Zinazobamba

Doyo: Kahama Haitabaki Maskini Katikati ya Dhahabu, Serikali ya NLD Itabadilisha Maisha ya Wanyonge Kupitia Uchumi Jumuishi

Kahama, Shinyanga

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake mkoani Shinyanga kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Soko la CDT, mjini Kahama.

Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Kahama, Mhe. Doyo aliwahakikishia wananchi kuwa serikali yake itajenga soko la kisasa litakalowawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa urahisi na usalama, bila changamoto za miundombinu duni kama zinavyowakabili kwa sasa.

Alifafanua kuwa soko hilo litakuwa na huduma muhimu kama maji safi na salama, umeme wa uhakika, na sakafu bora, ili kuhakikisha mazingira rafiki kwa biashara.

Aidha, Doyo alionyesha masikitiko yake kutokana na hali ya umasikini inayoendelea kuwakabili wananchi wa wilaya ya Kahama licha ya kuwa eneo hilo limebarikiwa kwa utajiri mkubwa wa madini, hususan dhahabu. “Wilaya hii imebarikiwa kwa madini ya dhahabu, lakini wananchi wake bado wanaishi katika lindi la umaskini. Tukipewa ridhaa ya kuongoza, tutahakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga,” alisema Doyo.

Mhe. Doyo alibainisha kuwa serikali ya NLD inalenga kujenga taifa lenye haki, usawa na maendeleo jumuishi, likiwa na wananchi huru, wenye maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maamuzi na shughuli za maendeleo ya kulijenga taifa lao.

Alisisitiza kuwa serikali yake itachukua hatua za haraka kutatua kero za wananchi wa Kahama na kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa wa kisasa na shirikishi, uchumi unaowanufaisha Watanzania wote bila ubaguzi wa kidini, kikabila, au kimkoa.

Doyo alisema dhamira yake ya kugombea urais ni kuunda serikali yenye uwajibikaji, inayosikiliza wananchi na kuweka vipaumbele katika sekta muhimu kama elimu, afya, ajira, kilimo, viwanda na miundombinu. “Tutapunguza matumizi yasiyo ya lazima, tukipunguza misafara ya magari ya rais, ununuzi wa magari ya gharama kubwa, posho na mishahara mikubwa ya wanasiasa hasa wabunge,  fedha hizo tutazielekeza kwenye huduma za kijamii na ujenzi wa miundombinu muhimu kama masoko ya kisasa.Katika muktadha huo, kwa nini wananchi wa Kahama wakose soko bora? Chagueni Doyo na wagombea wa NLD ili tulete maendeleo katika jamii yenu ya watu wa Shinyanga, na nanyi mfaidike na matunda ya rasilimali zenu,” alisisitiza Doyo.

Msafara wa kampeni wa Mhe. Doyo unaelekea Manyara, Kilimanjaro, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na Zanzibar.

No comments