Mkuu wa wilaya apalilia umuhimu kamati za maadili mahakamani
Mkuu wa Wilaya
ya Songea, Mhe. Pololet Mgema akifafanua jambo alipokuwa anaongea na Jaji Mkuu
wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 ofisini kwa
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akieleza jambo alipokuwa ofisini kwa
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akiwa katika ziara ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya
Songea
Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya
Songea, Mhe. Pololet Mgema amewashauri Watanzania kutumia Kamati za Maadili za
Mahakama ya Tanzania kutatua malalamiko waliyonayo dhidi ya maafisa wa Mahakama
pale wanapohisi hawakutendewa haki wanapotafuta huduma za utoaji haki mahakamani.
Akizungumza na Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma walipokutana Ofisini kwa Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma leo tarehe 3 Machi, 2022 katika siku yake ya mwisho ya ziara ya
kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea Mhe. Mgema amesema kuwa mbali na uwepo wa
Mahakama ambayo ndiyo inayotoa haki, kuna Kamati za Maadili za Mahakama ambazo
husikiliza malalamiko dhidi ya maafisa wa Mahakama.
“Mkuu wa Mkoa
ameshatoa maelekezo kupitia kwa Mwanasheria katika ofisi (yake) aweze kwenda
kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani kuwafahamisha uwepo wa Kamati za Maadili za
Mahakama kwenye ngazi ya Wilaya na Mkoa ili kama kuna mwananchi anafikiri
amefanyiwa jambo ambalo anaona ni la ukiukwaji wa maadili aweze kutoa
malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya, kwa maana ngazi zile za Mahakama ya Mwanzo,
lakini pia kwa Mkuu wa Mkoa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwa maafisa
kwenye Mahakama anazozisimamia,” amesema.
Amesema kuwa Kamati
hizo ni chombo na silaha muhimu ambayo itasaidia kuondoa malalamiko kwa
wananchi. “Tunahitaji wananchi wakihudumiwa waone kwamba kile ambacho wamepata
ni stahiki yao. Vinginevyo, tutaendelea kushirikiana. Tunao ushirikiano mkubwa
kuanzia ngazi zile za chini mpaka kwa Jaji Mfawidhi,” Mkuu huyo wa Wilaya
alimweleza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Mgema
aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua nzuri iliyochukua kuboresha
miundombinu ya majengo ya Mahakama, ikiwemo kujenga Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki katika Kanda ya Songea, ambacho kitatoa huduma za kimahakama kutoka ngazi
ya Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.
“Hili la ujenzi wa
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki tunalisubiri kwa hamu sana. Jengo hilo litatatua
ile changamoto ya wananchi kusafiri mwendo mrefu kwenda Iringa kufuata huduma
za Mahakama ya Rufani,” alisema.
Awali, Mkuu huyo wa
Wilaya alimwomba Jaji Mkuu kuangalia uwezekano wa kuwa na huduma zote za utoaji
haki kupatikana sehemu moja ili haki iweze kupatikana kwa wakati na kwa gharama
nafuu.
Kathalika, Mhe.
Mgema alibainisha kuwa wanatambua mabadiliko makubwa ndani ya Mahakama, hasa
kwenye eneo la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
kusikiliza na kuamua mashauri mbalimbali. Alisema kuwa kama Serikali
wanaipongeza Mahakama kwa hatua hizo, ingawa bado kuna changamoto, lakini
anauhakika zitashughulikiwa.
“Tunashukuru sana
Jaji Mkuu kwa mchakato huo ambao umeuanzisha na umeshaanza kufanya kazi na
umeonyesha mafanikio chanya na makubwa. Kadri tunapoboresha huduma za utoaji
haki tunaifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani,” amesema.
Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 amemaliza ziara yake
ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Songea. Katika
ziara yake ya siku nne, Jaji Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya
ya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru. Katika maeneo yote aliyopitia,
Mhe. Prof. Juma amekagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa
miundombinu pamoja na kuongea na watumishi wa kada zote.
No comments
Post a Comment