Zinazobamba

DHAMIRA YA SERIKALI NI KUHAKIKISHA VIJANA WANAFIKIWA NA KUSHIRIKISHWA: WAZIRI NANAUKA

Na Moses Mashala.

Imebainishwa kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha  vijana wanafikiwa walipo,wanasikilizwa kwa makini,na wanashirikishwa katika kujenga mustakabali wa Taifa. 

Hayo yamebainishwa leo Desemba 23,2025 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Joeli Nanauka wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuelezea utekelezaji wa mipango ya Wizara yake katika Serikali ya wamu sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, nakusisitiza kuwa Serikali inatambua kuwa vijana ndiyo nguvu kazi kubwa ya Taifa na ni muhimu kwa  maendeleo ya kiuchumi,kijamii na kisiasa. 

Aidha amesema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 ni takriba 20.6.ambapo wanachangia zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya Taifa. 

"Ndiyo maana nimesema wazi kuwa sitosubiri vijana wanifuate ofisini,mimi na timu yangu tutawafuata vijana walipo-iwe ni mashuleni, vyuoni, vijijini, mijini, kwenye ujasiriamali,maeneo ya kazi, mitaani au kwenye majukwaa ya kidijitali tuwasikilize,tuelewe changamoto zao na kubuni suluhisho la pamoja"amesema Waziri Nanauka 

Ameendelea kusema kuwa Mwelekeo huu unaenda sambamba na msisitizo wa Mheshimiwa rais alipohutubia na kufungua Bunge la 13 tarehe 14 Novemba,2025,ambapo alielekeza taasisi za Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya ajira,ujuzi, uzalishaji,na matumizi ya teknolojia ili vijana wanufaike na fursa za uchumi wa sasa na wa baadaye. 

Amesema kuwa Serikali pia inaendelea kuweka misingi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050(Dira 2050), inayosisitiza ukuaji jumuishi unaoweka mwananchi katikati,ikijumuisha uwezeshaji wa vijana, upatikanaji wa ajira zenye staha, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, na matumizi ya sayansi na teknolojia kama nguzo za mageuzi ya uchumi.Aidha, amesema Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030 imeweka dhamira ya kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni 8 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kwa kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji, na kukuza sekta zenye fursa kubwa kwa vijana.

Amesema kuwa sanjari na misingi hiyo,Serikali inaendelea kushughulikia changamoto kuu zinazowakabili vijana ikiwemo ukosefu wa ajira na ajira zisizo rasmi zisizo na tija, upungufu wa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, na upungufu wa mitaji kwa vijana wajasiriamali na kampuni changa zenye ubunifu (startups). 

"Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imejipanga kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (Toleo la mwaka 2024) na kuhakikisha kuwa vijana wanaandaliwa vyema na wanapata fursa za kujiajiri na kuajiriwa." Amesema 

Mikakati yetu itaelekezwa katika maeneo 13 ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Sera hiyo,ikiwemo elimu na mafunzo ya ufundi stadi,uvumbuzi na ubunifu,uchumi wa kidijitali,ukuzaji wa ajira,ushiriki wa vijana wenye shughuli za kijamii na kiuchumi uzalendo na maadili,afya na ustawi,malezi na makuzi,taaluma ya maendeleo ya vijana,uongozi,usawa wa kijinsia,mazingira,na ujumuishwaji wa vijana wenye ulemavu.

No comments