DK SLAA AMTAKA MKAGUZI NA MDHIBITI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KUMFANYA KUFANYA UKAGUZI OFISI ZA SPIKA WA BUNGE NA WABUNGE SAFARI ZOTE ZA NJE YA NCHI.
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbroad Slaa, ameibukia suala la matumizi mabaya
ya fedha unaofanywa na wabunge na kutaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi safari zote za nje zinazofanywa
na wabunge pamoja na ofisi ya Spika.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kigwa wilaya ya Uyui
jimbo la Igalula mkoani Tabora, alisema Bunge limegeuka kuwa sehemu ya
kuhujumu fedha za Watanzania.
Dk. Slaa alisema kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya
Bunge, Watanzania waunganishe nguvu zao kupiga kelele ili bunge lirudi
katika mstari wake wa kutetea wananchi kupata maendeleo.
Alisema amepata barua kutoka ofisi ya Bunge ambayo inaonyesha kuwa kati ya Julai-Oktoba Bunge limeomba Sh. bilioni 23.
"Shilingi bilioni 23 zilizoombwa na Bunge ambazo wanagawana tu zinaweza
kujenga madarasa 300 ya shule, madarasa 300 yanatumika kwa ajili ya
kupigana majungu,bunge limeacha misingi yake ya kutetea wananchi,"
alisema.
Alisema katika barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Bunge, Dk.
Kashilila, imetoa mchanganuo kuwa Sh. bilioni 2.890 zimetengwa kwa ajili
ya posho za jimbo kwa wabunge.
Sh. bilioni 2.218 zimetengwa kutumika katika vikao vya kamati za bunge
ambavyo hazina manufaa yeyote kwa wananchi na gharama za kamati teule za
uchunguzi zimetengwa milioni 300.
Dk. Slaa alisema barua hiyo inaonyesha kuwa gharama za wabunge kwenda
nje ya nchi zimetengwa Sh.bilioni 1.2, safari za viongozi nje ya nchi,
Spika na Naibu Spika zimetengwa Sh.milioni 300.
"Wabunge wanatengewa fedha kwenda kutalii Ulaya katika nchi maskini kama
Tanzania, ni lini wamerudi na kuleta tija kwa wananchi,mbunge anapata
takribani milioni 9 kwa ajili ya kutembelea wananchi wake lakini bado
wapo ambao hawaendi,"alisema.
Aliongeza kuwa matibabu ya wabunge nje ya nchi zimetengwa Sh.milioni 300
na gharama za uendeshaji wa ofisi ya Bunge ni Sh.bilioni moja.
Dk. Slaa alisema wakati fedha hizo za kuanzia Julai hadi Oktoba
zikiendelea kutafunwa, ofisi ya Bunge kwa mara nyingine imeomba fedha
nyingine Sh. Bilioni 29 kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, Alisema
kutokana na hali hiyo ni takribani Sh. bilioni 52 zimeombwa na ofisi ya
Bunge na kwamba ni wakati sasa kwa CAG kufanya ukaguzi wote wa wabunge
na ofisi ya Bunge.
No comments
Post a Comment