HAYA NDIO MAUZAUZA YALIYOFICHUKA KWA LOWASSA,SOMA HAPA
Pichani ni Lowassa |
RIPOTI MAALUM YA HUJUMA ZILIZOFANYWA DHIDI YA CHADEMA KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WILAYANI MONDULI.
UTANGULIZI
CHADEMA wilayani Monduli kilishiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa bila washirika wenzake wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kwani washirika wenzake hawakujitokeza kushiriki katika uchaguzi huu. Kwa kuwa pia hapakuwa na chama kingine chochote cha upinzani kilichoshiriki uchaguzi huu CHADEMA kilikuwa chama pekee cha upinzani kilichoshiriki uchaguzi huu wilayani Monduli.
Katika hatua zote za uendeshaji wa zoezi hili kuanzia hatua za utoaji fomu kwa wagombea mpaka hatua ya upigaji kura na uhesabuji wa kura CHADEMA imefanyiwa hujuma nyingi zinazotufanya tusikubaliane na matokeo batili yaliyotangazwa.
HUJUMA KATIKA HATUA ZA AWALI
Baadhi ya watu waliojitokeza kugombea uongozi kupitia CHADEMA walinyimwa fomu za kugombea kwa makusudi na watendaji wa vijiji/wasimamizi wa zoezi walipoenda kuchukua fomu. Kwa mfano wagombea wetu katika kijiji cha Eluwai kata ya Emairete na kijiji cha mti mmoja kata ya Sepeko walinyimwa kwa makusudi fomu za kugombea uongozi.
Wagombea wengine waliwekewa mapingamizi batili ambayo mpaka sasa wasimamizi wa zoezi wameshindwa kuyatolea maamuzi japo tuliwaandikia barua ya kuhoji uhalali wa mapingamizi hayo.
KUTOKUSHIRIKISHWA KATIKA UANDAAJI WA ZOEZI LA UCHAGUZI
Msimamizi wa uchaguzi kwa makusudi aliinyima CHADEMA karatasi ya mfano wa kura kwa ajili ya kuielewa kabla ya uchaguzi lakini aliwapatia viongozi wa CCM karatasi hiyo. Baadae CHADEMA kilitambua kwamba karatasi ile iliwekewa utata ambao maelekezo yake walipewa wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa CCM yanayoelekeza kwamba anayepigia kura wajumbe wa CHADEMA pia atalazimika kuwapigia wajumbe wa CCM lakini anayepigia kura wajumbe wa CCM hapaswi kuwapigia kura wajumbe wa CHADEMA.
CHADEMA pia kilishuhudia watendaji wa serikali wakitoa semina maalumu kwa CCM lakini hawakufanya hivyo kwa CHADEMA. Viongozi wa CHADEMA Mto wa Mbu walimkuta mtendaji wa kata anayefahamika kwa jina Kuruthum Hassan akitoa semina kwa kamati ya siasa ya CCM ya kata na walipomhoji alidai kama CHADEMA wanataka wamuambie.
NJAMA ZA KUHUJUMU MATOKEO YATAKAYOIPA CHADEMA USHINDI
CHADEMA wilaya ya Monduli kilimuandikia barua Mkuu wa Wilaya na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala (DAS) wilayani Monduli kuhusu njama zilizopangwa za kuhujumu matokeo yoyote yatakayokipa CHADEMA ushindi.
Katika barua na mazungumzo hayo CHADEMA kilimtaja mbunge wa Monduli ndugu Edward N.Lowassa kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji kuhusu namna ya kuvuruga ushindi wowote wa CHADEMA.
Matokeo ya njama hizo tulizoziripoti yamejidhihirisha wazi katika uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Majengo, Mto wa Mbu na Eslalei.
HUJUMA KUBWA ZILIZOFANYIKA SIKU YA UCHAGUZI.
1. Masanduku ya kupigia kura kwa baadhi ya wagombea kutokuwepo katika kituo cha kupigia kura kwa madai kwamba walijitoa.
Katika hali ya isiokuwa ya kawaida, baadhi ya wagombea wa CHADEMA na mawakala wao walipofika kwenye kituo cha kupigia kura hawakukuta masanduku ya kupigia kura kwa madai kwamba wamejitoa na hivyo wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa. Hata hivyo waendeshaji wa zoezi hawakuweza kuionesha CHADEMA barua yoyote inayoonesha kujitoa kwa wagombea hao.
Katika kijiji cha Losirwa kata ya Eslalei mgombea Godwin Ernest Maole aliambiwa amejitoa lakini hakuna barua yoyote iliyooneshwa. Kiongozi wa CHADEMA kata ya Eslalei alipohoji kuhusu barua ya kujitoa kwa mgombea wa chama chake alijibiwa “toa upumbavu wako hapa”.
Katika kata ya Lepurko kijiji cha Nanja wagombea wa nafasi za vitongoji nao hawakukuta masanduku ya kupigia kura zao kwa madai kwamba nao wamejitoa jambo ambalo si la kweli. Hata hivyo mgombea wa uenyekiti wa kijiji hicho ni kweli alijitoa baada ya kupewa fedha na CCM jambo ambalo tulishaliripoti TAKUKURU na wametuhakikishia wamelifanyia kazi na wameridhika kwamba alipewa fedha akajitoa.
2. Mgombea wa CCM kusambaza masanduku ya kura:
Katika tukio jingine lisilo la kawaida, mgombea wa uenyekiti wa kijiji cha Migungani kupitia CCM ndiye aliyeleta masanduku ya kupigia kura pamoja na nyaraka zote za kuendeshea zoezi zikiwemo karatasi za kupigia kura akiwa peke yake bila msimamizi wa uchaguzi.
Baada ya msimamizi wa uchaguzi kufika alikabidhiwa vifaa hivyo na mgombea huyo na kisha mgombea huyo alipotaka kuondoka ndipo mgombea wa CHADEMA alipomuomba lifti kwenye pikipiki yake ambapo alimchukua hadi kituo kingine cha Makao Mapya ambapo alimshusha kisha akaondoka na pikipiki yake akaenda nyumbani ambapo alirudi tena na masanduku mengine ya kura pamoja na vifaa vyote vya kuendeshea zoezi kwa ajili ya kituo hicho cha Makao Mapya.
Katika tukio hilo mgombea wa CHADEMA aliomba karatasi za kura zihesabiwe ili aweze kuzikagua lakini alikataliwa.
Ilipofika saa tano asubuhi karatasi za kupigia kura ziliisha katika kituo hicho na kumfanya msimamizi aagize zingine. Ilipofika saa nane mchana zoezi liliendelea tena baada ya karatasi zingine kuletwa.
Hata hivyo karatasi hizo zilizoletwa nazo ziliisha na katika hali isiyotarajiwa msimamizi wa kituo Theresia Lymo alitoa amri karatasi zilizobakia zikatolewe photocopy na zoezi liendelee. Hivyo zoezi katika kituo hicho liliisha kwa kutumia karatasi zilizotolewa kopi.
3. Katika kituo cha Ziwani kilichopo Jangwani msimamizi alisema kura hazitahesabiwa hapo kituoni na hivyo wahamie shule ya Msingi Magomeni kwa miguu kuhesabu kura. Hivyo walihama japo mgombea wa CHADEMA hakuafiki.
Katika kuhamisha kituo kiongozi wa CCM wa wilaya ndiye aliyebeba sanduku la kura. Wakati kiongozi huyo wa CCM alipokuwa amebeba sanduku hilo aliliangusha chini lakini halikufunguka. Hata hivyo walipofika shuleni aliliangusha tena karibu na mlango na ndipo lilipofunguka na kura kumwagika.
Kura zilipomwagika ghafla katibu mwenezi wa CCM wa kata aliyefahamika kwa jina la Mabia alimwaga kura zingine alizokuwa amezibeba kwenye mtandio zikachanganyika na za kwenye sanduku zilizomwagika. Kura zote zilirudishwa ndani ya sanduku.
Wakati tukio hili linatokea mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja tu la Gideon alikuwa akipiga picha tukio zima kwa simu lakini ghafla afisa mtendaji wa kata, Kuruthum Hassan alimvamia na kutaka kumpiga ndipo mtu anayefahamika kama Humphrey alipoawaamua.
Askari polisi aliyekuwepo katika tukio hilo alipoombwa aingilie alisema yeye anasikiliza amri kutoka kwa Kuruthum.
4. Katika kituo cha Jangwani mgombea wa CCM alileta watu kwa gari lake aina ya pick up na kuwakabidhi kwa wakala wake kituoni na kudai kwamba watu hao wote hawajui kusoma wala kuandika na hawajui kuongea Kiswahili hivyo akamuelekeza wakala wake awapigie wote kura upande wa CCM. Wakala wa CHADEMA aliyekuwepo katika kituo hicho alipinga kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa kanuni lakini msimamizi wa kituo aliruhusu watu wote hao wapigiwe kura na wakala wa CCM.
5. Katika baadhi ya vituo iliposhinda CHADEMA wasimamizi walisema wamechoka na kudai kwamba watatoa matokeo siku inayofuata yaani 15/12/2014. Hata hivyo ilipofika siku hiyo hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kutangaza matokeo hayo na mtendaji wa kata, Kuruthum Hassan pamoja na mtendaji wa kijiji walipotafutwa kuzungumzia suala hilo hawakupatikana ofisini kwao na baadae walionekana makao makuu ya wilaya. Mpaka inafika 16/12/2014 matokeo hayo yalikuwa hayajatangazwa japo yalisikika matokeo mengine tofauti na yale ya mawakala yakitangazwa kwenye vyombo vya habari =kwamba CCM imeshinda kwa asilimia 100.
Katika kitongoji cha Majengo ambapo CHADEMA ilipata kura 209 na CCM kupata kura 91 msimamizi wa uchaguzi alikataa kutoa karatasi ya kusainia matokeo. Wakala wa CHADEMA alipomhoji alimuambia asubiri kidogo kisha akatoka nje na kutoweka.
6. Mpaka inafika 16/12/2014 kura za wajumbe wa viti maalum zilikuwa bado hazijahesabiwa na inadaiwa kwamba masanduku ya kura hizo yapo kituo cha polisi Mto wa Mbu.
7. Idadi ya kura kuzidi idadi ya wapiga kura:
Utata mwingine ulijitokeza ni kwa idadi ya kura zilizohesabiwa kutoka kwenye sanduku kuzidi idadi ya watu waliopiga kura.
Kwa mfano katika kituo cha Migungani kusini jumla ya waliopiga kura ni 66. Katika matokeo CCM walipata kura 57, CHADEMA walipata kura 8 na kura 4 ziliharibika ambapo ukijumlisha kura zilizoharibika na zile za CCM na CHADEMA utapata kura 69.
8. Mawakala wa CCM kusaini Fomu za CHADEMA:
Kila kituo kilicholeta utata mawakala wa CHADEMA hawakusaini lakini katika hali ya kushangaza mawakala wa CCM walisaini sehemu ya mawakala wa CHADEMA. Ofisi inazo Fomu hizo kwa ushahidi.
9. Wagombea wa CHADEMA kufukuzwa wakati wa kuhesabu kura.
Katika kitongoji cha Migombani B mgombea wa CHADEMA alifukuzwa atoke kituoni kwa madai kwamba haruhusiwi kuwepo kituoni. Huu ni uvunjifu wa kanuni ya uhesabuji kura lakini mgombea alilazimika kuondoka kwa nguvu kubwa iliyotumika.
10. Uchaguzi kutawaliwa na vitisho pamoja na mashambulizi vilivyoongozwa na mtendaji wa kata Kuruthum Hassan.
Mawakala wengi walimripoti mtendaji huyo kwamba alikuwa akiwatukana na kuwashambulia kwa kuwasukuma na kuwatishia kuwaweka kituo cha polisi.
Mmoja wa wagombea walioshambuliwa na Kuruthum ni ndugu Allen John Swai aliyekuwa anagombea ujumbe kijiji cha Jangwani ambaye anadai Kuruthum alimfukuza kituoni akisema “toka hapa una kiherehere sana, kwani huko kwenye chama una cheo gani?” katibu wa CCM wilaya naye akadakia akisema “ondoka hapa tutakupoteza” kisha polisi wakamuambia mgombea huyo aondoke asiharibu amani
11. Wasiokuwepo katika orodha ya wapiga kura walioandikishwa kuruhusiwa kupiga kura.
Katika kituo cha Magadini msimamizi aliwaruhusu watu ambao hawajaandikishwa wakachukue vitambulisho vya mpiga kura waje kupiga kura.
Katika tukio hili wakala wa CHADEMA alikiri kwamba hafahamu kama watu ambao hawapo kwenye daftari hawaruhusiwi kupiga kura. Hivyo msimamizi wa kituo alitumia ujinga wa wakala huyo kuvunja kanuni za uchaguzi.
MWISHO
Matukio haya yote yanathibitisha ukweli wa yale tuliyomuandikia mkuu wa wilaya kabla ya uchaguzi kuhusu maelekezo ya kutotangaza ushindi wowote wa CHADEMA aliyopewa Mkurugenzi na Mbunge wa Monduli ndugu Edward N. Lowassa. Hujuma zote hizi ni matokeo ya mkakati maalumu ambayo yalihitimishwa kwa Mbunge wa Monduli kuutangazia ulimwengu kuwa katika jimbo lake, chama chake kimeshinda kwa asilimia 100!
Kufuatia hujuma hizo CHADEMA wilaya ya Monduli inakusudia kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo batili na uvunjwaji wa kanuni uliofanyika katika uchaguzi huu.
HAYA NDIO MAUZAUZA YALIYOFICHUKA KWA LOWASSA,SOMA HAPA
Reviewed by Full habari Digital
on
15:57:00
Rating: 5
Hakuna maoni
Chapisha Maoni