HESLB YAFUNGUA DIRISHA LA UOMBAJI WA MIKOPO YA ELIMU YA JUU KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026.
*Yawasisitiza Wanafunzi,Wazazi na Walezi kupitia miongozo ya Mikopo ili wajaze fomu kwa usahihi.
Na Mussa Augustine.
Taarifa hiyo imetolewa leo Juni ,19,2025 Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Dkt. Bill Kiwia wakati akizungumza na Waandishi wa habari nakubainisha kuwa dirisha hilo limefunguliwa tangu Juni 15,2025 nakuwataka Wanafunzi,Wazazi na Walezi waipitie miongozo ya Mikopo hiyo iliyopo kwenye tovuti ya Bodi hiyo www.heslb.go.tz ili waweze kujaza fomu zao za maombi kwa usahihi.
Aidha amesema kuwa katika mwaka wa masomo 2025/2026,Serikali imetenga kiasi cha shilingi Tsh Bilioni 917 kwa ajili ya kutoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wanaojiunga na Vyuo vya kati na vya elimu ya juu nchini,ambapo itawanufaisha wanafunzi 252,773,kati yao takribani wanafunzi 88,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza.
Aidha Dkt.Kiwia amedai kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Serikali imetumia kiasi cha shilingi trioni 2.7 kwa ajili ya kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu.
"Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 lipo wazi toka Juni 15, 2025 hadi Agosti 31 mwaka huu,HESLB imejipanga kutoa huduma kwa waombaji mikopo kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 0736 66 55 33 na kupitia ujumbe wa WhatsApp tu kwa namba 0739 66 55 33 kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni."amesema Dkt.Kiwia
Akizungumzia kuhusu Ruzuku ya Samia Scholarship,Dkt.Kiwia amesema kwamba wanafunzi zaidi ya mia saba(700) waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi watanufaika na ruzuku hiyo huku akiwataka Wanafunzi,Wazazi na Walezi kupitia miongozo iliyochapishwa kwenye tovuti ya Bodi hiyo waweze kujaza fomu kwa usahihi kwa ajili ya kuomba ruzuku hiyo.
"Naomba kuwasisitiza Wazazi na Walezi waanze kujaza fomu za maombi mapema,wasisubiri dakika za mwisho ambapo wanaweza wasikamilishe,kwani muda wa mwisho (Deadline) wa kutuma maombi unaweza ukawa umefika."amesema.
No comments
Post a Comment