Zinazobamba

CUF YASHAURI BUSARA ITUMIKE KUMALIZA KADHIA KANISA LA GWAJIMA

TUNASHAURI BUSARA ITUMIKE KATIKA KUMALIZA KADHIA YA KANISA LA UFUFUO NA UZIMA ILI KUMALIZA CHUKI:

CUF- Chama Cha Wananchi kinaumizwa na kuchukizwa na mambo yanavyoendelea katika Kadhia ya Kanisa la Ufufuo na Uzima (Kanisa la Askofu Gwajima) ambapo kwa hali iliyofikia, sasa busara isipotumika, maafa makubwa yanaweza kutokea baina ya Dola na Waumini wa Kanisa hilo.

CUF- Chama Cha Wananchi kinaamini kwamba busara ina nafasi kubwa ya kumaliza sintofahamu inayohusiana na Kadhia hiyo na bila ya kubainisha ni upande upi una makosa Kisheria katika suala hili, bado nafasi ya kulimaliza jambo hili na mambo mengine yanayovuta sana hisia za watu wengi kijamii kwa njia ya Suluhu inaweza kuleta matunda ya haraka kuliko 'kutunishiana misuli'.

CUF- Chama Cha Wananchi bado kina Kumbukumbu ya Kadhia baina ya Dola na Waumini wa Kiislam kwenye Sakata la Bucha la Nguruwe la Mbokomu Manzese mwaka 1993/94 na pia Sakata la Kufungwa kwa Msikiti wa Mwembechai baada ya Waumini kadhaa wa Kiislam kufyatuliwa risasi za moto na kuuawa mwaka 1998. 

Tunatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka na za makusudi kulimaliza Sakata la Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa njia ya Suluhu (kuliko Kisheria) kabla madhara makubwa zaidi hayajatokea na kuongeza dosari mbele ya jicho la Jumuiya za Kimataifa. 

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa 

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma 

CUF- Chama Cha Wananchi 

Juni 30, 2025```

No comments