Zinazobamba

TAASISI YA WAJIKI YAFIKISHA KAMPENI YA SAFARI SALAMA BILA RUSHWA YA NGONO WILAYA YA TEMEKE

Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) inayojihusisha na utetezi wa haki za wanawake pamoja na Watoto imetembelea kata ya Mbagala kuu jijini Dar es salaam kuonana na viongozi wa kata hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIKI Janeth Mawinza na jopo lake wakimkabidhi Mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga rushwa ya ngono, Afisa Maendeleo wa kata ya Mbagala kuu.

Katika ziara hiyo iliyofanyika novemba 8, 2021 ikiongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Bi. Janeth Mawinza yenye lengo kuu la kufikisha kampeni ya "Safari Salama bila rushwa ya ngono kwa wasichana na wanafunzi" katika wilaya ya Temeke  ambapo itaanza katika kata ya Mbagala kuu.

Aidha Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo amesema kuwa wameendesha kampeni hiyo kwa miaka kadhaa, ambapo mwanzo walianza na wilaya ya Kinondoni, wakaenda Ilala na sasa wanaanza na msimu mpya kwa wilaya ya Temeke.

Ameongeza kuwa kampeni hii ni shirikishi kwani wameamua kuwatumia watu wanaohushishwa na vitendo hivyo vya ukatili wa kingono kuwatumia kutoa elimu kwa wenzao baada ya wao kupewa mafunzo na shirika hilo.

“Tumeamua kuwatumia madereva wa Daladala, Bajaji na Bodaboda kwa kuwa wao ndio watuhumiwa wakubwa wa kuwarubuni wanafunzi na wasichana kwa kuwaomba rushwa za ngono ili waweze kupandisha katika vyombo vyao vya usafiri, na hii tumetumia dhana ya kusema mchawi mpe mwanao akulelee.”amesema Janeth Mawinza

Ameendelea kwa kuongeza kuwa madereva hao wamekuwa wakifanya nao kazi kwa kuzunguka maeneno mbalimbali kama mashuleni, kwenye vituo vya mabasi na majumbani, ili kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kuachana na suala zima la rushwa ya ngono Pamoja na madhara yake kwa ujumla.

Wakati wakisubiri kuja kuzindua kampeni hiyo rasmi katika kata ya Mbagala kuu Mkurugenzi huyo akiwa na jopo lake wakiambatana na Afisa maendeleo wa kata hiyo waliweza kutembelea kituo kimoja cha karibu na kuongea na vijana wa bodaboda juu ya madhara ya rushwa ya ngono kwao na kwa wanaowamba pia.

Mmoja wa madareva hao aliyefahamika kwa jila la Ally Seif Mapeto amesema kuwa amefurahishwa na elimu hiyo kwani ameweza kuongeza kitu kichwani, nakusema kuwa hata wao walikuwa wakitenda vitu hivyo bila wenyewe kujijua na sasa watakuwa wajumbe wazuri wa kuelimisha wenzao wenye tabia kama hizo waweze kuziacha.

Na mwisho ameitaka ofisi ya kata iweze kuwapokea vizuri watakapoleta kesi na maombi yao mbalimbali wasionekane wahuni kwa muonekano wao kwani wanataka kuisaidia jamii, Na pia wameutaka uongozi wa WAJIKI watakapokuja kuitambulisha kampeni hiyo rasmi basi waje na stika, Pamoja na mabango ya kutosha ya kuweza kubandika katika bodaboda zao ili elimu iweze kwenda mbali Zaidi.

Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza na kikosi kazi chake wakimuelezea Afisa Maendeleo wa Kata ya Mbagala kuu namna kampeni ya Safari salama bila rushwa ya ngono inavyoweza kufanya kazi.
Wajumbe wa WAJIKI wakisaidiana na Afisa Maendeleo wa kata ya Mbagala kuu kubandika Mabango katika Ofisi ya Serikali ya mtaa wa Mbagala kuu.

Kikosi kazi cha WAJIKI wakiwa na kikao kidogo na Diwani wa kata ya Mbagala kuu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIKI Bi. Janeth Mawinza kushoto akimkabidhi Diwani wa kata ya Mbagala kuu mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga rushwa ya ngono.
Diwani na Afisa Maendeleo wa kata ya Mbagala kuu katikati wakionyesha mabango waliyopewa na taasisi ya WAJIKI pembeni ni wajumbe wa shirika hilo.

Madereva wa Bodaboda wa Kituo cha Shule Mbagala kuu wakibandika mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga rushwa ya ngono.
Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIKI Bi. Janeth Mawinza Akitoa elimu juu ya madhara ya rushwa ya ngono kwa madereva wa bodaboda wa kituo cha shule kata ya Mbagala kuu.


Hakuna maoni