Zinazobamba

TGNP YAWANOA WANAJAMII KUWEZA KUNUFAIKA NA RASILIMALI ZILIZO NDANI YA JAMII YAO

Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa TGNP Dada Anna Sangai akiwezesha katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanajamii kutoka vituo vya Taarifa na Maarifa.

Wanajamii wametakiwa kuamka na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Hayo yameelezwa mapema jana julai 15 na Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa TGNP Bi. Anna Sangai wakati akitoa mafunzo kwa baadhi ya vituo vya Taarifa na Maarifa vya mkoa wa Dar es salaam.

Akiongea katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyofadhiliwa na Chou cha COADY International kupitia mradi wake wa Engage: Woman Empowerment and active Citizen, wenye lengo la kuisaidia jamii kuweza kuzitambua na kuzitumia fursa mbalimbali walizonazo katika maeneo  yao kwa kutumia moduli ya ABCD.

Afisa huyo amesema kuwa moduli hiyo licha ya kuwasaidia wanajamii kuweza kutambua fursa mbalimbali ndani ya jamii yao, lakini pia itawasaidia kuweza kupigania usawa wa kijinsia ikiwa ni Pamoja na kuhimiza serikali kuweza kutenga bajeti yenye mlengo wa kijinsia.

Ameendelea kusisitiza kuwepo na bajeti yenye mlengo wa kijinsia kwa kuwa itakuwa ni bajeti inayolenga makundi yote lakini pia inahakikisha rasilimali fedha zinazokwenda kutumika kwenye miradi ya maendeleo zinatumika kama zilivyokusudiwa.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ya ABCD yamewakutanisha wanajamii kutoka katika vituo vya Taarifa na Maarifa Kipunguni, Majohe, Saranga Mabwepande, Mabibo na kivule ambapo vituo hivi vilifanyiwa ulagibishi mwezi wa tatu mwaka huu, Na hii ni kuendelea kuwajengea uwezo ili waweze kuendelea kutekeleza mpango kazi waliyouandaa baada ya mafunzo yaliyopita.

Aidha dada sangai ameendelea kwa kusema kuwa mafunzo haya pia ni fursa ya wanajamii hao kuweza kubadilishana uzoefu wakati wa utekelezaji mpango kazi huo, Kwa kushirikishana na kusaidiana endapo kituo kimoja kitakuwa kimekwama au kinapitia kwenye changamoto ama nyingine.

Na mwisho amemaliza kwa kusema kuwa matarajio yao baada ya mafunzo haya ni kwamba watakuwa wameweza kuzalisha walaghibishi wazuri na wengi ambao wataweza kuwa mabalozi wazuri wa kwenda kuwafundisha wenzao ambao hawajaweza kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa TGNP Dada Anna Sangai akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanajamii kutoka vituo vya Taarifa na Maarifa vya mkoa wa Dar es salaam.


Baadhi ya wanajamii wakisikiliza kwa umakini mafunzo ya ABCD.
Mshiriki kutoka kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni Fatma Abdulahman akichangia mada katika semina ya ABCD iliyoandaliwa na TGNP. 
Baadhi ya wanajamii waliyoshiriki mafunzo ya ABCD  yaliyoandaliwa na TGNP wakiwa katika kazi za makundi.
Mwanaharakati kutoka kituo cha taarifa na maarifa majohe Joseph Safari akitoa ufafanuzi wa jambo katika semina ya ABCD.
Semina ikiendelea


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

                                        

Hakuna maoni