SERIKALI KUPUNGUZA USHURU WA MAGARI YA UMEME KWA 15%, NA KUSAMEHE KODI VIFAA VYA KUCHAJI MAGARI

Serikali imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme katika hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini.
Hatua hiyo imetangazwa leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Omar amesema pendekezo hilo ni sehemu ya hatua za kodi zinazolenga kuchochea matumizi ya teknolojia za nishati safi katika sekta ya usafiri.
Aidha, Serikali imependekeza kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwenye betri za umeme zinazotumiwa na wazalishaji au waunganishaji wa magari na pikipiki za umeme pamoja na kuendelea kutoa vivutio vya kikodi kwa waunganishaji na wazalishaji wa vyombo vya moto vinavyotumia umeme na gesi.
Katika hatua nyingine, Serikali imependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vinavyotumika katika vituo vya kuchaji magari ya umeme vinavyoingizwa nchini ili kuwezesha maendeleo ya miundombinu ya nishati safi.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ikiwa ni sehemu ya hatua za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala katika vyombo vya moto nchini..
No comments
Post a Comment