LOWASSA AIPA USHAURI MWANANA SERIKALI,NA AMWAGIA SIFA RAIS KIKWETE,SOMA HAPA KUJUA
Edward Lowassa |
Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ameiomba serikali kutogandamiza haki za msingi za wananchi kwa sababu ya haki za wanyamapori na kuwataka wananchi hao pia kuheshimu mipaka.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vitongoji huko Bwawani, Mto wa Mbu wilayani Monduli, Lowassa alisema pamoja na matatizo yaliyoko ni muhimu haki za raia zikalindwa.
"Hapa Bwawani najua mna matatizo na National Park...naomba serikali isifanye haki za wanyamapori kwa kugandamiza haki za msingi za raia," alisema Lowassa.
"Tunaheshimu sana utalii kwa sababu unatuingizia fedha, lakini tuheshimu haki za msingi za raia..na nyinyi tuheshimu mipaka iliyowekwa," alisisitiza. Eneo hilo limekuwa na mgogoro na Hifadhi ya Taifa ya Manyara inayopakana nayo, suala ambalo ni moja ya kero kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumzia wana CCM waliyojitoa chama hicho, Lowassa alisema "anayetupinga, atupinge kwa hoja..Kama kero hazijatatuliwa...siyo unaamua kutoka halafu unataka uhongwe ili urudi," alisema.
Alisema ndani ya chama wanagombania utekelezaji wa Ilani na hapo ni haki kwa mwanachama kukasirika iwapo Ilani haitekelezwi lakini si vinginevyo, na kusisitiza kuwa Mto wa Mbu itabaki kuwa ngome ya CCM.
"Mto wa Mbu itabaki kuwa ngome imara ya CCM na majirani zetu Karatu (anakotoka Dk. Wilbroad Slaa) wajue hivyo," alisisitiza. Mapema akizungumza katika mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Migombani kata ya Majengo, Lowassa ambaye anatajwa kutowania tena ubunge na kuelekeza nguvu kwenye urais, alijinasibu kwa mafanikio aliyoyapata katika kipindi chake cha miaka 20 ya ubunge.
"Mwaka 1995 wakati naingia ubunge, mtu ukija hapa Mto wa Mbu lazima ulale huwezi kutoka Monduli kuja hapa na kurudi...barabara ilikuwa mbaya kabisa," alisema na kuongeza anajivuna kuwa wamemaliza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Nne imefanya makubwa ikiwa ni pamoja na usambazaji umeme na maji vijijini.
"Haijawahi kutokea...Serikali hii ya Rais Kikwete imefanya makubwa sana katika umeme, barabara na maji. Mimi najua..nilikuwa waziri wa maji huko nyuma, serikali imejitajidi sana kusambaza umeme na maji vijijini," alisema.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni