AMANI YA NCHI HIKO SHAKANI,MJI WA TANGA WAPOTEZA MVUTO SOMA HAPA KUJUA
.
Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda
miongoni mwa wananchi huku askari wakiendelea kumiminika kwenda katika mapango
ya Amboni yaliyopo nje kidogo na Jiji la Tanga kukabiliana na wahalifu
wanaodaiwa kujificha kwenye mapango hayo.
Taarifa kutoka eneo la tukio
zinaeleza kuwa majira ya saa 5:00 asubuhi magari kadhaa yakiwamo ya kubebea
wagonjwa (ambulance) yalionekana yakielekea kwenye mapango hayo.
Mmoja wa wakazi wa kitongoji cha
Karasha ambaye ni mtumishi mstaafu wa serikali ambaye aliomba jina lake
lisitajwe, alisema kutokana na operesheni inayofanywa na vikosi hivyo tangu
juzi, inadaiwa kuwa wahalifu wamekimbilia katika msitu wa Mbogo ambao upo
kilometa chache kutoka mapango ya Amboni.
Wahalifu hao wamekuwa wakihisiwa na
baadhi ya wananchi kuwa huenda ni magaidi.
Wakati hayo yakiendelea,
wazungumzaji wakuu wa mamlaka za Serikali wamekuwa na usiri mkubwa wa kutoa
maelezo kuhusiana na tukio hilo kama kuna watuhumiwa waliokamatwa.
JWTZ LANENA
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Meja Joseph Masanja, akizungumza na NIPASHE jana, alisema
jeshi hilo halihusiki na kutoa taarifa za tukio hilo kwa kuwa operesheni hiyo
inafanywa na Jeshi la Polisi.
Meja Masanja alisema wanajeshi
wanachokifanya katika operesheni hiyo ni kusaidiana na Jeshi la Polisi
kupambana na wahalifu waliojificha katika mapango hayo.
“Operesheni inayofanywa Tanga ni ya
polisi, siyo operesheni ya kijeshi, hata kama wanajeshi wameenda huko kusaidia,
lakini JWTZ haliwezi kuhusika kutoa taarifa za kinachoendelea katika operesheni
hiyo,” alisema.
RMO TANGA AGOMA
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk.
Asha Mahita, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu hali za askari waliojeruhiwa
katika tukio hilo, alisema hawezi kuzungumza kwa sababu tukio hilo ni tofauti
na matukio mengine.
“Mimi ni mtu ambaye napenda sana
kushirikiana na waandishi wa habari, lakini tukio hili lipo tofauti kidogo na
mengine hasa kutokana na suala la usalama, hivyo siwezi kukueleza hao majeruhi
wanaendeleaje,” alisema.
Juzi askari sita waliokwenda eneo la
tukio walijeruhiwa kwa risasi na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa
Tanga-Bombo.
Tangu askari hao walipolazwa katika
hospitali hiyo, mamlaka kadhaa zimezuia watu kwenda katika wodi ya Galanosi
kuwaona wagonjwa huku maofisa kadhaa wa usalama wakiwa wametanda katika katika
jengo la wodi hiyo kuhakikisha hakuna mtu anayeingia.
RC TANGA KUTOA TAARIFA LEO
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said
Magalula (pichani), akizungumza na NIPASHE alisema leo atatoa taarifa ya
kinachoendelea kuhusiana na tukio hilo.
“Nimepigiwa simu na waandishi wengi
na nimewaeleza kuwa siwezi kuzungumza lolote hadi kesho (leo) nitatoa taarifa
rasmi kwa vyombo vya habari kuhusu kinachoendelea,” alisema.
BULIMBA: BADO HAKUNA JIPYA
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera
Bulimba, alipoulizwa alisema bado hakuna habari mpya kuhusiana na tukio hilo
zaidi ya taarifa zilizotolewa juzi.
“Wasilianeni na RPC Tanga, lakini
kimsingi, bado hakuna jipya, taarifa tuliyoitoa jana (juzi), hakuna
kilichoongezeka,” alisema.
CHAGONJA
Naye Mkurugenzi wa Opereshi na
Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja, ambaye yupo eneo la tukio alipotafutwa simu
yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema bosi wake yupo kwenye kikao.
Kamshina Chagonja alipotafutwa tena
simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na baadaye ikazimwa.
Mapigano ya askari na kikundi cha
uhalifu katika mapango ya Amboni yalianza Ijumaa na kusababisha kifo cha
askari mmoja na wengine sita kujeruhiwa wakati wakirushiana risasi na kikundi
hicho chenye silaha za kivita.
Kufuatia mapigano hayo, wakazi wa
Jiji la Tanga walieleza hofu yao na kupingana vikali na kauli ya Jeshi la
Polisi na kwamba bado hali ya usalama kwao ni tete.
Wananchi hao walieleza kuwa
kinachowapa hofu ni mgongano wa kauli za jeshi hilo katika tukio hilo wakati
Kamishna Chagonja alipokuwa akilizunguzia kwenye vyombo vya habari kwamba
waliarifiwa kwamba silaha za moto zikiwamo walizoporwa askari Januari 26
zimefichwa ndani ya mapango, lakini kilichokutwa ni silaha za jadi yakiwamo
mapanga, pinde na mishale pamoja na vifaa vya kutengeneza milipuko.
Elizabeth Mhagama, mkazi wa
kijiji cha Amboni, alisema licha ya Kamishna Chagonja kuwataka wakazi wa Jiji
la Tanga kutulia kwa kuwa hali ya usalama imeimarishwa, bado wanayo
mashaka na hofu kubwa kuhusu tamko hilo kulingana na mazingira yalivyo.
Mhagama alisema wanashindwa
kuielewa taarifa hiyo kwa sababu bado kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa
kuwa wahalifu hawajakamatwa, hivyo hawajulikani ni kundi gani, limetoka wapi na
lilikuwa na lengo gani.
“Tunaliuliza Jeshi la Polisi kikundi
hicho ni cha watu gani, je kinatokea wapi, kina nguvu kiasi gani hadi
kufanikiwa kujeruhi vibaya askari na kisha kutoroka?” alihoji Mhagama.
Naye Ally Shaban, mkazi wa
Kijiji cha Kongwa jirani na lilipotokea tukio hilo, alilitaka Jeshi la
Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu mwendelezo wa matukio ya uhalifu wa kutumia
silaha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi na kutokamatwa kwa watuhumiwa wa
matukio hayo.
Janathan Joseph, mkazi wa
Majimoto, alisema mbali na tukio la juzi yapo matukio mengine yakiwamo
yaliyosababisha mauaji kwa raia ambao walivamiwa na kuporwa mali na kuwa licha
ya watuhumiwa kushindwa kupatikana, lakini hakuna taarifa za mwendelezo wa
kushughulikiwa kwa matukio hayo.
Joseph alitoa mfano wa tukio la watu
waliyojeruhiwa na bomu la kutupwa kwa mkono kwenye banda la video la kijiji cha
Amboni mwanzoni wa mwaka huu ambako watu kadhaa walijeruhiwa na mmoja kati yao
kupoteza maisha, lakini hakuna aliyekamatwa.
“Yapo matukio mengi kama la
mfanyabishara wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe ambaye alivamiwa na
kuuawa kwa risasi kabla ya kuporwa mali, tukio la utekaji wa gari eneo la
Michungwani wilayani Handeni baada ya kuwekewa magogo barabarani…yote haya
hakuna kitu,” alisema Mariam Mdoe.
Walielezea tukio la uporaji wa
silaha na kusema kitendo cha askari polisi kunyang’anywa SMG mbili
zenye risasi 60 kwenye kibanda cha chips hivi karibuni jijini Tanga wakiwa
doria ni fedheha.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni