Zinazobamba

Mwenyekiti Bakwata agawa futari kwa makundi maalum dar

 

Na Mwandishi wetu

Mwenyekiti  wa Halmashauri Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Dar es salaam Sheikh Hussein Afif Al Azhary amegawa futari kwa familia 150 za makundi maalum yakiwemo walemavu wa macho na viziwi.

Akizungumza na waandishi wa habari waliohudhuria katika zoezi hilo, Sheikh Afif alisema wameweza kugawa futari kwa familia 70 za walemavu wa macho.

Aidha kwa upande wa viziwi, Sheikh Afif alisema wamefanikiwa kukabidhi futari kwa familia 80 na kufanya jumla ya wanufaika kuwa 150.

“Kila kifurushi kimoja kina mafuta ya kula lita 3, maharagwe, ngano, mchele, ofisi yangu imeratibu jambo hili na limekwenda vizuri kila mtu amefurahi,” alisema Afif.



 

Sheikh Afif ambaye ni muhitimu wa Chuo Kikuu cha Al-azhar cha Jijini Cairo, Misri mwaka 2013 alisema wahisani wamefurahishwa na ugawaji wa futari na kuahidi kuendelea kutoa misaada hiyo siku za usoni.

Kwa upande wao wanufaika wa futari hiyo, wameshukuru kupatiwa msaada na kuwaomba wadau wengine kutoa ili wapate fadhila za Allah

Sheikh Afif amedhamiria kuleta mabadiliko katika jiji la Dar es salaam hasa kulifanya baraza la mkoa kufahamika vizuri katika sekta za elimu, uchumi na afya.

Hapo awali Mkoa wa Dar es salaam ulionekana kumezwa na ofisi ya Makao Makuu ya Bakwata kiasi kwamba waislamu wanashindwa kutofautisha vitu vya baraza la mkoa na vile vya makao makuu.

Sheikh Afif ambaye ndiye Mwenyekiti mdogo kuliko wote wa kuchaguliwa, akiwa na miaka 35, alisema ofisi yake inafanya kila linalowezekana kuwaletea mabadiliko waislamu wa Dar es salaam, jiji lenye waislamu wengi.



Hakuna maoni