Wito wa Rais Kikwete alipozungumza na Watanzania waishio Poland
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu, Rais Kikwete awaambia Watanzania
Watanzania waishio nje Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema wajibu mkuu wa Watanzania
wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi
badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.
Rais Kikwete akiongea na Watanzania hao
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kuishi kwa Watanzania nje ya nchi
kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa
wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao
waliobakia Tanzania.
Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya wenyewe kwa kuiga tamaduni za
kigeni kupita kiasi.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio nchini Poland
usiku wa jana, Alhamisi, Novemba 21, 2013, kwenye Hoteli ya Bristol
mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne
katika Poland.
Aliwaambia Watanzania hao na familia zao: “Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea
vizuri nchi yetu, mtaitetea nchi yenu, mtaihangaikia nchi na kuleta
faida nyumbani. Ni jambo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza
kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi
yenu wenyewe. Nchi mbaya, viongozi hawafai..mnapata faida gani. Mnazo
nchi ngapi?”
Aliongeza Rais Kikwete: “Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao
hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba mtasukuma mbele maslahi ya
nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko
hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui.
Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”
Alisisitiza Rais Kikwete: “Mbona kazi za ma-Ngo’s mnazifanya vizuri bila
kusukumwa ama kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi?
Kama hata hamwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?”
Rais amesema kuwa kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na
kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa
kuanzishwa kwa uraia pacha (dual citizenship) ambao Watanzania waishio
nje wanaulilia. “Mnaweza kuhalalisha hoja ya uraia pacha kwa kuwa watu
wenye faida kwa nchi.”
Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa
Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala
hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
“Rasimu ya kwanza ya Katiba ililikataa jambo hilo kwa sababu hili ni
jambo lisilokuwa na ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu
kwenu ni jipangeni vizuri kutetea hoja yenu hii. Saidieni mjadala wa
jambo hilo badala ya kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na hivyo
kusahau yenye maslahi kwenu.”
Kuhusu kuiga tamaduni za nchi nyingine na kusahau za nyumbani, Rais
Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea kuwa baadhi wachache wanaoishi nje ya
nchi, wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya
kwao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa
suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni
kuwauza watoto wa kike.
Rais ambaye alionyesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, DAR ES SALAAM.
22 Novemba, 2013
Hakuna maoni
Chapisha Maoni