SAMWEL SITTA ATANGAZA VITA NA MAASKOFU NCHINI,WENYEWE WASEMA ATAKUWA ANAMPUUZA MUNGU,SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
Pichani ni Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samwel Sitta picha na Maktbaba |
MWENYEKITI
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amejiweka katika wakati mgumu kwa
kuzua mgogoro mpya dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo, baada ya kuita waraka
wao kuwa ni wa kipuuzi na wa hovyo hovyo.
Huku yeye
akisema kuwa waraka wao una lugha ya UKAWA, wao wamesisitiza kwamba ni waraka
wa kinabii, kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.
Wakati yeye
akikemea waraka wao, maaskofu wamesema ile ilikuwa sauti kutoka mbinguni, na
kwamba anapambana na Mungu.
Wakati yeye
akisema waraka wao haukuwa na utukufu wowote, wao wamemfananisha yeye na
Goliati wa kwenye Biblia aliyeshindwa na Daudi kwa sababu ya jeuri na matusi
kwa Mungu. Wamesisitiza kwamba kwa sababu ya jeuri yake, wataanzia pale
atakapoishia baada ya Bunge Maalumu la Katiba.
Juzi na jana
asubuhi, Sitta alitoa maneno ya kejeli dhidi ya viongozi wa Kikristo, hasa
Jukwaa la Wakristo, ambao walitoa waraka kuonyesha kutoridhishwa kwao na
mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba.
Sitta alitoa kauli
hiyo bungeni alipokuwa akielezea mwenendo wa upigaji kura za kupitisha ibara na
sura za rasimu ya katiba inayopendekezwa, akisema amekuwa akituhumiwa kwenye
mitandao kwamba anadharau maaskofu.
Kauli ya
Sitta
“Nimalizie na viongozi wangu wa kiroho…mababa zangu maaskofu,
natuhumiwa sana kwenye mablog kwamba nadharau maaskofu. Wakiwa na matendo kama
hayo hao baadhi ya maaskofu itabidi tuendelee kuwadharau.
“Ninao waraka huu
ambao umelazimishwa kutumwa katika makanisa. Sioni utukufu wa Ukristo katika
waraka huo. Huu waraka unamwamuru Rais airudishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kuna Ukristo hapa? Waraka huu unamlazimisha Rais asitishe mchakato wa Bunge
Maalum…tangu lini watu wa kiroho wanatoa maagizo ya kisiasa? Hii sio haki hata
kidogo…kuna Ukristo hapa? Waraka una lugha za wale UKAWA tuliowazoea.
“Hivi kweli
maaskofu wa Kikristo wanaweza kusema kwamba Wizara ya Katiba na Sheria irudishe
tovuti ya Tume ya Jaji Warioba na kuirejeshea nyaraka zake zote ili wananchi wasome
na kujifunza?
“Kwamba maoni ya
wananchi hayawezi kufutwa na kudharauriwa na chama tawala, hivyo basi Bunge la
Katiba lijadili na kuboresha tu rasimu ya katiba na si kubadilisha?
“Waraka huu kwa
shinikizo la maaskofu umesambazwa kwenye makanisa na kusomwa. Mimi nasema kama
Mkristo, tukianza kuruhusu nchi yetu kutoa nyaraka hizi za kisiasa zisomwe
makanisani kwa kudai huo ni msimamo wa maaskofu, basi nchi hii tutaipeleka
kubaya.
“Na mini kama mtu mzima lazima nionye
kuhusu tabia hii, ukizingatia nchi hii haina dini, hawa baadhi ya maaskofu
ambao walikusanywa Dar es Salaam na makundi yale yale yanayohusishwa na UKAWA,
kama wao ni wanachama wa siri wa vyama vya siasa vinavyochukia CCM wajitokeze
wazi
wazi,” alisema.
wazi,” alisema.
“Na kuna askofu mmoja ameapa kabisa
kwamba atawaelimisha waumini wake ili siku za usoni wawashughulikie viongozi
kama mimi. Nasema aendelee
lakini Mungu anaona yote yaliyo moyoni mwetu.”
lakini Mungu anaona yote yaliyo moyoni mwetu.”
Maaskofu
nao wanena
Chanzo hicho ilizungumza
na maaskofu kadhaa kutoka CCT, wakasema wamekerwa na kebehi na dharau za Sitta.
Askofu wa Kanisa
la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson
Bagonza, alisema waraka wa maaskofu ni nguvu kutoka mbinguni, si kukurupuka.
“Nimemsikia Sitta
akitushambulia. Sasa natumia hekima kumjibu kwamba maandiko matakatifu katika
Biblia; 1Samweli 17:31-37, hasa mstari wa 36, yanasema Goliati alipogombana na
kijana mdogo Daudi. Ushindi wake ulitokana na Goliata kumtukana Mungu wa Daudi.
“Na ukiona Goliati
anaanza kumtukana Mungu, ujue ushindi wa Daudi umekaribia. Hivyo ndivyo Sitta
sasa anavyokebei na kutukana viongozi wa dini. Hapo tunakumbushwa na maneno ya
Mungu yanayosema, ‘awakatae nyinyi niliowatuma, amenikataa mimi.’ Tazama
Luka 10: 16, ” alisema Askofu Bagonza na kuongeza:
“Na katika
kauli zake hizo amekuwa akisema kuwa waraka wetu unafanana na msimamo wa UKAWA
… sasa kama katupeleka huko nasi tutaeleeke huko huko, tusije kulaumiana tu,
mbele ya safari.
“Nilikuwa mmoja wa
wanakamati walioandika waraka huo. Wakati wenzangu wanautoa mbele ya umma, nilikuwa
kwenye msiba mzito wa Askofu Mkuu Mstaafu Mukuta, lakini nataka nimwambie hivi
mtetezi wetu yu hai, na wala hatuwezi kujitetea mbele yake (Sitta).”
Askofu wa Jimbo la
Katoliki la Bunda, Mhashamu Renatus Nkwande, alisema matamshi ya Sitta
yanaonyesha anavyohangaika kualalisha kilicho haramu.
Alisema
kitendo cha Sitta kuendesha BMK kwa kukejeli wajumbe wenzake walioondoka
bungeni (UKAWA) na wajumbe walioandaa rasimu ya pili kwenye Tume ya Katiba Mpya
chini ya Jaji Joseph Warioba, ni jambo la aibu ambalo halivumiliki, na ndiyo
maana walitoa waraka wa kutokubaliana nacho.
“Kwa kweli Sitta
ametutukana, ametafuta ubaya kwa viongozi wa dini, kwa kuwa tumesema ukweli ?
Sisi tulikuwa tunatimiza wajibu wetu kwa Wakristo …tulizungumza kutokana na
hitaji la wakati, na ulikuwa waraka wa unabii,” alisema.
Askofu wa KKKT
Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Steven Munga, alisema hawatajibizana na Sitta, bali
wataanzia pale alipoishia.
“Ukibishana na
mjinga utakuwa mjinga pia. Tunasubiri wamalizie kazi iliyowapeleka huko kula
fedha ya wananchi. Sisi viongozi wa dini tuna watu wengi zaidi,” alisisitiza.
Baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii waliliambia gazeti hili kuwa jeuri
ya Sitta imemfanya atangaze vita tatu kwa mpigo.
“Kwanza,
ametangaza vita na viongozi wa dini ya Kikristo. Pili ametangaza vita ya CCM na
viongozi hao, iwapo CCM haitamkemea hadharani. Tatu, ametangaza vita na imani
yake mwenyewe,” alisema mchambuzi mmoja.
Mzozo huu mpya
wa Sitta na viongozi wa dini unaweza kumweka njia panda, hasa kwa kuwa amekuwa
anatumia makanisa hayo hayo kujipigia debe na kushambulia wanasiasa wenzaka
anaopambana nao kusaka urais
Chanzo ni Gazeti makini la Tanzania Daima
Hakuna maoni
Chapisha Maoni