DC HAPI AWAONYA WATENDAJI KINONDONI,SOMA HAPO KUJUA
NA KAROLI
VINSENT
WATENDAJI na
viongozi wa Manispaa ya Kinondoni wametakiwa kujiepusha na ukusanyaji wa fedha
za wananchi bila kupata kibali cha Mkurugenzi wa manispaa ili kuepusha
migongano na ufujaji wa fedha za wananchi.
Aidha,
wametakiwa kuhakikisha wanatoa risiti za mashine za kielektroniki (EFD) kwa
kila michango halali wanayokusanya ili kupunguza malalamiko ya wananchi
kutopewa risiti wanapotoa michango.
Kauli hiyo
imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi wakati akiwa kwenye Kata ya
Makongo Juu ambako alitembelea kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na
kusikiliza kero mbalimbaki za wananchi.
Hapi alisema
kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakikusanya fedha bila utaratibu kutoka kwa
wananchi na kuzitumia kinyume na utaratibu hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma
maendeleo.
"Kama
viongozi mnataka kukusanya fedha za wananchi ni vema mkaomba kibali ili
yakitokea malalamiko tujuee yanatoka wapi na tunayashughulikia vipi. Huko
nilikopita nimekutana na kesi hizo wanakusanya michango, lakini haifiki,"
alisema Hapi.
Alisema zipo
kesi kadhaa za viongozi kutumia fedha za wananchi na hasa Wenyrviti wa serikali
za mitaa na baadhi yao wamekuwa wakiweka fedha hizo kwenye akaunti zao binafsi
badalaya ya akaunti za mitaa yao.
"Kama
wananchi wanataka kuchangia, waelekezeni utaratibu mzuri ambao hakutakuwa na
malalamiko alkini pia na nyinyi msije mkaingia doa kwenye uongozi wenu,"
alisema.
Katika hatua
nyingine, Hapi alitoa siku tatu kwa Kamati za Maendeleo za mitaa kuhakikisha
zimebandika taarifa za mapato namatumizi ya mitaa yao katika mbao za matangazo
ili kuweka uwazi.
Alisema
kamati hizo zina wajibu wa kuwasomea wananchi wao taarifa za mapato na
matumizi.
Hapi pia
alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepiga marufuku kutoa michango ya aina
yoyote, hivyo ikibainika wapo wakuu wa shuke ambao wanaenda kinyume na agizo
hilo watachukuliwa hatua za kisheria