Zinazobamba

SEKTA YA UTALII INAZIDI KULETA MAFANIKIO MAKUBWA.

Na Mussa Augustine

 Mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini kupitia Sekta ya Utalii yanaitangaza Tanzania kimataifa na kuitambulisha duniani kuwa ni nchi ya kwanza Afrika inayofanya vizuri kwa Utalii na ya sita dunia nzima.


Matamshi hayo yametolewa leo Oktoba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua onesho la nane la Utalii la kimataifa la  Swahili ( S!TE) linalofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini humo.

Dkt Mwinyi amesema mafanikio hayo ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ikiwemo miundombinu ya utalii na kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL)

Jitihada zingine ni  kuhamasisha mashirika mengine ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na nchi zenye masoko ya utalii, kujenga barabara na reli za kisasa zinazounganisha vivutio vya utalii, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, na kuimarisha huduma nyengine muhimu za utalii. 

Amesema kutokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza utalii nchini, Tanzania imeshuhudia idadi kubwa ya watalii wa kimataifa wanaotembelea sehemu mbalimbali za nchi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii. 

Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi amebainisha kuwa utalii ni sekta yenye ushindani mkubwa hasa kwa sekta ya utangazaji, bila kutangazwa kimataifa haiwezi kufikia malengo yaliyojiwekwa. 

Aidha  Dk. Mwinyi ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka sekta ya utalii, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 zinaonesha kuwa Tanzania imepokea idadi ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kufikiwa kwenye historia ya Tanzania na mapato yatokanayo na sekta hiyo, kufikia Dola za kimarekani bilioni 3.5.

Hata hivyo baadhi ya Wadau wa Sekta ya Utalii wameipongeza serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii ambayo imekua chachu ya Maendeleo kwa Taifa.


Hakuna maoni