WATHAMINI WAASWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA MISINGI YA TAALUMA ZAO
| Dkt. Medard Geho (aliyesimama) akitoa elimu kuhusu uthamini wa mashine na mitambo kwa watalaam wa uthamini katika Mafunzo ya siku moja yaliyotolewa Jijini Dar es Salaam ili kuwajengea uwezo |
Na: Eliafile Solla
Katika
ukuaji wa uchumi wa nchi ya Tanzania, uthamini una nafasi maalum kama ilivyo
kwenye nchi zote zilizoendelea. Kauli
hii imetolewa Jijini Dar es Salaam na Dkt. Medard Lucas Geho kutoka White
Knights Investiment Analysts Co. Ltd, alipokuwa akitoa elimu kwa wathamini
kuhusu uthamini wa mitambo na mashine kwenye mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo
watalaam hao.
Dkt.
Geho alisema, Tanzania inavyoingia kwenye uchumi wa viwanda, ni lazima uthamini
ufanyike kwa kufuata uhalisia na misingi ya taaluma ya uthamini ili kusaidia usimamizi
mzuri wa mitambo na mashine kwenye viwanda, uzalishaji mzuri wa malighafi na
pia kusaidia viwanda kuongezeka.
Mafunzo
haya ya uthamini wa mitambo na mashine yameratibiwa na Bodi ya Usajili wa
Wathamini kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam wa uthamini ili kuunga mkono
juhudi za Serikali katika kuelekea uchumi wa viwanda. Pia Mafunzo haya yameendeshwa
kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa bodi ya usajili wa wathamini ambapo
tangia bodi hii ilivyoanzishwa, haya ndiyo mafuzo yake ya kwanza ya kuwajengea
uwezo wataalam wa uthamini.
‘‘Hata
katika nchi za Marekani na Ulaya, kuna wakati uchumi wao huwa unaporomoka
kutokana na suala zima la uthamini na hasa wakati wa kutoa mikopo kwa kuweka
rehani ya mali. Changamoto kama hizi zinatokea pale uthamini unapofanyika na
thamani kuonekana iko juu kisha baada ya kuchukua mkopo mali iliyowekwa rehani
inakuwa haiuziki na hivyo kusababisha hasara kwa Taasisi ama Shirika lililotoa
mkopo. Ni muhimu mara zote kuhakikisha uthamini uko sahihi na hii ndiyo sababu
tunatoa mafunzo ili kuwajengea uwezo wataalam wa uthamini hasa katika kipindi
ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda; alisema Dkt. Geho’’
Kwa
upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Wathamini Bibi Edith Ushiwa amesema,
mafuzo haya yametolewa kwa wataalam wa uthamini kama hatua ya awali ya
kuwaandaa wakati Tanzania ikielekea katika uchumi wa viwanda. Hii ni kutokana
na uhalisia kwamba, viwanda na mitambo ni vya gharama na hivyo ni lazima
uthamini wake uwe makini na ufuate misingi ya taaluma ya uthamini. Katika
uanzishwaji wa viwanda na ununuzi wa mitambo, wathamini watahusika kwa asilimia
kubwa kwenye kufanya uthamini wa gharama za uwekezaji na mitambo itakayotumika
kuendesha viwanda hivyo. Ushiwa aliongeza kwamba, uthamini ni dhana pana sana
na hivyo wameamua kutoa mafuzo kwenye kipengele cha uthamini wa mitambo na
mashine kwani kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuwa na uchumi wa viwanda.
Mafunzo
ya uthamini wa mitambo na mashine yaliyotolewa kwa watalaam wa uthamini, yatawasaidia
kuboresha kazi zao za uthamini na kugundua vipengele muhimu vya kuangalia
wakati wa kufanya uthamini katika mitambo na mashine na hasa kusimamia miongozo
ya taaluma zao kwa mujibu wa sheria ya uthamini.
No comments
Post a Comment