Zinazobamba

TCRA YATOA LESENI 119 KWA WATOA HUDUMA ZA POSTA, DUKA-MTANDAO LAZINDULIWA

Na Mwandishi wetu, Dodoma


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  imetoa jumla ya leseni 119 kwa watoa huduma za Posta nchini na kuwapongeza kwa kutoa huduma kwa kuzingatia masharti ya leseni zao.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari wakati akiwasilisha salamu za TCRA katika uzinduzi rasmi wa Duka la Posta mtandaoni (Posta Online Shop), uliofanyika jijini Dodoma.

Aidha, amesema kuwa TCRA wakati wote iko tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya posta ili kuhakikisha huduma za posta zinakuwa za kisasa zinazokidhi mahitaji na matakwa ya wananchi katika zama za ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Amesema kuwa, matumizi ya teknolojia hasa ya Habari na Mawasiliano ni fursa ya kukuza biashara.

"Ni wajibu wetu kama wadau wa sekta ya Posta kuhakikisha kwamba tunashirikiana katika mambo muhimu ambayo yanaendelea, tumependekeza kuwa na wakati wa kushirikiana na wateja wetu katika sekta ya Posta kwa warsha ya nusu siku”
"amesema Dkt. Jabiri.

Ameongeza kuwa, watoa huduma za posta waliosajiliwa wamekuwa wakitoa huduma ndani ya nchi, Afrika Mashariki, Kimataifa na ndani ya miji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za posta na usafirishaji wa vipeto na vifurushi zenye uhakika wakati wote.

Katika maadhimisho hayo Shirika la Posta nchini limezindua wiki ya Posta na Duka la Posta mtandaoni linalomwezesha mtumiaji kuagiza na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi kwa utaratibu maalum uliowekwa na shirika hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA Mhandisi Kundo Andrew Mathew amesema kuwa ujio wa huduma za duka la Posta Mtandaoni utawasaidia wakulima, wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kisasa hatimae kuongeza tija.

"Duka la Mtandaoni tunalozindua leo ni matokeo ya ukuaji wa teknolojia; biashara mtandaoni ndio mwelekeo wa biashara duniani na inawezesha jamii kuhudumiwa kwa urahisi, kwa sasa wananchi hawataifuata Posta bali Posta itawafuata popote walipo"amesema  Naibu Waziri Kundo

Ameongeza kuwa mpaka sasa duka hilo la mtandaoni limesajili wafanyabiashara wapatao 300 ambapo bado usajili unaendelea.

Haya yanajiri kuelekea kilele cha Siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 9 na mwaka huu Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo jijini Dodoma.

Akizungumzia huduma hiyo, Kaimu PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo amesema kuwa, mtumiaji wa huduma za duka la posta mtandaoni sasa hatalazimika kusumbuka kupata bidhaa anazohitaji, kwani atachagua bidhaa aipendayo kwa njia ya mtandao na Shirika la Posta litamfikishia bidhaa hiyo popote alipo duniani.

"Mjasiriamali yeyote mwenye kitambulisho cha Mjasiriamali na Mfanyabiashara yeyote aliesajiliwa anaweza kujisajili na kuweka bidhaa zake kwenye duka letu mtandaoni" amesema Mbodo.

Aidha, amesema kuwa duka mtandao hilo linatumia lugha zaidi ya Ishirini ikiwemo Kiswahili hivyo kumwezesha mnunuzi, mjasiriamali na mfanyabiashara kuuza na kununua bidhaa zake popote duniani pasina kikwazo cha lugha.

Hakuna maoni