Zinazobamba

SCORPION AZIDI GONGA MWAMBA MAHAKAMANI,SOMA HAPO KUJUA

Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njetwe maarufu ‘Scorpion’ imeshindwa kuendelea kusikilizwa kwa mara ya nne mfululizo baada ya wakili wa utetezi kushindwa kufika mahakamani.

Wakili huyo, Juma Nassoro ameshindwa kufika leo, Alhamisi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa ajili ya kumtetea mteja wake, baada ya kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.

Wakili  Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga ameiambia Mahakama kuwa alipewa taarifa na wakili huyo kuwa alikuwa na kesi nyingine Mahakama kuu kwa Jaji Wambura.

“Mheshimiwa hakimu,  mshtakiwa yupo mbele ya mahakama yako lakini nimepata taarifa kutoka kwa wakili wake kuwa yupo Mahakama Kuu kwa Jaji Wambura mbapo anasikiliza kesi , hivyo tunaiomba Mahakama yako itoe ahirisho la mwisho na kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya  kuendelea na ushahidi”Alidai Katuga.

Hakimu  Mkazi  Flora Haule , anayesikiliza shauri hilo amekubalia ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 8, mwaka huu na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.