WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA QUALITY GROUP WABURUZWA MAHAKAMANI,SOMA HAPO KUJUA
Raia 14 wa India ambao wanafanya kazi Quality
Group iliyo chini ya Yusuf Manji leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya
kuwa na kibali.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Hati ya mashtaka, iliyosomwa na mwendesha Mashtaka,
wa uhamiaji Method Kagoma imewataja washtakiwa hao kuwa ni Rojat Surkar,
Jagadish Mamidu, Niladri Maiti, Sivarar Raja Sekaran, Mohammed Taher Shaikh,
Bijenda Kumar, Prasoon Kumar Mallik na Nipun Dinbandhu Bhatt.
Wengine ni Pintu Kumar, Anuj Agurwa, Varun Boloor,
Arun Kumar Kateel, Avinash Chandratiwari na Vikram Sankhala.
Akisoma hati ya mashtaka, Kagoma amedai kuwa,
Februari 13, mwaka huu, huko katika ofisi ya Quality Group Ltd iliyopo katika Wilaya
ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakiwa na viza
zilozoghushiwa za kufanyia kazi.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa siku na mahali
hapo washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakiishi nchini Tanzania
bila ya kuwa na kibali.
Kagoma aliongeza kuwa, Februari 13 mwaka huu, katika
jengo la Quality Group washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa
wakijihusisha na kufanya kazi katika kampuni hiyo kama washauri bila ya kuwa na
kibali cha kufanya kazi nchini.
Hata hivyo, washtakiwa hao ambao wanatetewa na
mawakili watatu, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo wamekanusha kujihusisha na
tuhuma hizo na wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Mahakama iliwaamuru washtakiwa hao kuweka dhamana ya
milioni tano kila mmoja na kuleta mdhamini mmoja kila mtu atakayeweka
kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, mwaka huu