ZITTO KABWE AMBANA RAIS MAGUFULI KWENYE SAKATA IPTL,AHOJI UKIMYA WAKE KWENYE UFISADI HUO,SOMA HAPO KUJUA
Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT Wazalendo,
Zitto Kabwe, ameendelea kumtaka Rais Magufuli kuchukua hatua dhidi ya
anachokiita ufisadi katika kampuni ya uzalishaji umeme ya IPTL, inayomilikiwa
na Kampuni wa PAP.
Tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani mwezi
Novemba mwaka 2015, Zitto amekuwa mstari wa mbele kumsihi na kumuomba Rais
Magufuli afanye maamuzi juu ya kampuni hiyo ambayo imekuwa ikilipwa milioni 300
kila siku bila kujali kama inazalisha umeme au la.
Kupitia mitandao ya kijamii, Zitto ameandika
"Rais John Magufuli ana fursa ya kihistoria kumaliza kabisa huu mtandao wa
wizi na utapeli uliodumu toka mwaka 1995. watanzania masikini na wanyonge
tutakuwa nyuma yake kwenye hili. Atende sasa."
Mnamo tarehe 21, Septemba 2016 Mhe. Zitto Kabwe
alimtaka tena Rais Magufuli aoneshe hasira zake dhidi ya hicho anachokiita
ufisadi mkongwe wa IPTL huku akieleza masikitiko yake juu ya kutochukuliwa kwa
hatua zozote hadi sasa.
Mhe. Zitto Kabwe ambaye amekuwa hachoki kulizungumzia
sakata hilo la IPTL amehoji ni nini kipo nyuma ya pazia, na ni nani mfaidika
hadi hatua zisichukuliwe, huku akitoa ushauri wa hatua zinazoweza kuchukuliwa
na mahakama kwa sasa.
"Mahakama Ina uwezo wa kurejea maamuzi yake kwa
kuitisha upya kesi zilizoamuliwa. Hivi hii Mahakama haioni suala la PAP
kumiliki IPTL na kuchota mabilioni ya fedha zilizokuwa Benki Kuu na kuendelea
kulipwa tshs 300m kila siku izalishe au isizalishe umeme? Ushahidi wote
ulionyesha utapeli wa Kimataifa uliofanywa na Harbinder Singh Seth lakini
kivuli cha uamuzi wa Mahakama umefanya matapeli hawa kuendelea kunyonya fedha
kutoka TANESCO. Huu mrija wa PAP/IPTL upo kinywani mwa The Chato Inc? Ama ni
jipu la mgongoni?". Alihoji Mhe. Zitto Kabwe