Zinazobamba

MBUNGE KAFULILA AMUANDAMA RAIS KIKWETE,AJIPANGA KUIYUMBISHA SERIKALI YAKE SOMA HAPA KUJUA

PICHANI NI Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila Picha na Maktba
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema kwamba analo bomu lingine kuhusu sakata ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Mbunge huyo amesema bomu hilo likilipuka litaitikisa serikali na vigogo waliohusika katika kashfa hiyo, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Kafulila amesema kutokana na hali hiyo, wanaojaribu kumtetea Profesa Muhongo na wengine, ambao Bunge liliazimia wawajibishwe kwa kwa kuhusika na uchotwaji wa fedha hizo, wanajidanganya kwa kuamini kuwa wamenusurika na yaliyozungumzwa bungeni.

Amesema anao ushahidi zaidi ya ule unaothibitisha tuhuma zinazowakabili wahusika hao.

Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika bonde la Uyole na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Jiji la Mbeya juzi jioni.

Kafulila alisema uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliotumiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuandaa ripoti iliyowasilishwa bungeni, pamoja na kugusa maeneo mengi, bado kuna ushahidi wa ziada alionao, ambao akiutoa, unaweza kuwa na athari mbaya zaidi kwa watuhumiwa na serikali pia.

Alisema wanaojaribu kuwatetea watuhumiwa hao, hasa Profesa Muhongo, hawajui wanalolifanya kwa kuwa kutokana na ushahidi uliopo, hata waziri huyo alipopewa nafasi ya kujitetea bungeni, alishindwa.

“Profesa Muhongo alipewa muda wa zaidi ya saa moja bungeni ili ajitetee, alishindwa kuthibitisha kuwa hahusiki na uchotwaji wa fedha za Escrow, muda aliopewa Muhongo hata Waziri Mkuu Lowassa hakupewa. Napenda kuwahakikishieni kuwa ushahidi wa ziada ninao, hivyo hata wakimlinda, haiwasaidii kwa sababu tukifika bungeni tutawabana kwenye kona mpaka wamuondoe hata kama hawapendi,” alisema Kafulila.

Alisema anazo nyaraka zaidi ya 600 zinazoonyesha namna ambavyo fedha za Tegeta Escrow zilivyochotwa, huku baadhi ya nyaraka hizo zikiwa ni muhimu, ambazo CAG wala Takukuru hawakuzipata kwenye uchunguzi wao.

Kafulila alisema suala la kuwawajibisha Profesa Muhongo na watuhumiwa wenzake, ni maridhiano baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na wabunge wa CCM, ambao kimsingi ndiyo wengi ndani ya Bunge kuonekana hawana nia ya dhati ya kuwawajibisha.

Alisema kutokana na ushahidi waliokuwa nao, ilibidi wabunge kuweka pembeni uzito wa hoja na badala yake kwenda kwenye kamati ya maridhiano ili kuona namna ya kumaliza suala hilo.

Kafulila alisema katika maridhiano hayo, wapo baadhi ya watuhumiwa ambao licha ya ushahidi kuonyesha wanahusika na pia kuzidiwa kwa hoja, walipaswa kuwajibishwa.

Lakini akasema walikubaliana kwenye kamati ya maridhiano kutowawajibisha ili kutoiangusha serikali.

Aliwataja waliosamehewa na Bunge kuwa wasiwajibishwe ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wengine, ambao hakutaka kuwataja jukwaani.

Alisema watuhumiwa ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi na Naibu Waziri wa wizara hiyo, ambao ni lazima wawajibishwe kutokana na maridhiano ya Bunge kupitia kwenye Kamati ya Maridhiano.

Alisema endapo kwa namna yoyote watuhumiwa hao hawatawajibishwa, CCM itakuwa imevunja maridhiano na maamuzi ya Bunge na sasa itabidi yawekwe kando ili wabunge waanze kushindana tena kwa hoja kuhusiana na suala hilo.

“Naomba wananchi muelewe kuwa wabunge tulikwenda kwenye maridhiano kwa sababu kubwa mbili; ya kwanza ni kwamba, wabunge wa Ukawa tulikuwa na hoja za msingi, lakini sisi peke yetu hatuwezi kupitisha jambo bungeni kutokana na idadi yetu kuwa ndogo,” alisema Kafulila.

Aliongeza: “Ya pili ilikuwa ni kwamba, wabunge wa CCM hawakuwa na hoja na pia hawakuwa na nia ya kufanya maamuzi ya kuwawajibisha watuhumiwa kwa sababu ni wenzao, lakini wao ndiyo wengi. Kwa kuwa bungeni tunafanya maamuzi kwa kupiga kura, tukaona tutazidiwa  kutokana na idadi yetu kuwa ndogo, hivyo tukakubali tukae mezani kufanya maridhiano na maridhiano yenyewe ndiyo hayo ya kuwafukuza akina Muhongo.”

Alisema ikiwa maazimo ya Bunge hayatatekelezwa, hilo pia litakuwa ni suala lingine ambalo litawafanya wawashe moto upya bungeni punde watakapokutana.

Kafulila alisema suala hilo lilipofikia limesababisha madhara makubwa kwa jamii na haoni sababu ya Rais Jakaya Kikwete, kuendelea kuwakumbatia watuhumiwa wa kashfa hiyo, badala yake anapaswa kuchukua hatua mara moja ili kunusuru taifa.

Alisema hivi sasa nchi wahisani wote wamesitisha misaada waliyokusudia kuipatia Tanzania, jambo ambalo linaliumiza taifa na kuwa wanaoteseka zaidi ni wananchi wanyonge.

Alisema kutokana na kadhia ya sakata la kampuni ya IPTL, hivi sasa hospitalini hakuna dawa, watu wanakufa na hata shughuli nyingine za kijamii hazifanyiki tena.

Kafulila alisema kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakusanya Shilingi bilioni nane kwa mwezi.

Alisema Shilingi bilioni tano zinaishia kuwalipa watumishi mishahara na Shilinghi bilioni tatu zinazobakia ndizo pekee zinazotumika kuendesha nchi.

Kafulila alisema kutokana na hali hiyo, maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kwa sababu huduma nyingi hazitolewi kwa wakati ama hazitolewi kabisa kutokana na ukata.

Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, serikali tayari imewaandikia makandarasi kote nchini kusimamisha miradi yote ya ujenzi wa barabara mahali ilipoishia ili tathmini ifanyike kujua deni ambalo wanaidai serikali.

Pia alisema wakandarasi hao wameagizwa wasiendelee na kazi kwa sababu serikali haina fedha za kuwalipa.

Alisema hali hiyo ni mwendelezo wa madhara yanayotokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kafulila alisema licha ya suala hilo kuleta athari kubwa kwa taifa, bado Rais Kikwete hajachukua uamuzi wa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa kuwafukuza kazi watuhumiwa wa kashfa ya akaunti hiyo.
 

CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni