Zinazobamba

MAALIM SEIF AMCHANACHANA RAIS KIKWETE NA KATIBA YAKE,APIGILIA MSUMARI WA MWISHO,SOMA HAPA KUJUA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Rais Jakaya Kikwete na Dk. Ali Mohamed Shein wasikubali kudanganywa na vigogo waliosimamia Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Amesema si kweli kwamba Katiba pendekezwa imekidhi matakwa ya Zanzibar kama walivyodai wajumbe wa BMK wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), bali wataendelea kuitambua Rasimu ya aliyekuwa Mwenyekiti wa mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Warioba.
Maalim Seif awavaa JK, Dk. Shein
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya demokrasia Kibanda Maiti Mjini Zanzibar ulihusu yaliyojiri katika BMK na sherehe za kukabidiwa katiba pendekezwa Oktoba 8 mwaka huu.
Akihutubia umati wa wanachama wa chama hicho, Maalim Seif, aliwataka marais hao kulinda heshima zao na kamwe wasikubali kudanganywa na aliyekuwa Mwenyekiti wa BMK Samwel Sitta na Mwenyekiti wa kamati ya uandishi wa Katiba pendekezwa Andrew Chenge.
“Nawataka marais hawa wanaotuongoza Kikwete na mwenzake Dk. Shein kulinda heshima zao… wasikubali kufungiwa ngulai na vigogo hawa wa CCM Sitta na Chenge kwa ajili ya manufaa yao na siyo wananchi” alisema.
Maalim Seif, alisema Katiba pendekezwa waliyoipokea imekosa uhalali wa wananchi hivyo kutokidhi kuwa katiba bora iliyobeba matakwa ya wazanzibari kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya Jaji Joseph Warioba.
“Rasimu tumeitunga sisi, wakaibadilisha wenyewe, wakaijadili wenyewe, wakaipitisha wenyewe na wameichezea ngoma wenyewe,” alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema Katiba inayopendekezwa imenyang’anya mamalaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kwa lengo la kulinda maslahi ya CCM.
Katibu Mkuu huyo naliyaponda mapendekezo ya katiba hiyo kwa madai kwamba imepatikana kwa njia za udanganyifu kwa ajili ya kuangamiza mamlaka ya Zanzibar kwa na kuyahamishia Dodoma.
Alisema katika Katiba inayopendekezwa ya Sitta, imeyaweka mambo ya uvuvi, kilimo na utamaduni na michezo kuwa ya muungano kwa lengo la kupora ardhi ya Zanzibar.
“Masuala ya uvuvi, kilimo na utamaduni na michezo siyo ya muungano…kila nchi inatakiwa isimamie yenyewe,” alisema.
Aidha alisema jambo jingine lililowekwa katika rasimu hiyo na siyo la muungano ni kuhusu suala la Tawala za Mikoa, kupewa mamlaka ya kugawa mikoa ya nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye aliyepewa mamlaka hayo.
Pia, kiongozi huyo aliishangaa kamati ya uandishi ya Chenge kuondoa suala la mahakama ya katiba iliyopendekezwa na Jaji Warioba ambayo alitaka iundwe mahakama ya juu itakayokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri lolote kutoka Zanzibar ama Tanzania bara.
‘Namshangaa Rais Kikwete kusema kwamba Katiba pendekezwa nzuri…Ipi? Katiba nzuri ni ile inayojali na kuthamini matakwa ya wananchi,” alisema Maalim Seif.
Aliwataka marais, kutokubali rasimu hiyo kupigiwa kura ya maoni kabla ya uchaguzi, kwani kwa upande wa Zanzibar haiwezi kupita mpaka ipatikane theluthi mbili na kupigwa kura ya maoni katika baraza la wawakilishi.
“Katiba pendekezwa ya Jamhuri ya Muungano haiwezi kupita Zanzibar, hapo itakapokubaliwa na theluthi mbili za wajumbe wa BMK …lakini pia ikubaliwe na wajumbe wa baraza la wawakilishi hapa Zanzibar, ikifahamu kuwa CCM haina wawakilishi wa kutimiza theluthi mbili,” alisema.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano, Mansour Yussuf Himid, alisema ataendelea kutetea maslahi ya Zanzibar popote na bila ya kuogopa mpaka Zanzibar ipate mamlaka yake kamili.
Himid, alisema ataendelea kupinga mfumo wa muungano wa CCM mpaka siku ya kiama kwa kuwa muungano uliopo, umejaa ukatili dhidi ya Wazanzibar.


“Kwa mujibu wa vitabu vya dini mbalimbali vinaeleza kila nafsi itaonja mauti, je wao wanaogopa nini? … kilichobakia ni kuingia mitaani kuwambia Wazanzibar wasikubali kuipitisha katiba hiyo,” alisema.

Hakuna maoni