Zinazobamba

MAKONDA AIPONGEZA CRDB KWA UBUNIFU WA KUTOA ELIMU YA FEDHA

*Azindua msimu wa nne wa kipindi cha Zogo Mchongo kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.


Na Mussa Augustine.

Benki ya CRDB imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi kupitia vipindi vya ubunifu hatua ambayo inaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi jumuishi na kuongeza uelewa wa kifedha kwa Watanzania.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Paul Makonda  Julai 22, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa msimu wa nne wa kipindi cha Zogo Mchongo,nakubainisha kuwa elimu ya fedha ni msingi muhimu wa kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu uwekezaji, biashara, matumizi na utunzaji wa fedha.

"Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeweka miongozo mbalimbali ya kuhimiza elimu ya fedha kwa wananchi, huku CRDB ikiwa miongoni mwa taasisi zilizofanikiwa kufikisha elimu hiyo kwa njia rahisi kupitia televisheni, mitandao ya kijamii na ushirikishwaji wa wasanii, wanamichezo na watengeneza maudhui," amesema Makonda.
Ameongeza kuwa, "Matumizi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii kusambaza elimu ya fedha yanatoa nafasi kwa wananchi wengi kuelewa fursa za kiuchumi, huku yakichochea ajira na kuongeza kipato kwa vijana wanaotumia vipaji vyao kutengeneza maudhui."

Waziri huyo amewashauri Watanzania kuacha kufuatilia taarifa zisizo na manufaa na badala yake kutumia muda kujifunza masuala ya fedha, biashara na uwekezaji ili waweze kunufaika na fursa zinazozalishwa na Serikali pamoja na taasisi za kifedha.

Katika hatua nyingine, Makonda amewaomba wananchi kujiandaa kikamilifu kuyatumia matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika nchini kama fursa za kuongeza kipato, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yatawezekana endapo elimu ya fedha itaendelea kuwafikia watu wengi zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema kuwa benki hiyo imebadili mkakati wake kutoka kuuza huduma za kifedha pekee na sasa inaweka nguvu kubwa katika kujenga jamii yenye maarifa ya fedha ili iweze kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya huduma za kifedha.

"Kipindi cha Zogo Mchongo ni sehemu ya mkakati wetu, ambapo kupitia msimu wa nne wananchi watapata elimu kuhusu uwezeshwaji wa kifedha kutoka benki ya CRDB ili waweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi," amesema Nsekela.


No comments