Zinazobamba

VIONGOZI NA WANANCHI WA KATA YA MAJOHE WAFURAHISHWA NA BUNGE LA JAMII LILILOFAYIKA KATIKA KATA YAO.

TGNP kwa kushirikiana na kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Majohe wametakiwa kuwa na Bunge endelevu la jamii, ili kuweza kuibua changamoto na kufahamishana mambo mengi yakimaendeleo katika kata hiyo kati ya viongozi na wanachi wao.

Diwani wa kata ya Majohe  Mh. Mohamed Sangonde Akitoa majibu kwa wananchi wake mapema jana katika bunge la jamii lililofanyika kata Majohe jijini Dar es salaam.

Hayo yameelezwa na Diwani wa kata ya Majohe Mh. Mohamed Sangonde mapema jana Disemba 31, 2021 katika Bunge la jamii lililofanyika katika kata hiyo likiwakutanisha viongozi wa kata, mitaa Pamoja na wananchi wao ili kuweza kupena elimu na taarifa mbalimbali za kimaendeleo katika kata hiyo.

Diwani huyo amesema kuwa amefurahishwa sana na Bunge hilo lililofanyika katika kata yake kwani limekuwa ni Jukwaa zuri la kuwakutanisha wanachi na viongozi wao na kuweza kuhoji mambo mbalimbali katika kata yao na viongozi kuweza kutoa majibu ya moja kwa moja kwa wananchi wao.

Aidha diwani huyo amesema kuwa mpaka sasa kata ya Majohe imepata fedha takribani shilingi Milion miambili na hamsini ( 250,000,000/= ) kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kata hiyo.

Ameendelea kwa kusema kuwa wanamshukuru Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kwani wampatiwa madarasa kumi katika kata hiyo ambapo mpaka kufikia tarehe 17 januari 2022 madarasa hayo yataanza kutumika, Kwani ujenzi wake utakuwa umekamilika kwa asilimia mia ikiwa tayari mpaka madawati kwa ajili ya wanafunzi watakao fanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba.

Mwenyekiti wa kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Majohe Bi. Amina Nassoro akiwakaribisha wageni katika Bunge la jamii mapema jana jijini Dar es salaam.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Majohe Bi. Amina Nassoro amesema kuwa wao kama waandaaji wa Bunge hilo wameweza kuwaalika wananchi kutoka mitaa yote ya kata ya Majohe ikiwemo mtaa wa Kichangani, Viwege, Rada, Mji mpya Pamoja na Kivule.

Ameongeza kuwa mpaka kuleta bunge mtaani hapo walianza na kufanya utafiti mdogo kwa wananchi kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu kama kushiriki katika mikutano ya kuibua ya serikali za mitaa, kuhusu mipango mbalimbali ya serikali ikiwemo MTAKUWA na imeonekana wananchi wengi hawashiriki na hata hizi kamati mbalimbali za mitaa yao hawazijui kabisa.

Ameendelea kusema kuwa wamepata Faraja kubwa kwani wananchi wameweza kupata majibu sahihi ya maswali yao kupitia viongozi wao, lakini wameelekezwa ni wapi mahali sahihi pa kupeleka malalamiko yao Pamoja na kesi mbalimbali za ukatili wanazokutana nazo huko katika mitaa yao.

Kwa upande wake mkazi wa kata hiyo Bw. Abdul Kasembe amesisitiza kuwepo na nguvu ya Pamoja kwa viongozi Pamoja na wananchi wao, kwani hii itasaidia kupata utatuzi wa changamoto kwa wakati endapo kutakuwa na ushirikiano kwa maana kiongozi peke yake hawezi kumaliza matatizo yote bila kushirikisha wananchi wake.

Naye Tabu Ally mkazi wa kata hiyo ameonyesha mfano wa nguvu za Pamoja kwa kushirikiana na wananchi wenzake wameweza kununua magogo na kujenga kivuko cha muda wakati wakisubiri diwani atakapoleta karavati aliloahidi wakati wa kampeni.


PICHA ZA MATUKIO...

Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Majohe ambaye pia ni Spika wa bunge la jamii kata ya Majohe Bi. Lucia Isack Ngoma  akiongoza Bunge hilo.
Abdul Kasembe mkazi wa kata ya Majohe mtaa wa Kivule akitoa yake ya moyoni katika Bunge la jamii lililofanyika kata ya Majohe jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Majohe wakifuatilia Bunge kwa umakini mkubwa.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia Bunge la jamii.
Mkazi wa kata ya Majohe Bi. Tabu Ally akiwasilisha hoja yake katika Bunge la jamii.
Washiriki kutoka mitaa mbalimbali ya kata ya Majohe wakifuatilia Bunge la jamii.
Baadhi ya wananchi na watoto wa kata ya Majohe wakifuatilia bunge kwa umakini.
Bunge likiendelea.

No comments