MACHUNGU YA UFISADI WA ESCROW YAANZA KUONEKANA ,SHILINGI YATANZANIA YASHUKA RASMI,SOMA HAPA KUJUA
Dar es Salaam. Hatua ya wahisani kuzuia Sh1 trilioni za
misaada ya kibajeti kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL na wasiwasi wa
Uchaguzi Mkuu mwakani, ni miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa kasi thamani ya
Shilingi nchini, imefahamika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wasomi na wadau
wa biashara nchini walisema sababu nyingine ni uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya
nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Januari 2,
mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1,586 lakini sasa
imepanda hadi Sh1,745. Ikumbukwe kuwa katikati ya mwaka huu, Dola moja ilikuwa
ikinunuliwa kwa hadi Sh1,800 katika baadhi ya benki na maduka ya kubadilishia
fedha, jambo lililoongeza gharama za ufanyaji biashara na kuongeza bei ya
bidhaa.
Escrow
Hivi karibuni, wahisani walitangaza kusimamisha misaada hadi
Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na kuchukua hatua.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi
alisema hatua iliyochukuliwa na nchi wahisani ya kuzuia fedha za misaada hiyo
ambazo zingeingia katika mzunguko wa fedha, imesababisha upungufu wa Dola
katika soko la fedha, hivyo kuongezeka thamani.
Alisema iwapo fedha hizo zingekuwa kwenye mzunguko, zingesaidia
kupunguza uhaba wa Dola uliopo ambao umesababisha kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo
kuchangia kupandisha thamani ya Shilingi.
“Hata kitendo cha Tanzania kuuza bidhaa chache nje ya nchi
kimechangia mahitaji ya Dola kuongezeka kutokana na uhaba wa fedha hizo hapa
nchini,” alisema Dk Ngowi akitaja sababu nyingine ya kuporomoka kwa Shilingi.
Hoja ya Dk Ngowi iliungwa mkono na Meneja wa Fedha wa Soko la
Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshindo Ibrahim akisema kuzuiwa kwa fedha hizo za
hisani, kumechangia kupaisha thamani ya Dola, licha ya kuwapo tatizo la kuuza
bidhaa kidogo nje ya nchi.
“Sisi ni waagizaji wakubwa wa bidhaa kuliko kuuza nje,
tunajikuta tunapata Dola kidogo kuliko mahitaji jambo linaloiongeza thamani
yake, lakini hili la wahisani kushikilia fedha za bajeti kutokana na sakata la
IPTL ni moja ya sababu kubwa kwa sasa,” alisema Ibrahim.
Iwapo wahisani ambao hutoa fedha zao kwa sarafu za kigeni
wataziachia, mtaalamu huyo alisema zitasaidia kupunguza wingi wa Shilingi kwa
kuwa Dola hizo zinatakiwa kubadilishwa kwa sarafu ya ndani ili zianze kutumika.
Alisema kuna wakati hali hiyo ni kawaida kibiashara.
atika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dhamana
na Uwekezaji ya Zan Securities, Raphael Masumbuko alisema safari hii Shilingi
imeshuka thamani kwa kasi isiyo ya kawaida tofauti na miaka ya nyuma, jambo
ambalo linaweza kuchangiwa na homa ya uchaguzi.
“Huenda imetokea kwa sababu tunaelekea katika kipindi cha
uchaguzi. Katika kipindi kama hiki, wawekezaji wengi kutoka nje huwa
wanahifadhi fedha zao katika Dola ili kujiokoa na hasara iwapo utatokea mfumuko
wa bei wakati wa mchakato wa uchaguzi,” alisema Masumbuko.
Alisema Shilingi pia imeshuka thamani kutokana na Dola kutumika
mno katika sekta ya nyumba na msimu huu ni wa kulipa kodi, hivyo Dola
inahitajika zaidi kuliko Shilingi.
“Nyumba nyingi siku hizi zinakodishwa kwa Dola wanaita ‘mita ya
mraba kwa Dola’ hadi majumba yanayomilikiwa na mifuko ya hifadhi za jamii… sasa
kwa hali hii usitegemee Shilingi itapanda thamani,” alisema Masumbuko.
Hata hivyo, alisema hali hii haitakiwi kutia hofu Watanzania kwa
kuwa inaweza kutengamaa baada ya msimu wa baridi kuanza Ulaya ambako watalii
wengi watakuja na kuleta fedha za kigeni, pia juzi, BoT imeuza dhamana
zitakazoipunguza Shilingi sokoni.
Mkuu wa Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es
Salaam, Deogratius Massawe alisema kuongezeka kwa bidhaa mbalimbali nchini
zinazonunuliwa kwa Dola pia kumechangia thamani ya fedha hiyo kuongezeka huku
Shilingi ikishuka.
Massawe alisema mfumo huo unawalazimisha Watanzania kununua
bidhaa hizo kwa bei ya juu zaidi tofauti na ile inayouzwa kwa Shilingi.
“Hata hivyo, ipo sheria inayomzuia mtu kumlazimisha mwingine
kununua kitu chochote kwa Dola, ila mteja anaweza kununua bidhaa kwa Dola iwapo
wamekubaliana na muuzaji.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benjamin Mutagwaba
alisema sera makini ndizo zinazoweza kuinusuru thamani ya Shilingi ya nchi hii.
“Kama kutakuwa na usimamizi mzuri, kilimo pekee kinaweza kuleta
mapinduzi katika biashara na kubadili thamani ya kubadili fedha. Kama mazao
yote yataongezwa thamani kabla hayajauzwa nje, nchi itapata fedha nyingi…
unaweza ukaona hata madini tunayasafirisha yakiwa hayajaongezwa thamani, jambo
ambalo si zuri kwa mustakabali wetu kiuchumi kama nchi,” alisema Profesa
Mutagwaba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya KPMG,
David Gachewa alisema hakuna njia ya mkato wa kuifanya Shilingi iwe na thamani
kama si kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.
“Miaka 10 iliyopita thamani ya Dola moja ya Marekani ilikuwa
Sh800 lakini leo hii ni Sh1,700 na bado tunaagiza bidhaa zilezile kwa sarafu
hiyo. Hii inamaanisha kuwa gharama za bidhaa hizo zimeongezeka na mwananchi
ndiye anayelipia. Hali hii itaendelea kama hakutakuwa na mabadiliko ya kiuchumi
ili kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi,” alisema Gachewa na kuongeza:
“Nadhani mafuta na gesi yatakapoanza kuzalishwa hapa nchini na
kusafirishwa kwenda nje itasaidia kwa kiasi kwa kuwa Serikali itaokoa fedha
zilizokuwa zinatumika kuagiza nishati hizo, pia kuna fedha zitakazoingia
kutokana na mauzo ya bidhaa hizo.”
Kauli ya waziri
Akijibu swali la Cecilia Pareso (Chadema - Viti Maalumu) wiki
iliyopita bungeni, kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya fedha za kigeni nchini,
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema linapunguza ufanisi wa sera za fedha
na uwezo wa BoT kutimiza wajibu wake kuwa mkopeshaji wa mwisho katika uchumi.
Malima aliongeza kuwa endapo wananchi watalazimika kutumia fedha
za kigeni, jambo hilo pia linaweza kuwa kero kwao kwa kuwasababishia usumbufu.
Hata hivyo, Malima alisema kiwango cha matumizi ya Dola nchini
hakijafikia kiasi cha kuwa na madhara hayo.
Alisema uwiano wa amana za fedha za kigeni na ujazo wa fedha,
ambao uliwahi kupanda hadi kufikia asilimia 34 mwaka 2003, kwa sasa umeshuka
mpaka kufikia asilimia 27.2 mwaka 2013.
Alisema mwaka 2007, Serikali ilitoa tamko rasmi kuhusu matumizi
ya fedha za kigeni katika kulipia huduma na bidhaa katika soko la ndani kuwa
Mtanzania yeyote asilazimishwe kulipia huduma au bidhaa yoyote kwa fedha za
kigeni.
Baada ya agizo hilo, Malima alisema fedha za kigeni zinazotunzwa
na BoT ziliongezeka kutoka Dola 228.3 milioni mwaka 1993 sawa na asilimia sita
ya Pato la Taifa hadi Dola 4 bilioni sawa na asilimia 14 ya Pato la Taifa mwaka
2012
Hakuna maoni
Chapisha Maoni