Serikali yaja na muongozo wa kusimamia kemikali hatarishi, wasafirishaji, wakala wa forodha wasifu hatua hiyo
Na Fatma Salum
Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
(GCLA) imeandaa mwongozo wa namna bora ya kusimamia mizigo hatarishi (dangerous
goods) zikiwemo kemikali hatarishi ili kuwa na utaratibu wa kisheria
utakaozingatiwa katika usimamizi, usafirishaji na uhifadhi wa kemikali hizo.
Hayo yamebainishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice
Mafumiko wakati akifungua kikao cha wadau wanaoshughulika na usimamizi wa
kemikali hatarishi kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kupitia, kujadili na kupokea maoni na mapendekezo ya kuboresha rasimu ya
mwongozo huo wa kusimamia mizigo hatarishi zikiwemo kemikali hizo.
Dkt. Mafumiko alieleza kuwa dhumuni kuu la kuandaa mwongozo huo ni
kuweka utaratibu na maelekezo ya namna bora ya kusimamia mizigo hatarishi
katika maeneo ya bandari, bandari kavu, viwanda, maghala pamoja na usafirishaji
wa kemikali hizo ambazo zisiposimamiwa kwa usahihi zinaweza kuleta madhara kwa
binadamu na mazingira.
“Mwongozo huu pia unabainisha makundi ya mizigo hatarishi , alama
za utambulisho wa mizigo hiyo (labelling) kulingana na tabia au sifa zake
pamoja na kubainisha utaratibu wa kisheria unaohitajika kwa kampuni au mtu
binafsi anayetaka kushughulikia au kusimamia kemikali hatarishi katika bandari,
viwanda, maghala au wakati wa usafirishaji wa kemikali hizo,” alisema Dkt.
Mafumiko.
Aidha Dkt. Mafumiko aliongeza kuwa uandaaji wa mwongozo huo
umezingatia nyaraka za kimataifa zinazosimamia, kushughulikia na kusafirisha
kemikali hatarishi na baadhi ya nchi ambazo nyaraka hizo zimetumika ni
Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani na Canada.
Pia kwa hapa nchini rasimu
ya mwongozo huo imeandaliwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na uzoefu wa wadau
mbalimbali katika kusimamia au kushughulikia mizigo hatarishi.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA),
Bw. Edward Urio ameipongeza Serikali kwa kuandaa kikao cha kujadili rasimu ya
mwongozo huo na kupokea maoni ya wadau ili kuhakikisha wanalinda usalama wa
binadamu na mazingira.
Pia Bw. Urio ameiomba Serikali kupanua wigo kwa kuongeza bandari
kavu za kutosha kwa ajili ya kuhifadhi mizigo hatarishi zikiwemo kemikali hizo
kwani zilizopo sasa bado hazikidhi mahitaji ukizingatia kuwa kuna ongezeko la
usafirishaji wa mizigo hiyo kupitia bandari zetu kwenda nchi jirani.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kusimamia na
kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na mizigo hatarishi haswa kemikali
hatarishi. Jitihada hizo ni pamoja na kutunga Sheria ya Usimamizi na Udhibiti
wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sheria namba 3 ya mwaka 2003 na kanuni
zake zilizofanyiwa mapitio mwaka 2020 ambapo sheria hii inasimamiwa na Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha
utekelezaji wa sheria hiyo na kanuni zake pia Mamlaka imekuwa ikiandaa miongozo
mbalimbali.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni