Zinazobamba

WANAHARAKATI WATAKA SOMO LA UKATILI WA KIJINSIA LIINGIZWE KWENYE MTAALA WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI.

Serikali imetakiwa kuongeza somo la ukatili wa kijinsia katika mitaala ya elimu kwa shule za msingi na sekondari, kwa kipindi hiki ambapo mitaala inaelekea kubadilishwa.

Mwanaharakati Selemani Bishagazi akitoa ufafanuzi wa jambo katika semina za GDSS.

Hayo yameelezwa na wanaharakati kutoka kata mbalimbali za jiji la Dar es salaam katika semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia duniani.

Akitoa wito huo kwa niaba ya washiriki wa semina za GDSS Selemani Bishagazi amesema kuwa serikali ni vema ikaweka somo la ukatili wa kijinsia mashuleni, ili kuwasaidia Watoto wajue viashiria na namna ya kukabiliana changamoto ya vitendo vya ukatili wakiwa bado wadogo.

Kwa kuendelea kukazia ameongeza kuwa watachangishana fedha wampe mtu mmoja apeleke malalamiko yao Bungeni Mjini Dodoma kwa kuwataka wabunge waliangalie suala hilo kwa umakini ikiwezekana kuweka sheria ya namna hiyo, na ikishindikana kila mmoja atalazimika kumpelekea hoja hiyo mbunge wake ili akaipiganie bungeni.

Ameongeza kwa kusema kuwa wao kama washiriki wa semina hiyo wanaanza mchakato wa kuandika barua kwa afisa elimu wa mkoa, kwa kumtaka auangalie vizuri utaratibu wa wanafunzi wa darasa la nne na kidato cha pili kukaa nyumbani kwa muda mrefu, hali inayosababisha Watoto kupata mimba za utotoni na kufanyiwa ukatili mwingine wa kijinsia wawapo majumbani.

Na mwisho amesema kuwa wamehamasishana kila mmoja kutengeneza ujumbe mzuri wenye kupinga vitendo vya ukatili na kutuma kwenye makundi ya whatsaap na sehemu nyingine, ili ujumbe uweze kusambaa kwa sehemu kubwa Zaidi nakupunguza vitendo vya ukatili katika jamii.

Mwanaharakati kutoka kata ya Kivule, Zahara Omary akiwasilisha kazi ya kundi lao.

Kwa upande wake mwanaharakati Zahara Omari kutoka kata ya Kivule ameitaka serikali kupitia mahakama kuweza kusikiliza kwa muda mfupi na kutoa hukumu mapema kwa kesi za ukatili wa kijinsia.

Lakini pia ameitaka serikali kupitia vyombo vyake vya usalama ikiwa polisi, mahakama, serikali za mitaa na mabaraza ya kata kuweza kuwalinda watoa siri Pamoja nakuweza kuwapa ulinzi.

Mwanaharakati Dora Michael akiwasilisha kazi ya kikundi chake mapema jana jijini Dar es slaam.

Naye mwanaharakati Dora Michael ameitaka serikali kuweza kupitia sheria ya ndoa na kuyafanyia kazi mapungufu yake, na bunge kuendelea kuweka sheria kali Zaidi kwa wale watakaobainika kutenda ukatili wowote wa kijinsia.

Kwa upande wake Afisa Programu Mwandamizi wa TGNP Joyce Mkina amesema haya wakati akitoa historia ya Maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani.

“Tunafahamu kuwa kila ifikapo Novemba 25 mpaka Disemba 10 dunia nzima inaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Na hii ni njia ya kuwaenzi wanawake watatu Wanaharakati waliouwawa kikatili na Mfalme wa visiwa vya Dominika tarehe 25 Novemba 1980 huko Amerika ya kusini.”alisema Mkina

Ameongeza kuwa mwaka 1999 Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha siku hiyo kuwa ni siku ya kimataifa ya kupinga ukatili wa kijinsia na dhuruma zote kwa wanawake ambapo, ambapo humo ndani kuna siku ya kupinga ukatili Duniani, Siku ya Ukimwi duniani, siku ya Haki za Binadamu n.k.

Mwanaharakati Selemani Bishagazi akitoa ufafanuzi wa jambo katika semina za GDSS jana Novemba 17 jijini dar es salaam.
Washiriki wakifuatilia mafunzo kwa umakini.
Muwezeshaji Wa Semina kutoka TGNP Dada Anna Kikwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi akichangia mada kwenye kundi lake wakati wa kufanya kazi za vikundi.
Washiriki wa GDSS wakifanya kazi za vikundi.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika kazi za vikundi.
Afisa Programu mwandamizi wa TGNP Joyce Mkina akito ufafanuzi kuhusu siku 16 za kupinga ukatili duniani.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja.

Hakuna maoni