Namna Maboresho ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta yatakavyochochea Ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano Tanzania
Na Mwandishi wetu
|
K |
atika kuboresha mazingira ya utoaji
huduma za mawasiliano nchini Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari wiki hii imetangaza maboresho ya Kanuni za Miundombinu ya Utangazaji Dijiti
na Kanuni za Leseni zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Maboresho ya Kanuni hizi pamoja na mambo mengine yanalenga kuboresha mazingira
ya uwekezaji na utoaji huduma nchini, na pia kupanua wigo wa upatikanaji wa
huduma za mawasiliano ya kielektroniki nchini.
Makala haya yananuia kuainisha maboresho
ya msingi yaliyofanywa kwenye Kanuni mbili ambazo ni Kanuni za Leseni, 2018 na Kanuni
za Miundombinu ya Utangazaji Dijiti, 2018. Lengo la mabadiliko haya ni kuendana
na mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA).
Sehemu ya Kwanza: Maboresho katika Kanuni za
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Leseni), 2022
Katika maboresho haya
mambo yaliyofanyiwa uboreshwaji ni kama ifuatavyo: -
Mosi; Kufuta ada ya masafa kwa wenye miundombinu ya utangazaji wa televisheni dijiti
(MUX) ili kuleta nafuu kwa wawekezaji kwenye eneo hili na kuwawezesha kupanua
wigo wa huduma za Mawasiliano pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora
za Mawasiliano;
Pili; kuainisha aina mpya ya leseni maalum kwa
watoa huduma wanaotengeneza bando za maudhui, kurahisisha utoaji wa leseni na
pia kuhimiza watengenezaji wa maudhui wa ndani kuandaa maudhui yanayohamasisha
ukuaji wa utamaduni wa Kitanzania na jamii inayoizunguka. Vilevile, kuongeza
ajira kwa vijana wanaovutiwa na uandaaji wa maudhui kwa kuzingatia kuwa hitaji
la soko katika miaka ya hivi karibuni limeongezeka kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo ongezeko la idadi ya watu.
Tatu; kubadili leseni ya vituo vya utangazaji
vya kijamii kuwa leseni ndogo. Lengo la maboresho haya haya ni kuchochea
uanzishwaji wa vituo vya utangazaji vya kijamii kwenye maeneo ya nchi
yasiyofikiwa au yanayopata huduma hafifu za utangazaji hasa wa redio. Hatua hii
pia itawezesha wananchi kunufaika kwa kupata huduma za maudhui ya utangazaji
yanayoakisi maisha na tamaduni zao katika maeneo husika. Aidha upatikanaji wa
leseni hizi utachukua muda mchache zaidi kwa kuwa mlolongo wa uchakataji wa
leseni umefupishwa tofauti na leseni kubwa ambazo zinahitaji mchakato wenye
mlolongo zaidi hadi hatua ya mwisho ya ukamilishwaji.
Nne; kupunguza ada za leseni ili
kuwezesha utoaji huduma nafuu na wenye viwango utakaosaidia kukuza ajira na
kuvutia watu wengi zaidi kuwekeza katika sekta ya Mawasiliano nchini.
-ano; kuainisha aina mpya ya leseni ya utangazaji kwa
maudhui maalum ya elimu ili kutoa nafasi kwa taasisi au mashirika yanayonuia
kutoa huduma ya elimu kutoa huduma hiyo kwa kuzingatia kwamba mazingira ya
utoaji elimu yamekuwa yakibadilika katika miaka ya karibuni kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo mkurupuko wa maradhi kama vile UVIKO-19 uliochagiza
kubadilika kwa modali ya uwasilishaji elimu maeneo mengi duniani, Tanzania
ikiwemo.
Sehemu ya Pili: Maboresho katika Kanuni za
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Redio na Televisheni), 2021
maboresho yafuatayo yamefanyika kwenye kanuni zinazoongoza huduma za utangazaji wa Televisheni na Redio, kama ifuatavyo, Mosi; Kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia kuchukua matangazo ya kibiashara (yasizidi dakika 5 kwa saa). Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, haikuruhusiwa chaneli za televisheni za kulipia kuweka matangazo ya kibiashara.
Wizara Pamoja na TCRA wanabainisha kwamba lengo
la kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia ziweze kuchukua matangazo ya kibiashara
ni kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji katika utengenezaji wa maudhui na
pia kuendana na uhalisia wa biashara ya chaneli za maudhui ya kulipia; kuhimiza
(promote) maudhui ya ndani na pia
kuwezesha wasanii wa ndani kutengeneza maudhui ya kulipia.
Nne; Kuruhusu chaneli za televisheni za kutazamwa bila kulipia (Free to Air) zioneshwe bila kulipia katika visimbuzi vyote nchini pasipo kujali ni vya kulipia au la. Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, chaneli za kutazamwa bila kulipia (Free to Air) hazikuruhusiwa kuoneshwa katika ving’amuzi vya kulipia nchini. Lengo la maboresho katika eneo hili ni kuongeza wigo wa mapato kwa watoa huduma wa chaneli za kutazamwa bila kulipia; kuongeza wigo wa ufikiwaji wa habari kwa wananchi kwani kwa maboresho haya kila king’amuzi kitaweza kuonesha chaneli zote, za kulipia na zisizo za kulipia.
Aidha hatua hiyo ya kuruhusu visimbuzi vyote kubeba chaneli za bila kulipia kunaongeza na kuwezesha uhuru wa watazamaji kuchagua chaneli watakazo kirahisi; pia itawezesha kutatatua changamoto ya mtumiaji kulazimika kumiliki kisimbuzi zaidi ya kimoja.
Mabadiliko mengine kwenye Kanuni hizi ni yanayoruhusu
chaneli za televisheni za kulipia kurusha matukio mbashara (live events) yakiwemo matukio ya kitaifa
kama vile hotuba za Viongozi Waandamizi wa Taifa. Kabla ya marekebisho haya chaneli
za kulipia hazikuruhusiwa kurusha matukio mbashara.
Sehemu ya Tatu: Maboresho katika Kanuni za
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Simu na Intaneti), 2021
Katika Kanuni hizi
mambo kadhaa yamefanyiwa maboresho na marekebisho kama ifuatavyo Mosi;
Kwanza ni kuboresha mfumo
wa leseni kwa kuainisha leseni ya Vituo vya Kuhifadhi Taarifa (Public Data Centre Licence). Maboresho
haya yanalenga kuongeza wigo wa uwekezaji katika huduma za mawasiliano hasa
katika masuala ya kuhifadhi taarifa kutokana na ongezeko la huduma mtandao kama
vile cloud computing services. Pili; kuainisha leseni kwa ajili
ya vituo vya maingiliano ya mtandao (Internet
exchange Points). Maboresho haya yatawezesha kuainisha vigezo vya kiufundi
vya miundombinu ya vituo vya maingiliano ya mtandao (Internet exchange Points).
Eneo la tatu ni, kupunguza ada za
masafa ya mawasiliano ya redio ili kuhimiza upelekaji
wa mtandao (network expansion) katika maeneo mengi zaidi nchini. Mabadiliko
haya yanaendana na Dira ya Maendeleo ya 2025 inayolenga kuhakikisha ufikishwaji
wa huduma za TEHAMA kwa wananchi wote. Maboresho ya nne yanahusisha kupunguza ada ya vituo vya mawasiliano ya
redio kutoka dola 3,000 na kuwa dola 100 kwa kituo, ili kuongeza kasi ya
usambazaji wa intaneti yenye kasi nchini hasa maeneo yasiyofikiwa kirahisi na
miundombinu iliyopo.
Tano; kuainisha ada kwa ajili ya mawasiliano ya simu kwa njia ya setilaiti
ili kuongeza udhibiti wa huduma za mawasiliano ya simu kwa njia ya setilaiti.
Sita; kuondoa ada ya usajili kwa madishi ya mawasiliano ya redio ili kuongeza
usambaaji wa huduma. Saba; kupunguza ada za madishi ya mawasiliano ya redio(VSAT)
kutoka dola 3,000 na kuwa dola 60 ili kuhimiza matumizi ya VSAT na pia
kuchochea uwekezaji kwenye eneo hili.
Nane; kutofautisha kati ya leseni ya
kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki kwa mafundi wakubwa na
wadogo. Mabadiliko ya tisa yanahusu kupunguza ada mbalimbali za leseni, ili
kupunguza mzigo wa ada kwa watoa huduma na kuhimiza uwekezaji zaidi na mwisho kuongeza
aina mpya ya leseni ndogo kwa ajili ya huduma mtandao, ili kutambua huduma mpya
za mtandao na kuweka mazingira wezeshi kiudhibiti.
Maboresho ya Kanuni ni suala muhimu katika kuhakikisha
utoaji wa huduma za mawasiliano unaendana na mabadiliko ya teknolojia na
uhalisia wa mazingira yaliyopo, ambapo dhamira ya Serikali ni kuendelea kufanya
maboresho ya Kanuni kila itakapohitajika kwa kuzingatia kuwa; teknolojia
inabadilika kila mara kama mkondo wa maji unavyobadili njia zake kila mtiririko
unavyosonga.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari kwa Pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanatarajia
kuona wadau wa sekta ya mawasiliano wakiendeleza ushirikiano madhubuti ili
kuendelea kuijenga Tanzania yenye huduma bora za mawasiliano ambazo ni chachu
ya maendeleo ya nchi yetu katika kujenga Uchumi wa Kidijitali.
Visimbuzi vyote sasa ruksa kubeba chaneli za bila kulipia;
· Chaneli za televisheni za kulipia ruksa kubeba matangazo; na
· Punguzo la ada ya leseni kuleta neema kwa watoa huduma na watumiaji.
Makala hii imetayarishwa na Kitengo cha
Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
No comments
Post a Comment