Zinazobamba

MADEREVA BODABODA DAR ES SALAAM KUJIUNGA NA USHIRIKA.


Lengo ni kuwafanya wanufaike na kazi wanayoifanya kwa kuwaletea maendeleo.

Na Mwandishi wetu,

Dar es salaam.

Kwa muda mrefu, waendesha bodaboda katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,hasa wilayani Ubungo,wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya mikataba kandamizi hali inayowazuia kumiliki vyombo vyao vya usafiri licha ya kufanya kazi kwa bidii kila siku.

Mikataba hiyo, ambayo mara nyingi imekuwa ikiwapa masharti magumu ya malipo kwa muda mrefu bila dhamana ya kumiliki pikipiki hizo,sasa inakwenda kuwa historia. 

Hali hiyo ni baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando,kutangaza rasmi kuwa utaratibu huo unafutwa,na nafasi ya vijana kunufaika kupitia ushirika inawekwa wazi.

Akizungumza kwenye kongamano la ushirika lililofanyika jijini Dar es Salaam, Mhe. Msando alisema kuwa serikali inachukua hatua kuhakikisha vijana hawalazimiki tena kuingia mikataba isiyo na tija, bali wanapatiwa mikopo yenye masharti nafuu kupitia vyama vya ushirika na benki zinazoshirikiana na serikali.

“Mikataba mingi waliyonayo waendesha bodaboda ni ya kinyonyaji – mtu anakabidhiwa bodaboda kwa muda wa miezi 17 hadi 19, lakini akikosa malipo kwa muda mfupi ananyang’anywa pikipiki, huku fedha alizolipa zikiteketea. Hili haliwezi kuendelea,” alisema.

Msando alieleza kuwa Wilaya ya Ubungo sasa inatekeleza mkakati wa kuhakikisha kila bodaboda anapata leseni, elimu ya usalama barabarani, pamoja na mikopo halali inayomsaidia kumiliki chombo chake bila kupunjwa.

Aliwapongeza waandaaji wa kongamano hilo, hususan Benki ya Ushirika, kwa kujitolea kuonyesha njia mbadala kwa vijana kupitia mfumo wa ushirika, ambao unalenga kuwainua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Enerest Nyambo, alisema kuwa kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuimarisha usawa katika maeneo ya kazi, pamoja na kuondoa changamoto za ukosefu wa mikopo rafiki.

“Tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, na tunachukua kwa uzito mkubwa maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ambaye pia amemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Ndugu Albert Chalamila. Tumejipanga kutekeleza kwa wakati,” alisema Nyambo.

Amehimiza wanachama wa vyama vya ushirika kote nchini kuzingatia taratibu zinazohusiana na utoaji wa mikopo ili kuimarisha uaminifu na mafanikio ya mifumo hiyo.

No comments