HIZI NDIZO SABABU ZA SERIKALI YA JK KUTABIRIWA MWISHO VIBAYA
Wakati Serikali ya Awamu ya Nne imebakiza takriban mwaka mmoja kuondoka madarakani, sifa ya Tanzania kwenye jumuiya ya kimataifa imeendelea kutiwa doa kutokana na kuhusishwa na ongezeko la ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma na ujangili.
Kutokana na hali hiyo, huenda uongozi wa awamu hiyo
iliyo chini ya Rais Jakaya Kikwete ikaiacha nchi vibaya na historia ya pekee ya
kuwapo kwa 'mikwaruzano' kati yake na wafadhili mbalimbali wanaoelezwa
kutoridhishwa na namna fedha za umma zinavyochotwa na wajanja wachache wakiwamo
viongozi wa umma.
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo na hatua ya
wafadhili kusitisha misaada yake kwa Serikali inayoisimamia Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: "Kwanza sina taarifa za kutosha
kuhusu msimamo wa Marekani na suala zima la MCC na escrow zaidi ya kuziona
kwenye magazeti yenu."
Aliongeza: "Kwa kuwa sina taarifa rasmi, siwezi
kusema chochote kuhusu hilo."
Juzi, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childressi
alieleza kuwa nchi yake haitatoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Milenia (MMC)
kwa Serikali ya Tanzania, hadi itekeleze maagizo ya Bunge kuhusu uchotwaji wa
fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow. Kauli ya kiongozi huyo imedhihirisha
ukubwa wa tatizo hilo, ingawa Ikulu imeshasema haitekelezi maagizo kwa
shinikizo la misaada.(P.T)
Katika tamko lake kwa umma, balozi Childress
alisema: "Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana
kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya
ufanyaji biashara Tanzania."
Aliongeza: "Tunatoa wito kwa Serikali kuchukua
hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala
muhimu kadhaa ya maendeleo."
Uamuzi huo umekuja wiki kadhaa baada ya wafadhili
katika nchi mbalimbali nao kuzuia kiasi kikubwa cha fedha kutokana na sakata la
uchotaji wa fedha za escrow Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Hata
hivyo, Waziri wa Fedha Saada Mkuya akizungumzia taarifa hizo hivi karibuni,
alisema hakuna mfadhili aliyekataa kutoa fedha, bali mazungumzo yalikuwa
yakiendelea vizuri.
"Nataka kuwahakikishia kwamba washirika wetu wa
maendeleo ambao wanatoa fedha kwa mfumo kusaidia bajeti kuu ya Serikali,
hawajasitisha msaada.
Kulikuwa kuna majadiliano baada ya kuonyesha
wasiwasi...Walikuwa wakisubiri Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ili waweze kutoa. Fedha hizo ni Sh922 bilioni na hapa
tunapozungumza Finland na Idara ya Maendeleo ya Kitaifa (DFID) wameshatoa kiasi
chao," alisisitiza.
Hata hivyo, wakati Serikali ikisema hayo, Wakala wa
Uchunguzi wa Mazingira (EIA) wameitaka MCC kutokubali kuidhinisha mkabata huo
na Tanzania wa Dola 450 milioni za Marekani (Sh700 bilioni), hadi Rais Kikwete
atakapochukua hatua stahiki dhidi ya rushwa iliyotawala na sakata la ujangili
na usafirishwaji wa pembe za ndovu kwenda nje hasa China.
Taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya mazingira,
ilitoa wito huo jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na
Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa MCC, Diana Hyde kwamba wasitishe hatua
hiyo kwa Tanzania.
Novemba mwaka huu, EIA ilitoa ripoti ya utafiti wa
ujangili uliyoanika madudu dhidi ya mauaji ya tembo na namna meno
yanavyotoroshwa nchini.
Hali hiyo inaelezwa huenda ikapunguza nguvu na
jitihada za Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akisisitiza kuwa anakwenda nje
mara kwa mara kwa ajili ya kuonana na wafadhili ili waisaidie nchi kiuchumi.
Jitihada za kumtafuta Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na naibu wake, Mwigulu
Nchemba kwa siku mbili mfululizo hazikufanikiwa kutokana na simu zao
kutopokelewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa.
Hata hivyo, Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi Mduma
alisema kuwa Balozi wa Marekani nchini, Childress alitoa taarifa hiyo kwa
nafasi yake.
"Anaweza akawa amesema yeye kwa nafasi yake na
waziri pia alizungumza kwa nafasi yake. Lakini kama waziri alisema hizo fedha
zitatolewa mwezi Desemba, tusubiri huu mwezi uishe ndipo tujue," alisema
Mduma.
"Kinachohitajika sasa ni kuwa na subira, kama
kutakuwa na mabadiliko yoyote tutawajulisha kwa sababu Desemba haijaisha na
kauli aliyotoa ya waziri ni nzito," alisisitiza Mduma.
Mduma alibainisha kuwa MCC walisema wanatoa fedha
hizo, hivyo lazima kusubiri kwani wanaweza kuamua kutoa sasa au hata mwakani.
Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Tumaini
Dar es Salaam, Deogratius Massawe alisema iwapo MMC itazuia fedha hizo,
Serikali italazimika kukopa fedha kwenye mabenki ya ndani.
Aliongeza kuwa pia baadhi ya miradi iliyokuwa
ikisubiri fedha hizo itakwama kukamilika, huku sekta binafsi nayo ikiathirika.
"Kutokana na kukosekana kwa fedha za kigeni thamani ya fedha itashuka,
sekta binafsi zitaathirika kwa sababu benki zitakimbilia kuikopesha
Serikali," alisema Massawe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za
Mitaa Tanzania (Alat), Dk Didas Massaburi akizungumza jana, alisema kuwa
wafadhili wameamini maneno ya upotoshaji yanayosemwa na baadhi ya wabunge kuwa
fedha za escrow ni za Serikali. Alisema siyo kweli kwamba fedha zilizochotwa ni
za umma badala yake Serikali inadai kodi ambayo haiwezi hata kufika Sh26
bilioni.
Mkazi wa Kijitonyama wilayani Kinondoni, Leonard
Gingo alisema uamuzi wowote utakaochukuliwa na serikali kukabiliana na suala
hilo, utakuwa umechelewa.
"Wananchi tumesubiri nani anawajibishwa kwa
kufukuzwa au kusimamishwa kazi wakati hatua zinachukuliwa, kitu cha ajabu
watuhumiwa bado wapo ofisini, wengine tumewaona wakitia saini mikataba,"
alisema Gingo.
Alisema haki nzuri ni ile inayotolewa kwa wakati na
kwa mtu sahihi na kwamba kuendelea kusita kuchukua hatua ni kuendelea kuwapa
watuhumiwa nafasi ya kuficha
Hakuna maoni
Chapisha Maoni