Murugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.



NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limeainisha mafanikio liliyoyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Shirika.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amesema katika kipindi hicho shirika limeweza kuanzisha huduma ya usafirishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda kwa kutumia mabehewa maalumu ya ubaridi.

Kadogosa ameongeza kwamba Shirika limeafanikiwa kupokea jumla ya mabehewa 62 ya abiria na vichwa vinne (4) kwa ajili ya SGR na mabehewa mapya 22 kwa ajili ya reli ya zamani - MGR.

Hata hivyo Kadogosa amebainisha kuwa Shirika limepata mafanikio kuanzia 2016/2017 hadi 2021/2022 ambapo ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kurejesha huduma ya usafiri katika njia ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha iliyokuwa imesimama kwa zaidi ya miaka 30 na kufanikisha ukarabati wa njia ya reli ya Port bell hadi Kampala nchini Uganda.

Mengine ni kurejesha biashara kati ya Tanzania na Uganda ikiwemo usafirishaji wa mafuta, chakula (WFP), na bidhaa za viwandani, kuongeza vitendea kazi kwa Ununuzi wa vichwa vya treni vitatu, mabehewa ya mizigo 44, ukarabati wa mabehewa ya mizigo 240 na kuundwa upya kwa vichwa vya sogeza saba na ununuzi wa vitendea kazi vitakavyotumika katika uendeshaji wa reli ya kisasa.
Mkurugenzi Mkuu Kadogosa ameongeza mafanikio mengine kuwa ni kuendelea na ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge na matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya ukusanyaji mapato na ukatishaji tiketi; na Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika usafirishaji wa mizigo kwa mabehewa yao.

Kuhusu manufaa kwa wafanyakazi, ajira na mafunzo, Kadogosa ameeleza kwamba Shirika limeendelea kufanya maboresho katika usimamizi wa Rasilimali Watu ikiwemo kuhuisha mifumo mbalimbali ya kiutumishi kama Muundo wa Utumishi na Mishahara, Kanuni za Utumishi za Shirika na Mpango wa Motisha Kanuni za Malipo ya Posho yenye lengo la kuboresha mazingira ya kazi wezeshi kwa wafanyakazi kuweza kuzalisha kwa tija.

Halikadhalika amesema hadi kufikia mwezi Machi, 2024, Shirika limetoa Jumla ya ajira 1,121 za kudumu na mikataba zimetolewa ndani ya Shirika la Reli, hiyo ikikwa ni ajira 820 za kudumu na ajira 301 za mkataba. Watumishi 2,334 wamepandishwa vyeo na kubadilishwa kada kati ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwamba Jumla ya watumishi 1,373 wamehudhuria mafunzo ndani ya nchi na nje ya nchi, hii ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uendeshaji wa mradi wa treni ya kisasa (SGR). Shirika limefanikiwa kulipa madeni ya watumishi na mifuko ya hifadhi ya jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 54.326.