Zinazobamba

UTAFITI WA CIP UNAONESHA MGOMBEA URAIS CCM ATAPIGIWA KURA KWA ASILIMIA 84.5 OKTOBA 29 MWAKA HUU.

Na Mussa Augustine.

Kituo cha Sera za Kimataifa Afrika (CIP–Africa)kimefanya utafiti unao onesha kuwa asilimia 84.5 ya walioshiriki kura ya maoni wameonesha kumpigia kura mgombea urais wa chama cha Mapinduzi (CCM).

Vilevile utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 3 watampigia kura mgombea urais wa Chama Cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA)na asilimia 3 kwa mgombea urais wa Chama Cha Wanachi(CUF),na asilimia 1.5 kwa mgombea wa Chama cha NCCR–Mageuzi,huku asilimia 8 wakisema kura yao ni siri.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo leo Oktoba 22,2025  jijini Dar es Salaam mbele ya Waandishi wa habari,Mkurungezi wa tafiti na uchapishaji CIP -Afrika,Thabit Mlangi asema kuwa kura hiyo ya maoni ilifanyika kati ya Septemba 30 hadi Oktoba 5, 2025 katika mikoa 19 ikiwemo 17 ya Tanzania bara na mikoa miwili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

"Utafiti huu ulilenga kupata taswira ya hisia za wananchi kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025"amesema Mlangi

Nakubainisha kuwa mikoa iliyoshiriki ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja,Kigoma,Kilimanjaro, Mara,Mbeya,Morogoro,Mtwara,Mwanza, Pwani,Ruvuma,Tabora na Tanga.

Mlangi amesema kwamba jumla ya wahojiwa wa utafiti huo ni 1,976 walioshiriki katika kura hiyo ya maoni, ambapo wanaume walikuwa 988 na wanawake 988,na kati yao,asilimia 29 walikuwa na umri kati ya miaka 18–25, asilimia 32 walikua na miaka 26–35, asilimia 13 wakiwa na miaka 36–45, asilimia 17 wakiwa na miaka 46–55 na asilimia 9 walikuwa na zaidi ya miaka 55.

Kwa upande wa elimu,amesema asilimia 14 walikuwa na elimu ya msingi, asilimia 57 elimu ya Sekondari,asilimia 28 elimu ya chuo na asilimia 1 walikuwa na elimu nyingine.

Aidha amesema kuwa utafiti  huo ulitumia mfumo wa sampuli nasibu, unaotumika kisayansi duniani,unaosaidia kuongeza usahihi wa matokeo kwa gharama nafuu na kutoa fursa sawa kwa washiriki wote.
Akizungumzia mwelekeo wa kisiasa na ushiriki amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 81 ya washiriki wanajiona kuwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa, huku asilimia 19 wakisema hawana ufuatiliaji wa karibu wa kisiasa,na kati ya wafuatiliaji hao,asilimia 43 walikuwa wanawake na wanaume ni asilimia 57.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa utafiti na uchapishaji CIP amesema kuwa asilimia 53 ya waliohojiwa walisema wamehudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa,na kati yao,asilimia 76 walihudhuria mikutano ya CCM,asilimia 15 mikutano ya ACT–Wazalendo, asilimia 2 CHAUMMA na asilimia 7 walihudhuria mikutano ya vyama zaidi ya kimoja.

Akizungumzia upande wa ushawishi wa Sera na ushiriki wa uchaguz amebainisha kuwa matokeo yanaonyesha kuwa asilimia 46 ya walioshiriki kura ya maoni wameshawishiwa na sera za vyama vya siasa,huku asilimia 54 wakionyesha kutoshawishiwa na sera hizo.

Halikadhalika Mlangi amesema kuwa kuhusu ushiriki wa uchaguzi,asilimia 83 wamethibitisha kuwa watapiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025.

Aidha kuhusu upande wa vipaumbele vya Wananchi warioshiriki katika kura ya maoni walitaja vipaumbele ambavyo wangependa rais ajaye avipe kipaumbele kuwa ni pamoja Maji asilimia 78, Elimu bora asilimia 78,Miundombinu ya Barabara na Madaraja  asilimia 69,huduma bora za Afya asilimia 63,Kupambana na rushwa kwa asilimia 60 pamoja na kuimarisha Demokrasia  kwa asilimia 47.

Amefafanua kuwa baadhi ya wananchi, hususani wa Ilala na Segerea, walionyesha hofu kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi miongoni mwa wanafunzi, wakimtaka rais ajaye kulipa kipaumbele suala hilo katika kulidhibiti.

Hata hivyo upande wa kura ya maoni kwa Wabunge na Madiwani amesema matokeo ya kura ya maoni kuhusu wagombea hao bado yanachambuliwa kutokana na mkanganyiko wa taarifa,ikiwemo kuwepo kwa ripoti zenye majina ya wagombea bila vyama na nyingine zenye vyama bila majina hivyo taarifa kamili inatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

Amehitimisha kwa kusema kuwa asilimia 91 ya washiriki wameridhishwa na namna Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inavyosimamia maandalizi ya uchaguzi mkuu hadi sasa, wakieleza kuwa inaonyesha uwazi na umakini katika mchakato huo.

No comments