Zinazobamba

TUZO ZA KIMATAIFA ZA UTALII KANDA YA AFRIKA NA BAHARI YA HINDI KUFANYIKA TANZANIA.


Mkurugenzi Mtendaji TTB Ephraim Mafuru 

*Watu zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya Nchi wanatarajiwa kushiriki.

Na Mussa Augustine.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tuzo za 32 za Kimataifa za Utalii kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi ambapo watashiriki watu zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Juni 11,2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Nchini(TTB) Ephraim Mafuru wakati akizungumza na Waandishi wa habari kufuatia tuzo hizo zitakazofanyika Juni 26 mwaka huu katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es salaam.

Aidha Mafuru amesema kuwa tuzo hizo zimeandaliwa kwa kushirikiana na Kampuni ya World Luxury Media Group ambapo tuzo mbalimbali zitatolewa kwa wadau wa sekta ya Utalii Kitaifa na Kimataifa huku akiwasihi wadau wa Sekta ya utalii Mkoa wa Dar es Salaam kuchangamkia fursa hiyo ikiwemo kutoa huduma kwa  wageni watakaoshiriki.

"Lengo la tuzo hizo ni kutambua mchango wa wadau wa utalii Duniani,ambapo kwa awamu hii Tanzania imepewa heshima ya kuandaa tuzo hizo,hatua hiyo itakua chachu kubwa kwa nchi yetu kuendelea kutangaza sekta ya Utalii Kimataifa nakuongeza mnyororo wa thamani kupitia TTB" amesema Mafuru.

Nakuongeza kuwa" kufanyika kwa  tuzo hizi nchini kwetu ni kutokana na jitihada zinazofanywa na  Rais Dk Samia Suluhu hassan kuifungua nchi kiuchumi,hivyo  tunapaswa tumpongeze Rais wetu,na ikumbukwe kwamba tuzo kama hizi ziliwahi kufanyika miaka ya nyuma lakini  hazikufanyika  kwa ukubwa kama ilivyo kwa sasa".

Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TTB ameongeza kuwa  kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa tuzo hizo kwa nchi za Afrika na Bahari ya Indi kumetokana na ushindi wa nchi ya Tanzania katika tuzo zilizopita kwani Tanzania iliongoza kwa kuwa na tuzo tano,ikizishinda nchi nyingine za Afrika.

"Mkutano wa tuzo kama hizi  ulifanyika mwaka 2024 Mombasa Kenya,ambapo  Tanzania ilishinda tuzo tano ambapo Bodi bora ya utalii Afrika ilichukua TTB,kivutio bora cha utalii Afrika ilikuwa Mlima Kilimanjaro,hifadhi Bora ya Taifa  Afrika ilikuwa Serengeti,pamoja na tuzo ya kivutio bora cha safari Duniani,mafanikio haya yametokana na kazi kubwa inayofanywa na ikiongozi wetu Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan",amesema.

Aidha amefafanua kuwa kampuni 38 kutoka Sekta binafsi na zingine 12 kutoka Serikalini zitashiriki  katika tuzo hizo,huku akibainisha kuwa TTB itaendelea kuweka mikakati bora ya kuifanya mikutano mikubwa ya utalii iendelee kufanyika Nchini Tanzania na kutangaza vivutio vya utalii ili kuwezesha kuogeza idadi kubwa ya watalii nchini humo.
Mkurugenzi Mtendaji hoteli ya Johari Rotana Ahmed Said.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli ya Johari Rotana ambayo ndio mshirika mkubwa wa kutoa huduma kwa wageni watakao shiriki tuzo hizo Bw.Ahmed Said amesema kuwa  hoteli yake  imejipanga vyema kuhakikisha inatoa hiduma bora kwa wageni wote watakaofika kwenye tuzo hizo.
Mkurugenzi Masoko hospitali ya Shiffaa Victoria Tarimo
Naye,Mkurugenzi wa Masoko kutoka hospitali ya Shiffaa Bi.Victoria Tarimo amesema hospitali hiyo imejipanga  kuhakikisha inatoa huduma za afya kwa kiwango cha kimataifa kwa wageni watakaopatwa na changamoto za kiafya wakati wa tuzo hizo.

"Hospitali ya Shiffaa tumejipanga vizuri na tunavifaa vya kisasa kabisa kwa ajili ya kuwahudumia wageni na tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha tunawapa huduma nzuri kwani tuna wataalam wa kutosha lakini pia tutakuwa na gari la wagonjwa kwa ajili ya dharura",amesema.

Amesema Hospitali hiyo imejipanga kusapoti agenda ya Rais Dk Samia ya utalii tiba(Medical Tourism)kwa vitendo.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa Tuzo hizo zilianzishwa  mwaka 1993 lengo likiwa ni kutambua mchango wa wadau waliopo katika sekta ya utalii katika maeneo mbalimbali Duniani.

No comments