili kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha zilizowekwa na raia wake Uswisi, ikifuatiwa na Uganda yenye wateja 57 walio na jumla ya dola za Marekani milioni 89.3 (Sh. bilioni 156.4) huku Burundi ikiwa na wateja 11 wenye dola za Marekani milioni 29.4 (Sh. bilioni 51.5).

           Nchi nyingine za Afrika na kiasi cha fedha kwenye mabano ni Ethiopia (dola milioni 10), Somalia (dola milioni 15.5) na Tunisia (dola milioni 554.2).

           Aidha, Afrika Kusini ni kinara kwa nchi zote barani Afrika, ikiwa na wateja 1,787 wenye dola za Marekani bilioni mbili (Sh. trilioni 3.5) na kwa dunia, nchi zinazoongoza na kiasi chao cha fedha kwenye mabano ni Switzerland (dola bilioni 31.2), Uingereza (dola bilioni 21.7), Venezuela (dola bilioni 14.8), Marekani (dola bilioni 13.4), Ufaransa (dola bilioni 12.5), Israel (dola bilioni 10), Italia (dola bilioni 7.5), Bahamas na Brazil (dola bilioni 7 kila moja) na Ubelgiji (dola bilioni 6.3).

MWANASHERIA MKUU, MKURUGENZI TAKUKURU 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema apewe muda aweze kupitia ripoti hiyo ndipo atakuwa tayari kuzungumza.

“Siwezi kuzungumza suala ambalo silijui kiundani…. kwanza sijaiona ripoti yenyewe, ngoja niitafute na kuipitia ndipo nitakuwa na cha kusema,”alisema.

Masaju alisema anachofahamu kuwa serikali iliunda tume kwa ajili ya uchunguzi wa fedha zinazodaiwa kufichwa Uswis na kwamba tume hiyo bado haijawasilisha ripoti.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, alipotafutwa na Chanzo changu jana alijibu kwa kifupi akisema: “Sina comments (maoni)”. Kisha Hosea akakata simu wakati mwandishi akijaribu kumpa maelezo zaidi na kumhoji juu ya hatua watakazochukua.

ZITTO, MPINA
        Tuhuma za kuwapo kwa vigogo wenye akaunti za siri nchini Uswisi ziliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), bungeni mwishoni mwa mwaka 2012. 

         Aidha, Mbunge wa Jimbo la Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, amekuwa mstari wa mbele pia kufuatilia suala hilo kwa karibu na kutaka serikali ichukue hatua.

“Sisi kwa pamoja tuliridhia kuundwa kwa tume maalum ya kuchunguza, Watanzania wanataka kujua hatma ya fedha zao zilizofichwa nje ya nchi, mbinu zinazotumika kuficha fedha hizi na fedha nyingine zilizofichwa nje ya Uswisi,” Mpina aliwahi kukaririwa wakati akizungumzia suala hilo.

           Agosti 2012, Zitto aliwahi kusema kuwa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswisi na kuchapishwa na magazeti mbalimbali ya hapa nchini mwezi Juni, 2012, ilionyesha kuwa viongozi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara wakubwa ndiyo wametoroshea fedha zao katika benki za Uswis.

            Alisema habari zaidi zinaeleza kwamba mabilioni haya yanatokana na ‘deals’ zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kadhaa kwenye sekta za Nishati na Madini. Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa na Kampuni za utafutaji wa Mafuta na Gesi katika Pwani ya mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.  

           Mwaka jana, Zitto alikaririwa akisema kuwa wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi na kwamba, wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa. 

             Zitto alisema vilevile kuwa Tanzania imepoteza jumla ya dola za Marekani bilioni 1.25 kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hiyo ya kuwapo kwa Watanzania wanaoficha fedha zao Uswis.

            Kufuatia hoja hiyo ya Zitto, Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka juzi ambayo ilikuwa inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

           Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,  Dk. Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.


CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni