Zinazobamba

DIRA YA MAENDELEO 2050 INALENGA KUJENGA TAIFA JUMUISHI LENYE USTAWI,HAKI NA LINALOJITEGEMEA: DKT.GWAJIMA.


Na Moses Mashala.

Imeelezwa kuwa Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi,haki na linalojitegemea kwa kuwekeza zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi zaidi ikiwemo sekta ya Kilimo,Utalii,Viwanda,Ujenzi,Michezo,Sanaa za ubunifu na Madini. 

Hayo yamesemwa leo Desemba 22,2025 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu Dkt.Dorothy Gwajima wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuelezea mafanikio na mipango mikakati ya Wizara hiyo chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Aidha amesema kwa msingi huo mwelekeo wa Serikali katika uwekezaji kwenye sekta hizo unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa makundi maalumu huku akitoa wito kwa jamii kuvitumia vyuo vya maendeleo ya jamii na Maendeleo ya jamii ufundi ili waweze kupata maarifa na ujuzi utakaochangia kuleta maendeleo kwa kujiajiri,kuajiriwa na kuajiri wenzao.

Waziri Gwajima amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Rugemba,Ruaha(Iringa)Mlale(Ruvuma)Mabughai(Tanga)Uyole (Mbeya)Monduli(Arusha)Misungwi (Mwanza)na Buhare(Mara) pamoja na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru(Arusha).

Katika hatua nyingine amesema kuwa ili kuwa na Taifa lenye Wananchi Wazalendo wanaozingatia maadili ya kijamii ni muhimu kuwekeza katika malezi na makuzi bora ya watoto. 

"Katika kufikia lengo hilo Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu ya malezi kupitia mwongozo wa wajibu wa Wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya watoto na familia". amesema 

Nakuongeza kuwa,"Hadi kufikia Desemba 2025 wataalam wa ngazi ya Mikoa na Halmashauri wameshapatiwa mafunzo kuhusu mwongozo huo ili wapeleke ujumbe huo katika Jamii".

Amesisitiza umuhimu wa Wazazi wote wawili yaani baba na mama kushirikiana katika kuwalea watoto ili kufikia ukuaji timilifu kimwili,kiakili na kisaikolojia.

Vilevile amesema kuwa ni muhimu kwa Wazazi au walezi na jamii kuwa karibu na watoto wao kwasababu watakua wanatengeneza muunganiko(Bondi)na hivyo kuwezesha upendo toshelevu wa watoto na Wazazi au walezi wake. 

"Kukosekana kwa hiyo bondi kunapelekea watoto kutokua na upendo kwa Wazazi ama walezi wao hasa wanapokua watu wazima na kuwatelekeza Wazazi wao"amesema Dkt.Gwajima.

No comments