JK APIGILIA MSUMARI WA MWISHO MASHINE ZA EFDS
RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza msimamo
wa Serikali, kwamba mashine za elektroniki za ukusanyaji kodi (EFDs), lazima
ziendelee kutumika nchini. Alisema hayo jana wakati alipozungumza kwenye
uzinduzi wa Ofisi za Mamlaka ya Bandari (TRA) mjini Karatu katika Mkoa wa
Arusha, na kuongeza kuwa changamoto za mashine hizo zinajadilika.
“Najua kuna maneno mengi kuhusu suala
hili. Kwa hiyo maelekezo yangu ni kwamba kaeni chini, mjadili matatizo yaliyopo
na kupata ufumbuzi. Kama ni suala la bei pia linazungumzika lakini tunahitaji
mfumo huu wa malipo ya kodi,” alisema.
Aliagiza viongozi wa TRA kukaa chini na
wadau na watumiaji wa mashine hizo kuzungumza na kutafuta majawabu
yanayolalamikiwa na wadau.
Alisema kuacha kutumia mashine hizo ni
kurudi nyuma kwa kuwa zimeshaanza kutumika duniani kote na hata nchi jirani
baadhi zimeshaanza kutumia na nyingine ziko katika maandalizi ya kutumia.
“Kwenye hili tusirudi nyuma kwa sababu
tukifanya hivyo, tutakuwa tunarudi nyuma sana kwa sababu dunia nzima inaelekea
huko na hata majirani zetu wote ama wameanzisha mfumo huo ama wanajiandaa
kuuanzisha.”
“Hatuwezi kurejea kwenye mfumo ule wa
kutumia vijirisiti. Mfumo wa sasa unaifanya kazi ya kukusanya kodi kuwa rahisi
kwa Serikali yenyewe na kwa walipa kodi. Najua watu hawapendi kulipa kodi
lakini hakuna njia ya jinsi ya kuendelea isipokuwa kwa kulipa kodi,”
alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa muda mrefu TRA imekuwa ikisisitiza
kuwa utaratibu wa kutumia mashine za EFDs ulianzishwa kwa lengo la
kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa kumbukumbu za biashara za kila siku
pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa ukadiriaji wa kodi. Mfumo huo wa kutumia
mashine za kodi za kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu.
Awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 kwa
wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Awamu ya pili ilianza 2013 ikiwahusu
wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT ambao mauzo ghafi kwa mwaka ni
Sh milioni 14 na zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa za TRA,
wafanyabiashara zisizo rasmi zikiwemo za mama lishe na wale wanaotembeza bidhaa
barabarani, hawahusiki kwa sababu hawana sehemu maalumu ya kufanyia biashara.
Miongoni mwa wafanyabiashara
wanaotakiwa kutumia mashine hizo ni wenye maduka ya vipuri, mawakili, maduka ya
jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na
vipuri vyake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, biashara za kutoa huduma
za chakula, wauzaji wa pikipiki, maduka makubwa ya nguo na biashara zinginezo
Kwa mujibu wa taarifa za TRA, kwa nchi nzima walengwa ni wafanyabiashara laki
mbili tu kwa awamu ya pili kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na
nusu ambao wamesajiliwa kulipa kodi.
Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya
siku moja kukagua shughuli za maendeleo wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha
na leo atafanya ziara kama hiyo ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa
Kilimanjaro. CHANZO: HABARILEO (FS)
Hakuna maoni
Chapisha Maoni