Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam Omary Kumbilamoto akizindua Duka jipya la Mandasi Store lililopo Banana, Ukonga.

Mkurugenzi wa Duka la Mandasi Store Abdullahi Mandasi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Duka jipya la Mandasi Store, Banana, Ukonga jijini Dar es Salaam.

NA Mussa Austine

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam Omary Kumbilamoto amezindua duka jipya la kisasa la simu, vishkwambi na Laptop la Mandasi Store lililopo Banana, Ukonga jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Mei 2, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi huo Meya Kumbilamoto amempongeza Mkurugenzi wa Duka hilo Abdullahi Mandasi kwa uwekezaji huo kwani utafanikisha Watanzania wanaoishi maeneo jirani kupata simu kwa bei nafuu pamoja na kukopeshwa.

Hivyo Kumbilamoto amesema uwekezaji huo umesogeza huduma karibu na wananchi na kwamba wananchi hawatalazimika kwenda kununua simu, laptop na vishkwambi Karikoo na badala yake watapata huduma dukani hapo.

Meya Kumbilamoto ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi na watu wote wanaokopa simu katika maduka kuwa waaminifu kwa kulipa mikopo yao na sio kutafuta njia kukwepa, lengo ni kuhakikisha huduma hiyo inazidi kuwafikia watu wengi zaidi.

"Nimekuwa nikiitwa kufungua maduka mengi ya kuuuza simu lakini yamekuwa ya gharama kubwa lakini kwa mandasi ni tofauti nimekuta simu za bei ya kawaida ambazo kila mmoja ataweza kuzipata na hata kama hana hela taslimu anaweza kukopa na kulipa kidogo kidogo," amesema Meya Kumbilamoto.

Kwa upande wake Mandasi amesema tangu wameanza uwekezaji kwenye mikoa mbalimbali nchini wameshatoa mikopo ya simu zaidi ya elfu 26,000 ambapo wanamaduka 14 ndani ya mikoa 10 Tanzania nzima.

Baadhi ya mikoa hiyo  ni pamoja na Morogoro, Dar es Salaam, Shinyanga, Mwanza, Arusha, Iringa, Njombe, Dodoma.

Ameongeza kuwa kupitia uwekezaji huo, wametoa ajira kwa vijana wa Kitanzanzia 36 na wameahidi kuendelea kutoa ajira kwa kukuza huduma hiyo kwa kufungua maduka zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu bei ya Simu amesema zipo simu janja za kushilingi laki moja hadi milioni tatu, ambapo kwa mkopaji wa simu za gharama kubwa zaidi anatakiwa kuwa mtumishi wa umma ili kurahisisha ufuatiliaji wake.