TEA KUSIMAMIA UANZISHWAJI NA UHUISHAJI WA MIFUKO YA ELIMU YA HALMASHAURI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati. I. Geuzye akiwasilisha nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma |
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa
Tanzania (ALAT), wakipata elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa na uanzishwaji
wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri katika banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA) jijini Dodoma.
Bi. Bahati Geuzye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA), akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa
Tarime Bi. Gimbana Ntavyo, mara baada ya kutoa nasaha zake kuhusu uanzishaji na
uhuishaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri katika Mkutano Mkuu wa ALAT wa
mwaka jijini Dodoma.
0 Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati. I. Geuzye (katikati) akiwa
amezungukwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) wakichukua mawasiliano yake mara baada ya kutoa nasaha zake kwa wajumbe
hao jijini Dodoma
Na Eliafile
Solla, TEA
Miundombinu bora ya elimu katika Halmashauri nyingi hapa nchini ni
changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya
kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo.
Kauli hii imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA) Bi Bahati. I. Geuzye, alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika
katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Awali ya yote Bi. Bahati alibainisha kwamba, Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA) inatambua umuhimu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
katika kuhamasisha na kuboresha mahusiano yao ya kiutendaji na Halmashauri za
Majiji, Manispaa na Miji kote nchini.
‘‘Kutokana na changamoto hizo za miundombinu bora ya elimu,
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo inaratibu na kusimamia Mfuko wa Elimu wa
Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), imeandaa utaratibu utakaowezesha Halmashauri zetu kuanzisha Mifuko
ya Elimu na kwa zile Halmashauri ambazo tayari zina mifuko hiyo tuna dhamira ya
kuihuisha na kuanza kuitumia kikamilifu’’, alisema Bi. Bahati.
Aliongeza kwamba, katika mwaka 2020 sheria ndogo ya uanzishwaji wa
Bodi ya Mfuko wa Elimu wa Halmashauri iliridhiwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana
wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na vile vile mwongozo wa uanzishwaji wa Mifuko
umekwishaandaliwa na kusambazwa kwa wajumbe hao wa mkutano wa ALAT.
‘‘Kazi iliyopo mbele yetu ni kutekeleza lengo kuu la kuanzisha na
kuhuisha Mifuko ya Elimu katika Hamlashauri zote nchini, moja ya mipango
inayolenga uboreshaji wa elimu katika maeneo wanayoishi wananchi’’ alibainisha
Bi. Bahati
Zoezi hili la uanzishwaji na uhuishwaji wa Mifuko ya Elimu ya
Halmashauri lina faida nyingi ikiwemo kuwezesha Halmashauri kukuza ushirikiano
wa jamii katika kuchangia miradi ya kipaumbele ya elimu; kuboresha, kuendeleza
na kukuza viwango vya elimu katika Halmashauri husika.
Vile vile mifuko hii itawezesha Halmashauri kutenga sehemu ya
mapato yake ya ndani kwa ajili ya miradi ya elimu ndani ya Halmashauri pamoja
na kuratibu upatikanaji wa michango kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali
na ya kiserikali, mashirika ya kidini na watu binafsi kwa ajili ya kusaidia
uendelezaji wa miradi ya elimu ndani ya Halmashauri hiyo.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni